HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 27, 2019

MWENGE WAZINDUA KIWANDA CHA MAJI ASILI NA JIWE LA MSINGI BARABARA YA MBUYULA MBINGA MJI

MWENGE wa uhuru kitaifa umemaliza mbio zake kwenye Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma kwa kuzindua, kukagua, kuweka jiwe la msingi, kutembelea miradi tisa ya thamani ya shilingi 924,150,266.14 ikiwemo mradi wa maji Asili (Mdaka Five) na barabara ya lami ya Mbuyula. 

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa wa mwaka huu, Mzee Mkongea Ally akizungumza jana wakati akizindua kiwanda cha maji Asili cha Mdaka Five aliwataka wamiliki wake kutoa ajira kwa wakazi wa eneo hilo. 

"Kupitia kiwanda hiki cha maji Asili hongereni sana watu wa Mbinga mji mmepiga hatua kwenye viwanda kwani Rais John Magufuli ana amini katika Tanzania ya viwanda ili kuongeza ajira na kulipa kodi," alisema Ally. 

Akizungumza wakati akiweka jiwe la msingi la barabara ya lami ya Mbuyula, Mzee aliwapongeza Tarura kwa ubora uliotumika ikiwemo kuzingatia urefu na upana. 

"Tunatoa ushauri kuwa vipimo vyote vilivyoelekezwa vifanyiwe kazi ipasavyo ili barabara hii iweze kuwanufaisha wananchi wa eneo hili pindi ikikamilika kabisa," alisema Ally. 

Meneja wa Tarura Halmashauri ya Mji wa Mbinga, mhandisi Ismail Mafita, akisoma taarifa ya barabara ya hiyo ya lami awamu ya kwanza alisema inajengwa na mkandarasi Ovans Construction Ltd kwa gharama ya shilingi 152,570,000.00.

Mhandisi Matifa alisema barabara hiyo imetengewa shilingi 16,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa mfereji wa upande wa pili, kuweka kivuko cha waenda kwa miguu na alama za barabarani ila kilometa zilizobaki zitamalizwa baada ya fedha nyingine kuletwa. 

Alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutapunguza adha ya usafiri kwa wakazi wa kata za Mbinga Mjini, Mbambi, Matarawe na wanaoenda kupata huduma za afya katika hospitali ya Mji wa Mbinga (Mbuyula). 

Mkurugenzi wa Mdaka Five Co. Ltd, Joseph Mdaka alisema mradi wa kiwanda cha maji Asili umegharimu shilingi 265,500,000. ikiwemo jengo na mashine na hadi kukamilika kwake itagharimu shilingi 485,500,000 ikiwemo ujenzi wa maghala na uzio kiwandani.

Mdaka alisema lengo la mradi huo ni uzalishaji wa maji ya kunywa ambao ni safi na salama kutoka chanzo cha maji mlima Mhekela kilichotunzwa vizuri kwa kupanda miti eneo lote linalozunguka chanzo. 

"Uwepo wa kiwanda hiki utazalisha ajira za kudumu 25 na utahudumia wananchi wa Mbinga na Ruvuma kwa ujumla kwa kuhakikisha nchi inakuwa na uchumi wa kati na mkakati wa kila mkoa kuwa na viwanda visivyopungua 100," alisema. 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, Grace Quintine alisema mwenge wa uhuru umeridhishwa na miradi yote tisa ya thamani ya shilingi 924,150,266.14 na hakuna hata mmoja uliokataliwa. 

Quintine alisema kauli mbiu ya mbio za mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka huu ni "Maji ni haki ya kila Mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa". 
 Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa wa mwaka huu, Mzee Mkongea Ally akipeana mikono na Mkurugenzi wa Mdaka Five CO. Ltd, Joseph Mdaka baada ya kuzindua kiwanda chake cha maji Asili kilichopo mtaa wa Masumuni Halmashauri ya mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma. 
 Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa wa mwaka huu, Mzee Mkongea Ally akizindua mradi wa maji wa Maganagana, kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, Grace Quintine. 
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa wa mwaka huu, Mzee Mkongea Ally na Meneja wa Tarura, Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, Ismail Mafita, wakiangalia upimaji wa upana wa barabara ya lami ya Mbuyula ambapo aliweka jiwe la msingi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad