HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 2, 2020

TUTAENDELEA KUWAWEZESHA WAJASIRIAMALI KIUCHUMI KUFIKIA UCHUMI WA VIWANDA-NBC

 Meneja wa benki ya Taifa ya Biashara NBC tawi la Mwanza Rogers Masolwa, akizungumza kwenye mkutano wa mashauriano ya uwekezaji uliofanyika jijini Mwanza.

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imesema itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano ya kuiwezesha nchi kuingia kwenye uchumi wa viwanda kwa kuendelea kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kiuchumi kupitia uwekezaji katika utoaji wa mikopo na mitaji ya kibiashara. 



Hayo yameelezwa jijini Mwanza na Meneja wa Benki ya NBC Tawi la Mwanza, Rodgers Masolwa, wakati wa kikao maalum cha mashauriano baina ya Serikali na wawekezaji na timu ya Mawaziri na manaibu Waziri kutoka wizara nane, walio kwenye ziara maalum kwenye mikoa ya Kanda ya ziwa. 



Alisema Benki ya NBC ni Benki Washirika mojawapo wa wafanyabiashara na Serikali ikiwa na historia ya kipekee nchini ikiwa ni benki ya kwanza iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 1 ya mwaka 1967, na kupitishwa na Bunge Februari 15, 1967. 
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella (aliyeketi) akifurahia jambo na Meneja wa benki ya Taifa ya Biashara NBC tawi la Mwanza Rogers Masolwa, kulia ni  Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu( Uwekezaji) Angelah Kairukiw wa mkutano wa mashauriano ya uwekezaji uliofanyika jijini Mwanza.

“Serikali ilichukua uamuzi wa kuunda Benki ya Taifa ya Biashara ili iweze kupeleka huduma za kibenki kwa Watanzania na hivyo kuwawezesha wananchi kiuchumi,” alisema na kuongeza kuwa NBC ndiyo Benki kongwe Tanzania ambayo inaendelea kuwatumikia watanzania kwa zaidi ya miongo mitano kwa uaminifu mkubwa. 

Alisema kwa sasa benki hiyo inamilikiwa na makampuni matatu, Kampuni ya ABSA Group Limited inayomiliki asilimia 55 ya hisa, Serikali ya Tanzania inayomiliki asilimia 30 ya hisa na International Finance Corporation inayomiliki asilimia 15 ya hisa. 

“Umiliki huu wa hisa umetokea baada ya Serikali yetu kupitisha uamuzi wa kuibinafisisha benki mnamo mwaka 2000. Benki inaunga mkono dhamira ya dhati ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kuifikisha kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo 2025.” 
Mbunge wa Nyamagana Stanislaus Mabula akiweka saini kwenye kitabu cha wageni cha NBC, Meneja wa benki ya Taifa ya Biashara NBC tawi la Mwanza Rogers Masolwa(aliyevaa suti), wakati wa mkutano wa mashauriano ya uwekezaji uliofanyika jijini Mwanza 

Aidha, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) inaunga dhamira hiyo kwa kuwawezesha wafanyabiashara katika sekta mbalimbali za kiuchumi kwa kutoa mitaji ya fedha ikiwa ni moja ya benki yenye mitaji mikubwa ya kifedha hapa nchini kuliko benki zingine. 

“Tumewawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kwa kuwapatia mitaji mikubwa kuagiza bidhaa muhimu kutoka nje ya nchi kama vile sukari na mafuta ya Petroli au kuuza nje ya nchi mazao ya kilimo,” alisema. 

Aliongeza kuwa kwa sasa benki hiyo inaendelea kutekeleza ajenda yake ya kidijiti, ikiwekeza maradufu kwenye mifumo ya teknohama ili kurahisisha utekelezaji wa miamala ya fedha kwa urahisi na kwa gharama nafuu kwa wateja wake. 

Aidha alisema, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Benki hiyo imeshusha riba ambayo imekuwa ikitoza kwenye mikopo, ambapo tangu mwaka 2016, riba kwa mikopo isiyokuwa na dhamana imeshuka kutoka wastani wa asilimia 22 hadi 17 kwa mikopo ya kibiashara ya muda mfupi ambapo riba hiyo imeshuka kutoka wastani wa asilimia 17 hadi 13.9. 

“Kwa mikopo ya muda wa kati na mrefu, riba imeshuka kutoka wastani wa asilimia 11.2 hadi asilimia 10, nia yetu ni kuona wateja wetu wanavutiwa na riba ndogo ili waweze kuendeleza biashara zao kwa ajili ya ustawi wa maisha yao,” alisema. 

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu( Uwekezaji) Angelah Kairuki, aliipongeza Benki hiyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kuiwezesha Serikali katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimaendeleo hapa nchini na kuzitaka benki nyingine za hapa nchini kuiga mfano wa Benki hiyo. 


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela alisema Mwanza ni mkoa wa kimkakati ulio na mazingira mazuri ya uwekezaji ambapo aliwataka wawekezaji wa ndani na nje kwenda kuwekeza katika mkoa huo wenye fursa nyingi za kiuchumi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad