HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 28, 2019

Waziri Jafo alipongeza Jiji la Dodoma kwa kubuni miradi ya Maendeleo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanaweka mikakati ya kubuni miradi ambayo itawasaidia katika kujiwekea vitega uchumi na kukuza mapato katika Halmashauri zao ili kuachana na utegemezi katika Serikali.

Ameyasema hayo leo wakati wa utiaji wa saini Miradi ya Ujenzi wa majengo mawili ya vitega uchumi vya Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square, Jijini Dodoma.

Mhe Jafo amesema Halmashauri zote nchini zinatakiwa kuwa wabunifu, kujipanga na kuweka mikakati ya kuondokana na unyafuzi wa mapato kwa kuanzisha miradi ambayo itasaidia kuongeza mapato na kuleta maendeleo kwa jamii.

Amesema kuwa kama Halmashauri zote zingekuwa wabunifu na kuamua kujitoa katika utendaji kazi kusingekuwa na unyafuzi wa mapato bali zingejikita katika kubuni na kuibua miradi ya maendeleo ili kujikwamua kiuchumi na kujiongezea vitega uchumi vitakavyoleta maendeleo katika Halmashauri zao

“ Kusipokuwa na ubunifu, kujitoa katika utendajikazi wa watumishi wa Halmashauri, hali ya unyafuzi wa mapato itaendelea na bado Halmashauri nyingi zitakuwa ni tegemezi kwa Serikali, hivyo ninaziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanabuni vitega uchumi ili waweze kujitegemea kwa kutumia mapato yao ya ndani ” Anasisitiza Mhe.Jafo

Mhe. Jafo amezitaka Halmashauri zote nchini kuiga mfano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kubuni Miradi ya Maendeleo kwa ajili ya vitega uchumi na kuondokana na utegemzi kwa Serikali.

Amefafanua zaidi kuwa watumishi wa Serikali za Mitaa nchini kuacha kufanyakazi kwa maigizo, kwa kujionyesha kwenye mitandao bali wafanyekazi kwa weledi lengo likiwa ni kuwahudumia wananchi maskini na kulipeleka taifa katika uchumi wa kati

“Kuna watu nchi hii wamezoea maigizo, hivyo kwa wale ambao wapo chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuacha kufanyakazi kwa maigizo bali watu wafanyekazi kwa weledi ili kufikia mallengo ya Serikali.” Amesisitiza Mhe. Jafo

Amesema watu wasipende kujionyesha kwenye mitandao kuwa wanafanyakazi , bali wafanye kazi kwa ajili kulitumikia taifa hasa wananchi maskini kwa kuwa nchi hii inabadilika na kinachohitajika ni maendeleo ya Taifa.

Amewasii vijana waliopewa dhamana ya uongozi nchini kufanyakazi kwa bidii na maarifa waliyonayo na kuacha kufanyakazi kwa maigizo, lengo likiwa ni kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli katika kufikia uchumi wa kati.

Amewapongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuweza kutumia Makusanyo ya Fedha za Ndani kwa ajili ya ujenzi wa vitega uchumi lengo kubwa ni kutoa unyafunzi wa mapato na kupunguza utegemezi kwa Serikali.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Bilinith Mahenge amesema kuwa kupitia miradi hiyo Wananchi wa Mkoa wa Dodoma watapata fursa ambazo zitawasaidia kuongeza kipato na kukuza uchumi wa Dodoma utaongezeka .

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad