HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 13, 2019

TULIA TRADITIONAL DANCES FESTIVAL KURINDIMA SEPTEMBA 26 HADI 28 TUKUYU, MBEYA

*Kila mshiriki kunufaika na mashindano hayo ikiwemo kupata nafasi ya masomo katika chuo cha sanaa Bagamoyo (TASUBA)

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

MASHINDANO ya ngoma za asili yanayojumuisha vikundi mbalimbali kutoka Mikoa ya Tanzania bara na visiwani yajulikanayo Kama "Tulia Traditional Dances Festival" kwa mwaka huu yanatarajiwa kutimua vumbi kuanzia Septemba 26 hadi 28 mwaka huu huko Tukuyu jijini Mbeya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam balozi wa mashindano hayo na mwigizaji wa filamu nchini Yvonne Cherry maarufu kama Monalisa amesema kuwa kwa mwaka huu vikundi vilivyoomba kushiriki vimekuwa vingi zaidi ukilinganisha na mwaka jana ambapo vikundi 108 kutoka Tanzania bara na visiwani vitashindana.

"Kuna vikundi vinatoka Mikoa ya Dodoma,  Kigoma, Kilimanjaro, Tanga, Kagera, Mwanza, Mtwara, Njombe, Lindi, Dar es Salaam na Songwe na watazamaji zaidi ya 1500 wanakadiriwa kushuhudia ngoma hizi na kubwa zaidi kwa mwaka huu kipengele cha chakula cha asili kimeongezwa ambapo kila kikundi kishiriki kitakuja na akina Mama wawili ambao watapika vyakula vya asili ili wahudhuriaji  wapate kufahamu vyakula vyetu vya asili na kuuenzi utamaduni wetu" ameeleza Monalisa.

Kuhusiana na zawadi zitakazotolewa kwa washindi hao Dotto Bernad Bwakeya maarufu kama Ditto amesema kuwa, watakaoshiriki katika mashindano hayo wote ni washindi na watapewa zawadi ili kupongezwa kwa juhudi zao;

"Mshindi wa kwanza atakayeibuka kidedea atazawadiwa pikipiki 22 yaani pikipiki moja kwa kila mwanakikundi, mshindi wa pili atapata fedha taslimu shilingi milioni moja kwa kila mwanakikundi, mshindi wa tatu atapata shilingi laki saba kwa kila mwanakikundi na kila siku kikundi kilichoshiriki kitapata fedha taslimu shilingi laki nne na hiyo ni pamoja na baadhi ya washindi kupata nafasi ya masomo katika chuo cha sanaa Bagamoyo" ameeleza Ditto.

Amesema kuwa kwa mwaka huu nafasi 40 zimetengwa ambapo baadhi ya washindi watadhaminiwa kusoma cha sanaa (TASUBA) kilichopo Bagamoyo na kusoma kozi fupi na wenye vigezo watadhaminiwa kusoma ngazi za cheti na Astashahada ili wakimaliza wajitengenezee nafasi na fursa kwao na kwa vijana wengine.

Mwasiti Almas nyota wa muziki wa Bongo Fleva amesema kuwa; kwa mwaka huu taasisi ya Tulia Trust imeshirikiana na ubalozi wa China ili kufanikisha tamasha hilo pekee linaloendeshwa nchini ambapo ubalozi wa China umetoa pikipiki 22 zitakazotolewa kwa washindi wa kwanza kwenye tamasha hilo.

Taasisi ya Tulia Trust iliyo chini ya Naibu spika wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania  Dkt. Tulia Ackson ilianzishwa mwaka 2015 ikiwa na malengo ya kuwasaidia watu watu walio hatarini hasa akina mama, walemavu, wazee pamoja na kupambana na magonjwa na umaskini.
 Mabalozi wa mashindano ya ngoma za asili yajulikanayo kama "Tulia Traditional Dances Festival" wakiwa wameshika fulana maalumu iliyobeba dhima ya mashindano hayo, kulia ni Yvonne Cherry (Monalisa,) Mwasiti Almas (kushoto) na katikati  Dotto Bernad Bwakeya (Lameck Ditto.) Leo jijini Dar es Salaam.
 Msanii wa Muziki wa Bongo Fleva Dotto Bernad Bwakeya maarufu kama Ditto (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mashindano hayo ambapo amesema kuwa washiriki wote ni washindi na zawadi watakazopewa ni pongezi kutokana na juhudi zao, leo jijini Dar es Salaam.
 Msanii wa muziki wa Kizazi kipya Mwasiti Almas akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mashindano hayo na kueleza kuwa taasisi hiyo na ubalozi wa China umeshirikiana kwa ukaribu zaidi katika kufanikisha malengo ya mashindano hayo, leo jijiji Dar es Salaam.
Yvonne Cherry maarufu kama Monalisa (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mashindano hayo ya ngoma za asili yanayotarajiwa kufanyika mapema mwezi huu ambapo amesema kuwa zaidi ya watazamaji 1500 wanakadiriwa kushuhudia mashindano hayo, leo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad