TMDA YATOA GAWIO LA BILIONI 29 KWA SERIKALI YA AWAMU YA TANO KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MINNE - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 27 November 2019

TMDA YATOA GAWIO LA BILIONI 29 KWA SERIKALI YA AWAMU YA TANO KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MINNE

TMDA inaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa gawio kwa Serikali kwa kila mwaka ambapo kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali iliyopo madarakani, Mamlaka hiyo imefikisha jumla ya bilioni 29.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati wa kutoa gawio la TMDA kwa mwaka 2018/19 baada ya kumkabidhi Rais Magufuli mfano wa hundi yenye thamani ya bilioni 12.475 katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino tarehe 24 Novemba, 2019; Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa TMDA, Mhe. Balozi Dkt. Ben Moses alisema, “Kazi ya Bodi yangu ni kuhakikisha tunaisimamia ipasavyo Mamlaka hii ili iweze kutimiza majukumu yake ya msingi kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa maendeleo ya nchi yetu, na kwa kweli Menejimenti na watumishi wa Taasisi hii wamekuwa wakifanya kazi kwa kujituma na kuweza kufikia mafanikio haya na tutahakikisha yanakuwa endelevu.”
Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Danstan Hipolite alisema, “TMDA itaendelea kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili kulinda afya ya jamii, lakini pia itaendelea kusimamia vema rasilimali za Serikali ilizo nazo ili kuwa na tija na kuchangia katika pato la Taifa kama ambavyo Serikali imekuwa ikielekeza.”
TMDA ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambayo kabla ya tarehe 01 Julai, 2019 ilijulikana kama Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambapo jina hilo lilibadilika baada ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2019 kufanya marekebisho katika Sheria Mama ya taasisi hiyo kwa kuhamisha majukumu ya udhibiti wa bidhaa za vyakula na vipodozi kwenda katika Shirika la Viwango Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad