HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 9 October 2019

PSPTB YAWAWEKA KIKAANGONI WAKUU WA VITENGO VYA MANUNUZI TAASISI 20 ZA SERIKALI

Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB)  imewataka wakuu wa vitengo vya ununuzi na ugavi katika taasisi 20 nchini zikiwepo BoT, TBS, TCAA na NIMR kukaa pembeni kupisha uchunguzi.
Maamuzi hayo yametolewa leo PSPTB baada ya kupokea  ripoti ya PPRA na kuonesha taasisi hizo kukosa weledi katika manunuzi ya umma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Ununuzi na Ugavi wa Umma (PSPTB) Godfred Mbanyi amesema, taasisi kumuajiri mtu asiyesajikiwa na bodi hiyo ni kosa  la jinai na adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka miwili jela au faini ya milioni mbili au vyote kwa pamoja.

Mbanyi amesema toka mwaka 2016 hadi 2019 walifanya ukaguzi kwenye mikoa tisa na katika taasisi 146 na kubaini jumla ya watumishi 268 hawajasajiliwa kwenye bodi ya ununuzi na ugavi na mpaka kufikia Septemba 2019 wataalamu 146 wamesajiliwa na 89 wakiwa bado huku 33 hawapo kazini kwa sababu mbalimbali.

Amesema, bodi kwa kutumia mamlaka iliyonayo chini ya kifungu cha 33 cha kanuni za maadili na mienendo ya wataalamu inafanya uchunguzi wa kina kwa wakuu wa vitengo vya ununuzi toka taasisi hizo na kuwapeleka mbele ya kamati ya maadili ya bodi.

Mbanyi amesema, kwa sasa inawaagiza wakuu wa taasisi hizo kuwatoa kuongoza vitengo vya idara za ununuzi mpaka shauri lao litakapokamilika na watajulishwa.

"PSPTB inawaagiza waajiri wote kwenye sekta ya umma na binafsi kuhakikisha watu wote wanaofanya kazi za ununuzi na ugavi wamesajiliwa na wana sifa stahiki kwa mujibu wa sheria,"amesema Mbanyi. 

Taasisi hizo ni pamoja na wizara ya maji na umwagiliaji, Wakala wa umeme Vijijini (REA), Mamlaka ya Anga, Veta Makao Makuu, Mamlaka ya Bandari, Manispaa ya Ubungo, Manispaa ya Kahama, TANAPA, Wakala wa mbegu za Kilimo (ASA), Mamlaka ya maji na usafi wa Mazingira Singida, Wilaya ya Kaliua, Wilaya ya Nkasi, Wilaya ya Masasi, Shirika la Reli Nchini (TRC), Manispaa ya Kigamboni.
Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya wataalumu wa Manunuzi na Ugavi (PSPTB), Godfred Mbanyi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu bodi hiyo ilivyofanya ukaguzi kwa taasisi 146 zilizopo katika mikoa tisa  na kubaini jumla ya watumishi 268 wanafanya kazi za ununuzi na ugavi bila kusajiliwa na Bodi hiyo wakati wa mkutano  uliofanyika katika ofisi za bodi hiyo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wafanyazi pamoja na waandishi wa habari wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya wataalumu wa Manunuzi na Ugavi (PSPTB), Godfred Mbanyi alipokuwa  anazungumza na waandishi wa habari  katika ofisi zaBodi hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Mkutano ukiendelea

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad