HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 13, 2019

DAWASA WAKABIDHI MRADI WA MAJI WA MANEROMANGO KWA RUWASA

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam DAWASA wamekabidhi vifaa vya mradi wa maji wa Kisima  kwa Mamlaka ya maji Vijijini RUWASA kwa ajili ya kuutekeleza kwenye Mji wa Kisarawe.

Mradi huo utapeleka maji kwenye Shule ya Sekondari Maneromango na kutatua tatizo la maji kwa wanafunzi na walimu wa shule hiyo.

Akizungumza baada ya kupokea vifaa, Mkuu wa Shule ya Sekondari Maneromango Pili Jabir ameishukuru Mamlaka ya Dawasa kwa kuweza kuwapelekea maji kwenye shule yao kwani wamekuwa na adha ya maji kwa muda mrefu.

Amesema kumekuwa na kero ya maji katika shule hiyo na wanafunzi wamekuwa wanaenda kuchota maji kwenye visima vya wanakijiji kitu kinachopelekea kutopata muda toshelezi wa masomo.

" Napenda kuwashukuru Dawasa kwa kutuletea mradi huu, utawasaidia wanafunzi kuepukana na shida ya maji safi na salama iliyokuwa kwa muda mrefu na utawasaidia kupata muda mwingi wa kujisomea,"amesema Pili.

Kwa upande wa Mhandisi wa RUWASA Wilaya ya Kisarawe, Ally Nzwenge amesema wamepokea mradi huo wa kupeleka maji kwenye Shule ya Sekondari Maneromango na wanaahidi kuufanyia kazi ili kuondoa kero ya maji kwa wanafunzi.

"Mradi huu tutautekeleza kulingana na usanifu uliokuwa tayari umeshafanywa na Dawasa na wanashukuru sana kwa kuwakumbuka wanafunzi hao,"

Nzwenge amesema, kukamilika kwa mradi huu kutaondoa magonjwa ya mlipuko yaliyokuwa yanawakuta wanafunzi kwa kukosa maji safi na salama na pia utawasaidia kupunguza muda mwingi wa kwenda kuchota maji vijiji vya jirani.

Makabidhiano ya mradi huo yamefanywa na Mhandisi Lilian Masirago ukishuhudiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii Neli Msuya na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Maneromango Pili Jabir.

Vifaa hivyo vilikabidhiwa kwa Mwalimu Mkuu ambavyo ni pamoja na mabomba, mita ya kusoma maji, pampu, tanki lenye ujazo wa lita 10,000 na vingine vitakavyotumika kwenye mradi huo.
Mhandisi kutoka DAWASA Lilian Masirago na Mhandisi wa RUWASA Wilaya ya Kisarawe, Ally Nzwenge wakisaini makabidhiano ya mradi wa maji wa Shule ya Sekondari Maneromango utakaotatua changamoto ya maji kwa muda mrefu. Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii Neli Msuya (wa pili kushoti)na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Maneromango Pili Jabir (wa kwanza kushoto) na wafanyakazi wengine wa Mamlaka hiyo.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii Neli Msuya akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Maneromango Pili Jabir vifaa vya ujenzi wa mradi wa maji utakaosaidia kutatua kero ya maji kwenye shule hiyo kwa muda mrefu. Wengine ni wafanyakazi wa DAWASA na RUWASA.
Mabomba yatakayotumika kusambaza maji kwenye mradi wa maji wa Shule ya Sekondari Maneromango Kisarawe.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad