BILIONI 10.5 KUMALIZA TATIZO LA MAJI KIGAMBONI, DAWASA WATIA SAINI NA KAMPUNI YA ADVENT - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 17 December 2019

BILIONI 10.5 KUMALIZA TATIZO LA MAJI KIGAMBONI, DAWASA WATIA SAINI NA KAMPUNI YA ADVENT

 Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja (kulia) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Advent Construction Tanzania Ajith Prasad (kushoto) wakibadilishana mkataba wa makubaliano wa uendelezwaji wa ujenzi wa mradi wa usambazaji maji Kimbiji utakaohusisha ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa Lita milioni 15 litakalojengwa eneo la Kisarawe II na kituo cha kusukumia maji (pumping station). Utiaji huo wa saini umeshuhudiwa na Mbunge wa Kigamboni na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Sarah Msafiri na viongozi wengine leo katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kigamboni.

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

Wakazi wa Kigamboni wako mbioni kuondokana na kero ya upatikanaji wa maji safi kwa muda mrefu baada ya mradi wa maji wa visima vya Kimbiji ulioibuliwa mwaka 2005 kuanza kuendelezwa kwa kujenga miundo mbinu ya usambazaji maji.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam DAWASA wameitia saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa usambazaji maji Kimbiji na kampuni ya Advent ya Tanzania wenye thamani ya Bilioni 10.5

Mkataba huo umetiwa saini ukishuhudiwa na Mbunge ww Kigamboni na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Sarah Msafiri na viongozi wengine.

Akizungumza kabla ya utiaji saini, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema Kigamboni ni moja ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam ambapo mtandao wa maji ni mdogo katika eneo la Navy yakitokea mtambo wa Ruvu Chini kupitia bomba la inchi 16.

Luhemeja amesema, mradi wa visima vya Kimbiji una visima vyenye urefu wa mita 600 na uwezo mkubwa wa uzalishaji maji na mkakati ni kuviendeleza ikiwa na kuanza ujenzi wa miundo mbinu itakayochukua maji kutoka kwenye visima hivyo.

Amesema, wameingia makubaliano na kampuni ya Advent ya kujenga tanki la kukusanyia maji kutoka visima mbalimbali (sump well) lenye ujazo wa Lita 540,000, ujenzi wa Kituo cha Kusukumia maji (pumping station), ujenzi wa mabomba ya kusafirishia maji yenye urefu wa jumla ya km 6 hadi kwenye tanki.

Pia, litajengwa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa Lita Milioni 15 litakalojengwa katika eneo la Kisarawe II.

Kwa upande wa Naibu Waziri, Ndugulile amewaongeza sana Dawasa kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kupeleka maji katika Mkoa mpya wa Kihuduma wa Kigamboni kwani ni miaka mingi kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo mengi ya Wilaya hiyo.

Ndugulile, amesema mradi unachukua miezi 12 mpaka kukamilika, na utakapokamilika utaondoa kero ya maji ya wakazi wa Kigamboni, na amefurahishwa kwa Dawasa kuipa hadhi wilaya hiyo kuwa mkoa kamili wa kihuduma na amewaahidi kushirikiana nao katika kuleta maendeleo.

"Nikiangalia takwimu ya miaka ya mitatu ya nyuma, huduma ya maji kwa sasa imekuwa san nawapongeza mnafanya jitihada kubwa za kuhakikisha maji yanapatikana tena mnajenga miradi kwa fedha za ndani na hii ndiyo kasi anayoenda nayo Serikali ya  awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli kuelekea uchumi wa kati wa Viwanda," amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi Dawasa Laston Msongole amesema wanaendelea na jitihada za kuhakikisha Mkoa wa Dar es Salaam unamaliza tatizo la maji kwa kuwafikia wananchi wote hususani maeneo ya nje ya mji ambapo mtandao wa Dawasa haujafika.

Kwa sasa wananchi wa Kigamboni wanapata maji kutoka kwenye visima virefu vipatavyo 29, ambapo kwa sheria mpya vinasimamiwa na Dawasa vyenye uwezo wa kujaza Lita 225,556 kwa saa vikiwa na vizimba 151 na wateja 2,324 .

Visima hivyo ni pamoja na Minondo, Mwasonga, Kisarawe II, Vijibweni, Geza ulol, Ungindoni, Maweni, Puna na baadhj mengine ya maeneo.

Mradi wa maji wa Kimbiji unakuwa moja ya chanzo kikubwa cha maji chenye uhakika kwa jiji na maendeleo ya Mkoa wa Dar es Salaam.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja (kulia) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Advent Construction Ajith Prasad (kushoto) wakitia saini mkataba wa makubaliano wa uendelezwaji wa ujenzi wa mradi wa usambazaji maji Kimbiji utakaohusisha ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa Lita milioni 15 litakalojengwa eneo la Kisarawe II na kituo cha kusukumia maji (pumping station). Utiaji huo wa saini umeshuhudiwa na Mbunge wa Kigamboni na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Sarah Msafiri na viongozi wengine leo katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kigamboni.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa makubaliano wa uendelezwaji wa ujenzi wa mradi wa usambazaji maji Kimbiji utakaohusisha ujenzi wa tanki la maji lenye ujazo wa Lita milioni 15 litakalojengwa eneo la Kisarawe II na kituo cha kusukumia maji (pumping station) leo katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kigamboni.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi Dawasa Laston Msongole akizungumzia utiaji saini wa mkataba wa uendelezwaji wa Visima vya Kimbiji kwa kujenga miundo mbinu ya usambazaji maji, mkataba huo umetiwa saini leo katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kigamboni.
 Mbunge wa Kigamboni na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile, akiwapongeza DAWASA kwa kazi kubwa ya kupelekamaji  katika Mkoa mpya wa Kihuduma wa Kigamboni kwani ni miaka mingi kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo mengi ya Wilaya hiyo.
 
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Sara Msafiri akiwashukuru DAWASA kwa kufanikisha mradi mkubwa wa maji wenye thamani ga Bilion 10.5 kuanza kutekelezwa ndani ya Wilaya yake.
Watendaji na viongozi mbalimbali wakifuatilia hafla ya utiaji saini.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad