MSAFARA WA KIJINSIA WAMPA SHAVU KIJANA MJASIRIAMALI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 4, 2020

MSAFARA WA KIJINSIA WAMPA SHAVU KIJANA MJASIRIAMALI

 
 Mwakilishi wa Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Bi. Imelda Kamugisha akizungumza na wananchi wa mkoa wa Shinyanga wakati wa mapokezi ya msafara wa kijinsia ulifika mkoani humo kwa lengo la kutoa elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
 Wasanii Shetta na G nako wakitumbuiza katika Eneo la Nguzo nane Mkoani Shinyanga wakati Msafara wa kijinsia unaolenga kutoa elimu ya mapambano dhidi ya vitendo vya kikatili uliposimama mkoani hapo.
 Msafara wa Kijinsia ukiongozwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Bi. Imelda Kamugisha wakikabidhi baiskeli kwa Martin Christopher Matiku ikiwa ni moja ya kuwawezesha Mabalozi wake wa kupambana na vitendo vya ukatili mikoani.
 . Baadhi ya wasaidizi wa kisheria wakitoa msaada wa kisheria kwa  wananchi wa mkoa wa Shinyanga waliojitokeza kuupokea msafara wa kijinsia unaolenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya vitendo hivyo.
  Wananchi wa mkoa wa Shinyanga wakifurahia burudani iliyokuwa ikitolewa na wasanii Shetta na G nako kwa kuweka mikono juu wakati wa mapokezi ya msafara wa kijinsia ulifika mkoani humo kwa lengo la kutoa elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

Na Mwandishi Wetu Tabora

Timu ya Msafara wa kijinsia unaolenga kutoa elimu juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia umefanikiwa kumpa  ubalozi na kumuwezesha kijana Martin Christopher baiskeli itakayomsadia kujikwamua kiuchumi na kuwa mfano kwa vijana na jamii katika mapambano dhidi ya vitendo vya kikatii mkoani Shinyanga.

Hayo yamefanyika  jana mkoani humo wakati wa mapokezi ya  Msafara wa Kijinsia kutokomeza ukatili unaolenga kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya kufanya vitendo vya ukatili wa kijinsia kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika Kitaifa Simiyu Machi 08, 2020.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu Bi. Imelda Kamugisha amesema kuwa Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa wanafunzi na watoto wadogo wa kike kupata mimba na kuolewa katika umri mdogo.

"Hapa Shinyanga kuna vitendo sana vya watoto wa kike na wanafunzi kupewa mimba wakiwa bado wadogo na kuolewa pia hili sio sawa naomba tulikemee kwa nguvu moja" alisema

Aidha amewataka vijana hasa waendesha baiskeli, bodaboda na bajaji kuwa mabalozi wazuri wa kutoa taarifa katika vyombo vya usalama mara waonapo vitendo hivyo vikitokea kwani watakuwa wameisadia jamii kuondokana na vitendo hivyo vinavyokatisha ndoto hasa za watoto wa kike nchini.

“Wanaofanya vitendo hivi ni watu wa karibu na familia zetu, wanawapa mimba watoto wetu tunanyamaza kisa ndugu. Wengine wazazi na walezi wanawaozesha watoto wakiwa wadogo hili sio sawa kabisa" alisema

Akitoa shukrani zake mara baada ya kupewa ubalozi na baiskeli kwa ajili ya biashara Martin Christopher Matiku ameishauri jamii ya mkoa wa Shinyanga kuwa pia mabalozi wazuri wa kuhakikisha wanakemea vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao ili kuweza kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia vinatokomea.

“Naushukuru huu Msafara wa Twende Pamoja naahidi nitakuwa Balozi mzuri na nitasaidia kutoa elimu juu ya madhara ya vitendo vya ukatili naamini itasaidia kuokoa watoto wa kike na kiume pamoja na wanawake katika madhara haya” alisema

Naye Mtoa Huduma za Kisheria mkoa wa  Shinyanga Anna Kadaso Mtao amesema kuwa kesi nyingi zinazopokelewa katika madawati hayo ni za vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa vipigo unyanyasaji wa wanawake katika mirathi na kesi za wanaume wakinyanyaswa pia zipo ingawa bado sio nyingi zinazotolewa taarifa.

Msafara wa kijinsia kutokomeza ukatili wa kijinsia upo katika mzunguko ulioanzia mkoa wa Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Tabora na umefika mkoani Shinyanga. Msafara huu utapokelewa mkoani Simiyu kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad