Mwenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} Kisiwa cha Unguja kwa niaba ya Kamati Mbili za Visiwa vyote vya Zanzibar Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud wa kwanza Kulia akizungumza na Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 yanayounda Taifa la Nigeria waliowasili Nchini Tanzania kwa Ziara maalum. Kushoto kwa Mh. Ayoub Mohamed ni Mkurugenzi wa Uratibu wa Shughuli za SMT na SMZ anayesimamia Mfuko wa Tasaf upande wa Zanzibar Nd. Khalid Bakar Amran.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) Unguja ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed akisisitiza jambo wakati akizungumza na Waratibu hao.
Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Nigeria na Waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) wakijadiliana mambo mbali mbali yanayohusu mafanikio makubwa yaliyopatikana katika maendeleo ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania(TASAF).
Mwenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) Unguja ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed kati kati waliokaa vitini akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Nigeria waliowasili Nchini kwa ziara Maalum. Picha na – OMPR – ZNZ.
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini Tanzania (TASAF) upande wa Zanzibar
unatarajia kuzigusa Shehia zote 388 katika muelekeo wake wa
utekelezaji wa Mpango wa kuhudumia Kaya Maskini kwa Mwaka 2019/2020
Tasaf Awamu ya Nne.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) Kisiwa cha Unguja kwa niaba ya Kamati Mbili za Visiwa vyote vya
Zanzibar Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alisema hayo wakati akizungumza na
Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 yanayounda Taifa la Nigeria
waliowasili Nchini Tanzania kwa Ziara maalum.
Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi
aliwaeleza Waratibu hao waliofika Zanzibar kujifunza Mpango Maalum wa
kuhudumia Kaya Maskini kwamba Shehia zinazohudumiwa kwa sasa
zimeshafikia 233 kati ya 388.
Alisema katika muelekeo huo hakutakuwa na Shehia hata Moja isiyoguswa
katika masuala ya Kaya Maskini kazi itakayokwenda sambamba na mapitio
ya Shehia ambazo kwa sasa zinaendelea kuhudumiwa kutokana na kuwa na
sifa za kuingia katika Kaya Maskini lakini zilishindakana kutokana na
ufinyu wa Bajeti katika Awamu iliyopita.
Mheshimiwa Ayoub alitanabahisha kwamba Mapitio hayo yatachambua katika
kuzifanyia tathmini Shehia ambayo zilikuwa na Kaya Maskini lakini kwa
sasa tayari zimeshakuwa Kiuchumi na kukosa sifa ya kuwa Kaya Maskini.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) Kisiwa cha Unguja aliwafahamisha Waratibu Wakuu hao wa Majimbo
36 ya Nigeria kwamba yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika
uimarishaji wa Ustawi wa Jamii kupitia Mfuko wa Tasaf.
Alisema uundwaji wa Vikundi vya Kijamii katika Shehia mbali mbali za
Visiwa vya Unguja na Pemba umesaidia kuibua Miradi tofauti
iliyowezesha Wananchi Kiuchumi na hatimae kupiga hatua kubwa ya
mapambano dhidi ya kuondokana na ukali wa Maisha.
Hata hivyo Mh. Ayoub alisema Sekta ya Kilimo imeleta faida kubwa ndani
ya Mfuko wa Tasaf ingawa bado zipo baadhi ya changamoto zinazowakazwa
Wananchi katika maeneo yao hasa kwenye Sekta ya Afya na Elimu ambazo
ndio kichocheo cha kuimarika kwa Ustawi na Maisha ya Jamii kwa ujumla.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania
{TASAF} Unguja ameipongeza Timu ya Waratibu hao Wakuu wa Majimo 36 ya
Nigeria kwa uamuzi wao wa kufika Zanzibar kujifunza muenendo mzima wa
harakati ya maendeleo yanayotokana na Mfuko wa Tasaf.
Akitoa Shukrani zake Kiongozi wa Timu hiyo ya Waratibu Wakuu wa
Majimbo 36 yanayounda Taifa la Nigeria Naibu Mkurugenzi wa Taasisi
inayosimamia masuala ya Ustawi wa Jamii Bwana Ortutu alisema ziara yao
Nchini Tanzania imekuja kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana
katika mpango wa kuhudumia Kaya Maskini.
Bw. Ortutu alisema Tanzania ni miongoni mwa Nchi chache Duniani
zilizofanya vizuri na kuchukuwa anafasi ya juu katika kuendeleza
Mpango huo, huku Visiwa vya Zanzibar vikifanya vizuri zaidi
ikilinganishwa na upande wa Tanzania Bara.
Alisema ujio wao wa kuja kujifunza Nchini Tanzania utawapa nafasi ya
kuibua njia zitakazowasaidia kupata mbinu za muelekeo wa kupambana na
changamoto zinazowakabili katika kutoa huduma kutokana na idadi kubwa
ya Wakaazi wake zaidi ya Milioni 200 wanaoishi ndani ya Majimbo 36 ya
Nchi hiyo iliyo Magharibi ya Bara la Afrika.
Mapema akitoa Taarifa Mwakilishi wa Mfuko wa Tasaf wa Kanda Bibi Saida
Saleh Adam alisema zaidi ya Shilingi Bilioni 27 zimeshatolewa katika
Mpango Maalum wa kuhudumia Kaya Maskini Unguja na Pemba.
Bibi Saida alisema fedha hizo zililengwa katika uimarishaji wa huduma
za Afya na na Sekta ya Elimu katika kuwapatia mahitaji ya Vifaa
Wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu ndani ya mpango wa
stawisha Maisha Vijiji 20.
Ujumbe huo wa Timu ya Waratibu Wakuu wa Majimbo 36 ya Taifa la Nigeria
walipata fursa ya kukagua Kituo cha Afya Kiyanga kilichojengwa kupitia
mradi wa Kijamii ndani ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tasaf pamoja na
kuona maeneo ya uzalishaji wa mazao ya viungo.
No comments:
Post a Comment