DAWASA, MAAFISA AFYA WAJA NA LENGO MOJA LA KUTOKOMEZA KIPINDUPINDU - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 22 October 2019

DAWASA, MAAFISA AFYA WAJA NA LENGO MOJA LA KUTOKOMEZA KIPINDUPINDU

Na Zainab  Nyamka, Globu ya Jamii

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam DAWASA wameweka mpango kazi wa kupambana na kutokomeza  magonjwa ya mlipuko (kipindupindu)  kwa kushirikiana na Maafisa Afya wa kata Jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kimefanyika leo kwa Maafisa Afya kutoka kata mbalimbali za Manispaa zote za Jiji na DAWASA kujadiliana kwa pamoja namna ya kupambana na magonjwa hayo.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii DAWASA Neli Msuya amesema katika mkakati wa muda mfupi watasaidia kutoa vidonge (dawa) kwa ajili ya kusafisha maji ya visima na kuwapatia wananchi.

Amesema, kwa kushirikiana na maafisa afya watahakikisha wanafanya vikao kila mwisho wa mwezi ili kuhakikisha magonjwa ya mlipuko ikiwemo kupindupindu kisiwepo ndani ya Mkoa wa Dar es salaam.

Neli amesema, kuna changamoto ya uharibifu wa mazingira kwa wale wanaotiririsha majitaka ila baada ya kikao hiki anaamini Maafisa Afya watawavumbua wale wote wanaofanya vitendo hivyo.

"Tunatambua kuna maeneo yanatabia ya kutiririsha maji taka wakati wa mvua, wanayaachia maji na kusambaa na ndio yanakuwa chanzo kikubwa cha magonjwa ya mlipuko kwahiyo mpango mkakati tuliofikia kwa pamoja ni Maafisa Afya kusimamia kwa weledi na kuhakikisha tunatokomeza tabia hiyo,"amesema Neli.

Aidha, Neli amesema kuna watoa huduma wa maji wanaouza maji kutoka kwenye visima vyao mara nyingi tumekuwa tunawashauri waweke dawa na hata hivi karibuni tumewapatia dawa kwa ajili hiyo.

Pia, baada ya sheria mpya ya maji kuanza kufanya kazi, wamiliki wote wa Visima wametakiwa kuja kujisajili na kupatiwa leseni baada ya maji yao kupimwa na kuthibitishwa kama yanafaa kwa ajili ya matumizi kwa binadamu.

Ameeleza, kuna changamoto ya visima vifupi vilivyopo kwenye maeneo yenu ambavyo kiuhalisia hamuwezi kuviweka dawa ila ninaamini mtavifanyia kazi kama tulivyokubaliana.

Akielezea mchakato wa majitaka, Charles Makoye amesema kuwa wamekuwa na mkakati wa kuendelea kujenga mabwawa ya majitaka kwenye maeneo tofauti pamoja na ujenzi wa vyoo vya jamii ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Makoye amesema, kuna baadhi ya maeneo yaliyokuwa yanaongoza kwa magonjwa ya mlipuko yamepungua kasi ikiwemo Vingunguti baada ya kujenga mfumo wa vyoo unaopeleka maji moja kwa moja kwenye mabwawa na umewasaidia wananchi kupunguza kasi ya magonjwa hayo.

Afisa Afya Mkoa Dar es salaam, Enezael Emmanuel amewataka maafisa afya kuanza kutekeleza yale waliyokubaliana kwenye kikao cha leo na kuanza kuyafanyia kazi kabla madhara hayajaanza kujitokeza.

Kwa upande wa Maafisa afya wameahidi kushirikiana na DAWASA katika kupambana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kutekeleza yale waliyokubaliana pamoja na vya kila mwezi.

Maafisa Afya Wameiomba DAWASA kupeleka mifumo ya majitaka kwenye maeneo yao ambayo yana changamoto kubwa na wananchi wamekuwa wakiathirika kwa kiasi kikubwa kipindi cha mvua na baadhi yao kutiririsha maji taka.
Afisa Afya Mkoa Dar es salaam, Enezael Emmanuel amewataka maafisa afya kuyafanyia kazi maazimio yote yaliyoafikiwa kwenye kikao chao pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam DAWASA ya kuhakikisha wanatokomeza magonjwa ya mlipuko.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam DAWASA Neli Msuya akizungumza na maafisa afya wakati wa kikao cha pamoja na kufikia mpango mkakati wa muda mfupi na muda mrefu la kutokomeza magonjwa ya mlipuko.
Meneja wa Majitaka na Usafi ww Mazingira DAWASA Mhandisi Charles Makoye akielezea mkakati wa mamlaka katika kujenga miundo mbinu ya majitaka na vyoo vya jumuiya katika Mkoa wa Dar es Salaam na namna watakavyopambana na magonjwa ya mlipuko.
Maafisa afya wakiwa wanafuatilia kikao

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad