HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 6, 2019

WAFANYAKAZI WENGI HAWAZIJUI HAKI ZAO ZA UNYONYESHAJI NCHINI

Na Andrew Chale.

IMEELEZWA kuwa wafanyakazi wengi  hapa Nchini hawajizui haki zao za unyonyeshaji kutokana na dhana ya kutoelewa haki na wajibu wa sheria zilizopo.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam wakati wa semina ya Waandishi wa Habari  katika wiki ya unyonyeshaji maziwa ya Mama iliyoandaliwa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC).

Akitoa mada juu ya kanuni ya kazi na unyonyeshaji  maziwa ya mama, kanuni ya mwaka 2017, amebainisha kuwa, Mwanamke na Mwanaume wote kwa pamoja wanazo haki za uzazi kwa kila mmoja kulingana na haki hizo hata hivyo baadhi yao hawazijui haki zao.

“Mwanamke mwajiriwa anazo haki za kutimiza majukumu yake ya uzazi na kufanya kazi au kuzalisha bila kubaguliwa, kubugudhiwa au kupoteza ajira.
Likizo ya uzazi ikiwa ni moja ya haki za uzazi, humpa mama muda wa kumuwezesha kutoa matunzo muhimu kwa mtoto miezi ya mwanzo ya maisha yake hii ikiwa ni pamoja na kumnyonyesha.

Vilevile likizo ya uzazi humpa mwanamke mmwajiriwa muda wa kupumzika na hivyo kusaidia mwili wake kurudi hali ya kawaida baada ya kujifungua.  Kwa mantiki hiyo, ni muhimu mwajiri na mwajiriwa kufahamu vizuri haki na wajibu wao katika utekelezaji wa sheria hiyo” Alieleza Nchimbi.

Nchimbi aliongeza kuwa, katika sheria mpya  Mwanamke mwajiriwa anapaswa kumfahamisha mwajiri wake nia ya kuchukua likizo ya uzazi angalau miezi mitatu kabla ya tarehe ya makisio ya kujifungua akiwa ameambatanisha vielelezo vya madaktari.

“Mama ana haki ya kupewa likizo ya uzazi sio chini ya  siku 84 yenye malipo. Kwa mama aliyejifungua mtoto zaidi ya mmoja (mapacha au zaidi) anapaswa kupewa likizo ya uzazi  ya siku  100 yenye malipo.

Mama  ana haki ya kuchukua likizo yake ya mwaka  (siku 28) katika mwaka huo huo aliyopata likizo ya uzazi. Aidha anaweza kujadilina na mwajiri kuunganisha likizo ya uzazi na ya mwaka” alieleza Nchimbi.

Aidha, sheria hiyo imefafanua kuwa, endapo mtoto huyo atafariki, Mwanamke ana haki ya kupewa tena likizo ya uzazi ya siku 84 yenye malipo endapo mtoto wake atafariki kipindi cha mwaka mmoja tangu kuzaliwa.

Katika sheria hiyo mpya pia imebainisha kuwa, mwajiri aharuhusiwi kumpa mwanamke mwenye mimba au anayenyonyesha  kazi zinazohatarisha afya yake au mtoto.

“Mwajiri anapaswa kumpa mwanamke mjamziti ama mwenye mtoto kazi mbadala bila ya kwenda tofauti ya mkataba au makubaliano ya ajira yake.

Kisheria mwajiri anawajibika kumpa mwanmke mwajiriwa likizo nne tu za uzazi katika kipindi chote cha ajira. Pia mwajiri haruhusiwi kumuachisha kazi mwanamke kutokana na sababu zinazohusiana na ujauzito au kujifungua” alieleza Nchimbi.

Hata hivyo Nchimbi alimalizia kuwa, Mama anayenyonyesha ana haki ya kupewa  muda wa saa mbili  kwa siku wakati wa kazi kwenda kulimsha ama kumnyonyesha mtoto wake.

“Hii kuongeza namna ya kumsaidia mama, mwajiri na mwajiliwa wanaweza kukubaliana kutenga muda katika saa mbili za wakati wa kazi, wao watakavyoona lakini pia kwa sasa kuna utararibu umeanzishwa baadhi ya ofisi kuwa na sehemu ya mama kunyonyesha mtoto kwa muda huo, akiwa kazini” alimalizia Nchimbi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi idara ya Elimu ya lishe na mafunzo, Bi. Sikitu Simon amevipongeza vyombo vya habari nchini kwa kutoa ushirikiano namna ya kuripoti masuala ya lishe  kwani kupitia vyombo vyao ujumbe umekuwa ukifika kwa wakati.

“Navipongeza vyombo vya habari kwa namna vinavyofikisha habari muhimu juu ya lishe. Hivyo kupitia mafunzo haya yatakuwa chachu  kwenu kuendelea kuelewa vizuri na kwa kina ili mkawe mabalozi wazuri.

Milango ipo wazi watalaam wetu wapo hapa na mnakaribishwa muda wowote”alieleza Bi. Sikitu Simon.

Katika semina hiyo wanahabari kutoka vyombo mbalimbali waliweza kupata mafunzo yaliyowasilishwa kwa njia ya mada na watalaam wa taasisi hiyo huku pia wakipata wasaha wa kuuliza maswali na kujibiwa.

Afisa Utumishi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania, Maurice Nchimbi akiwasilisha mada juu ya likizo za uzazi kwa mwanamke wakati wa semina ya waandishi wa habari iliyofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
  Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakiwa  kwenyenye   semina hiyo.
Picha ya pamoja (Pichana na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad