ALICHOKIFANYA DIAMOND NIUUNGWANA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, April 27, 2020

ALICHOKIFANYA DIAMOND NIUUNGWANA

Charles James, Michuzi TV
SADAKA! Tena Sadaka kubwa anaitoa kwenye muda ambao kweli watu waliihitaji. Huku Corona, huku Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ukiwa umeanza. Hujanielewa!.

Supastaa na Rais wa Wasafi, Diamond Platnumz ametangaza kuwalipia kaya 500 za watanzania wanaoishi kwenye mazingira magumu kodi ya miezi mitatu kila mmoja.

Diamond ametangaza kutoa Sadaka hii katika kipindi ambacho watanzania wengi mifuko yao imechanwa chanwa na gonjwa lenye roho mbaya la Corona.

Zaidi anatoa Sadaka hii kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hakika tunapaswa kusimama wote na kumpigia mizinga ya heshima Diamond. Hii inaitwa kurudisha fadhila kwa jamii yako.

Diamond wote tunafahamu historia yake ya maisha. Mara kadhaa amekua akisimulia namna alivyoangaika kuipata senti tano nyekundu. Masela wanaita 'kuhaso'. 

Huyu ni kijana wa kimaskini ambae alikulia maisha ya shida katika mitaa ya Tandale. Ni nani asiyejua aina ya maisha ya Tandale? Ni uswahili, uswazi haswa. Ugali Mende, Mchuzi Sisimizi.

Akapambana na kutoboa. Akaachia singo aliyoipa jina la Kamwambie. Hatujakaa sawa akabutua Mbagala. Tanzania ikasimama. Watanzania wakamfungulia milango kwa mikono miwili. Wakamwambia 'Karibu Baba'.

Hiyo ni miaka 10 na ushee iliyopita. Toka hapo juhudi zake zimelipa haswa. Ameshinda tuzo nyingi na kubwa za kila aina, amefanya kolabo za kimataifa kabambe sana. Ni kusema dogo ametusua sana.

Ni yeye ambaye ameifanya Bongo Fleva ikapata thamani mbele ya mapromota. Ni yeye ambaye ameisogeza Bongo Fleva duniani. Hili liko wazi sana. Diamond amekua njia ya muziki wetu ughaibuni.

Lakini unadhani ameyafanya haya peke yake? Thubutu!! Ni baraka na sala za watanzania ndizo zimemsogeza hapo alipo. 

Leo tunaposema yeye ni miongoni mwa mastaa wa gharama Afrika siyo kwa sababu yeye anajua kuimba sana, siyo kwa sababu yeye ni mtumbuizaji mzuri sana.

Baraka za watanzania kwake zimekua msaada mkubwa katika hilo, sapoti  ya wabongo imezidi kipimo kwake. Yeye mwenyewe ni shahidi wa namna watanzania wamekua wakimsapoti kwenye kila hali.

Kitendo cha kutangaza kuzilipia kodi za miezi mitatu kaya 500 za watanzania ni kuonesha uungwana wake kwa watu Milioni 50 ambao wamekua wakimsapoti kwenye muziki na biashara zake zingine.

Hii siyo tu atapata heshima duniani bali ataandikiwa thawabu hata mbinguni. Narudia tena tunapaswa kusimama kumpigia mizinga ya heshima.

Diamond ametoa funzo kwa mastaa wengine nchini siyo tu wa Muziki hata kwenye Soka na michezo mingine. Kuna haja kwao ya kurudisha shukrani kwa mashabiki na watu wote ambao wamekua wakiwasapoti.

Kuna kundi kubwa la watu wenye majina makubwa ambao hawajawahi kukumbuka hata jamii ya mtaani kwao achilia mbali watanzania kwa ujumla.

Hawajui bila watanzania hawa ambao wamewasapoti kwenye muziki, filamu na soka lao wangekua si chochote si lolote. 

Wapo matajiri wakubwa lakini wamekaa kimya na fedha zao. Hawajatoa barakoa wala sanitaiza.

Wapo wanasiasa ambao wameingia bungeni kwa kura za walalahoi wa kitanzania lakini hawajawahi kukumbuka kurudisha fadhila. Huyu Diamond anapaswa kupewa heshima yake.

Mrembo namba moja nchini kwa miaka 15, Wema Sepetu ameongeza hili kwenye Sadaka ya Diamond, " Mnyonge Mnyongeni haki yake mpeni" akimaanisha pamoja na mambo mengine aliyonayo Diamond ila kwenye hili anastahili pongezi.

KWANI NI MARA YA KWANZA KUFANYA HIVI?

Hii siyo mara ya kwanza Diamond kutoa msaada kwa wenye uhitaji. Hii siyo mara ya kwanza Diamond kuwashika mkono watu. Huyu bwana huwa hacheki peke yake. Anacheka na watanzania wenzake.

Oktoba 2018 kwenye kumbukizi yake ya kuzaliwa, alitangaza kugawa Bima za afya 300 kwa watoto, mitaji ya biashara kwa akina Mama 200 na Bodaboda 20 kwa masela wa Tandale.

Hivyo hili la kuwalipia kodi watu 500 siyo la kwanza kulifanya. Anaendelea pale ambapo alishaanza.

Siyo kwenye jamii tu. Kwenye muziki ambapo ndipo eneo lake la kutafutia riziki, Diamond amewashika mkono vijana wengi wa kitanzania.

Ni vijana ambao kushikwa kwao mkono na Diamond kumeinua maisha yao, kumeboresha familia zao. Kumbuka haikua lazima kwa Diamond kusaidia wasanii wengine. 

Lakini kwa sapoti ambazo amekua akipewa na watanzania akaona ni jukumu lake na yeye kuwainua wasanii wengine.

Yatazame mafanikio ya Harmonize, Rayvanny leo! Nyuma yao yupo Diamond. Mbosso na Zuchu ni mifano mingine ya siku za hivi karibuni. 

Tunawahitaji mastaa wengine wengi kama Diamond kwenye Nchi yetu. Mastaa ambao wako tayari kutoa hoteli zao kwa Serikali ili zitumike kama Karantini ama Hospitali kipindi hiki cha Corona.

Mastaa ambao watarudisha fadhila kwa watanzania ambao hupakua ngoma zao kwa malipo mitandaoni.

Tunahitaji wengine wanaoweza kusema watalipia gharama za matibabu ya wagonjwa wa moyo pale Taasisi ya Jakaya Kikwete. 

Hatuhitaji mastaa ambao wanawahitaji watanzania pale wanapokua wamekwama wao. Ni somo kubwa ambalo Diamond ametoa kwetu sote. Tujitafakari.

Lakini ngoja nikunong'oneze jambo kama kutoa kwa Jamii yenye uhitaji kuna malipo makubwa mbele za Mungu, basi sitashangaa tukimkuta Diamond anakunywa mvinyo peponi.
0683 015145

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad