Na Catherine Sungura –Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee wa Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile amemuagiza Msajili wa Baraza la Madaktari la
Tanganyika kushirikiana na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania
kufuatilia mtoto aliyekatwa mkono baada ya kuhamishiwa hospitali ya
Taifa ya Muhimbili kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala.
Dkt. Ndugulile ametoa maagizo hayo wakati akizindua bodi ya nane ya
maabara binafsi za afya kwenye ukumbi wa Veta jijini hapa.
“Nilitegemea baraza la madaktari muwe mmeanza uchunguzi, kwahiyo
nakupa maagizo kesi hiyo muanze kufuatilia na kama itathibitika ni
uzembe waliohusika wachukuliwe hatua, ndani ya wiki mbili mtuletee
majibu ili mimi na Mhe. Waziri tujue tunachukua hatua gani.
Dkt. Ndugulile amesema kwenye mabaraza bado kuna changamoto ya baadhi
ya mashauri kuchukuliwa hatua hivyo kama mabaraza ya kitaakluma ni
vyema kuangalia ufanisi wa majukumu yao na kuchukulia hatua pale
taaluma inapokosewa na waliokosea wachukuliwe hatua.
Dkt. Ndugulile ameitaka bodi hiyo kusimamia usajili wa maabara zote
nchini kwani hivi sasa imetokea uanzishwaji wa maabara kiholela
zinazotoa huduma kwa wananchi bila ya kusajiliwa hivyo kufanya ukaguzi
ili kubaini maabara hizo na kuzichukulia hatua.
“Naomba sheria ifuate mkondo wake ili kubaini wale wote walioanzisha
huduma za maabara bila kufuata sheria na taratibu za usajili,
tushirikiane kuhakikisha kuwa hakuna taasisi au mtu atakayefungua au
kutoa huduma za maabara bila kusajiliwa”. Amesisitiza Dkt. Ndugulile.
Aidha, Naibu Waziri huyo amesema baraza hilo ni chombo muhimu na ndio
moyo wa sekta ya afya kwani maabara inatoa muelekeo wa mgonjwa kwa
kuthibitisha tatizo, hivyo inahitajika maboresho katika utoaji huduma
za maabara.
“Sasa hivi huduma hizi zimekua ni biashara kwani asiliamia 70 ya homa
wala sio Malaria ni virusi watu wanakunywa dawa sana pasipo kuzingatia
misingi kwani maabara hizi zinatumika kama sehemu ya matibabu na hata
upasuaji, mtu anaenda maabara anakaa dakika kumi na tano anaambiwa ana
UTI wakati mwingine anaambiwa ana malaria plasi plasi hii maana yake
ni nini hili linahitaji ufuatiliaji”. Alisema Dkt. Ndugulile.
Hata hivyo aliitaka bodi hiyo mpya kusimamia ubora wa huduma za
maabara ili kuinufaisha jamii na kuhakikisha huduma za afya katika
jamii zinaboreshwa kukidhi viwango vitavyotarajiwa na hivyo kuboresha
afya na maisha ya watanzania.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la maabara binafsi Prof. Said Abood
aliahidi kutekeleza maagizo yote waliyopewa na Naibu waziri ikiwemo ya
kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini maabara bubu na ambazo
hazijasajiliwa pamoja na kuhakikisha maabara zinatoa huduma
zinazostahili ili kuweza kumsaidia daktari kumpatia mwananchi huduma
stahili.

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt. Faustine Ndugulile alipokua akiongea wakati wa uzinduzi wa
bodi ya maabara binafsi za afya kwenye ukumbi wa hoteli ya Veta jijini
Dodoma.

Baadhi ya wasajili wa mabaraza ya kitaaluma yaliyo chini ya wizara ya afya wakimsikiliza Naibu Waziri(hayupo pichani) wakati wa uzinduzi huo.

Aliyekuwa mjumbe wa bodi iliyoisha muda wake Dkt. Charles
Massambu akipokea cheti cha shukrani kutoka kwa Naibu Waziri Dkt.
Faustine Ndugulile

Kaimu Msajili wa bodi ya Maabara binafsi Dickson Majige
akipokea cheti cha shukrani wakati wa uzinduzi huo

Picha ya pamoja mgeni rasmi na wajumbe wa bodi iliyomaliza muda wake

Naibu Waziri Dkt. Faustine Ndugulile akiwa kwenye picha ya
pamoja na bodi mpya ya nane ya baraza la maabara binafsi za afya.
No comments:
Post a Comment