HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, 13 October 2019

WAKANDARASI MIRADI YA MAJI MTWARA WATAKIWA KUONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI

Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maji kwenye Wilaya za Newala, Tandahimba na Masasi, Mkoani Mtwara wametakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wake ili ikamilike mapema hasa ikizingatiwa mahitaji muhimu ya kukamilisha miradi hiyo yamekamilika.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga ametoa agizo hilo Oktoba 12, 2019 Mkoani Mtwara kwa nyakati tofauti alipofanya ziara kwenye miradi ya maji inayotekelezwa kwenye wilaya hizo.

Naibu Katibu Mkuu Sanga alitembelea mradi wa Mkwiti uliyopo Wilaya ya Tandahimba, Chanzo cha Maji cha Mitema, Mradi wa Makonde na aMradi wa Kilidu yote ya Wilaya ya Newala na mradi wa Chipingo Wilayani Masasi.

Mara baada ya kuzungukia miradi, Mhandisi Sanga alisema hajaridhika na kasi ya utekelezaji wake licha ya kwamba vifaa vinavyohitajika kukamilisha miradi hiyo ikiwemo mabomba na mitambo ya kusukuma maji vikiwa vimekamilika.

Alisema haoni sababu kwanini miradi inatekelezwa kwa kusuasua licha ya kuwa vifaa muhimu vipo eneo la mradi. "Nimezungukia maeneo ya miradi nimeona vifaa muhimu vinavyohitajika kukamilisha miradi vipo, hakuna sababu ya kuendelea kupoteza muda," alisisitiza Mhandisi Sanga.

Alisema kinachotakiwa ni wananchi kupata maji mapema iwezekanavyo na kwamba suala la kupoteza muda halitokubalika hasa ikizingatiwa maeneo inapotekelezwa miradi yanasumbuliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji.

Aliagiza wasimamizi wa miradi ambayo ipo katika hatua ya ulazaji bomba kuharakisha kumaliza shughuli hiyo hasa ikizingatiwa msimu wa mvua umefika na kwamba mitaro hiyo ikiendelea kubaki wazi itajifukia na italazimika kuchimbwa upya.

"Nimeona mitaro imechimbwa na imekamilika na mabomba yapo hakikisheni kuanzia sasa mabomba yanalazwa ili kuepusha gharama ya kufanya kazi mara mbili ya kuchimba mitaro ya maji," aliagiza Naibu Katibu Mkuu Sanga.

Mhandisi Sanga aliagiza wasimamizi wa miradi kuhakikisha kwenye kutekeleza miradi wanaanza na maeneo yatakayoleta matokeo ya haraka ili wananchi waanze kupata huduma na baadaye waendelee na maeneo mengine wakati ambao tayari wananchi wanakuwa na huduma.

“Mnatakiwa kuwa wabunifu wakati wa ujenzi wa miradi, mnapaswa kuanza na maeneo yatakayoleta matokeo ya haraka ili kwanza wananchi wapate huduma na huku mkiendelea kutekeleza maeneo mengine,” alisisitiza Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga yupo Mkoani Mtwara kwa ziara ya siku tatu ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji inayotekelezwa Mkoani humo ili kujionea hatua ya utekelezaji wake sambamba na kufahamu changamoto zilizopo ili kuzitafutia ufumbuzi.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kulia) alipotembelea mradi wa maji wa Mkwiti, Wilayani Tandahimba. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Mtwara (MTUWASA), Mandisi Rejea Ng’ondya.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akikagua mitambo ya kusukuma maji kwenye kituo cha Mtongwele ambacho kitatumiwa kupelekea maji kwenye mradi wa Mkwiti kutokea chanzo cha Mitema (Mitema Well Field). Kulia ni Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (katikati) akielekeza jambo wakati wa ziara yake kwenye mradi wa maji wa Kilidu, Halmashauri ya Mji wa Newala. Kushoto ni Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba.
  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akikagua mradi wa maji wa Chipingo-Mkaliwata wa Wilaya ya Masasi, Mkoani Mtwara unaotumia maji kutoka Mto Ruvuma.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga akielekeza jambo wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa maji wa Chipingo-Mkaliwata unaotekelezwa Wilayani Masasi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akikagua mradi wa maji wa Makonde Wilayani Newala ambapo pia ni eneo kilipo chanzo cha maji cha Mitema (Mitema Well Field) ambacho kitatumika kwa ajili ya miradi ya Mkwiti, Makonde na Kilidu.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad