WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Bashay, wilayani Karatu watumie fursa zinazojitokeza kwenye sekta ya utalii kuboresha maisha yao.
“Tumieni fursa ya uwepo wa eneo hili. Halmashauri wakishajenga vizimba vya biashara, leteni bidhaa zenu kama vile picha za tingatinga, mapambo, vinyago na vyakula vya asili ili watalii wakija hapa wapate huduma kutoka kwenu,” alisema.
Ametoa wito huo jana jioni (Jumapili, Julai 21, 2019) wakati akizindua mradi wa ujenzi wa vituo vya polisi vya kupunguza changamoto kwa magari ya utalii barabarani na kukabidhi gari la polisi kwa ajili ya patrol ya watalii katika eneo la Bashay, wilayani Karatu, mkoani Arusha.
Waziri Mkuu alizindua kituo cha kutolea huduma za usalama kwa watalii wilayani Karatu ikiwa ni ishara ya kuwakilisha vituo vingine vitatu vinavyoendelea kujengwa mkoani Arusha katika maeneo ya Kikatiti (Arumeru), Makuyuni (Monduli) na Engikaret (Longido).
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi wakazi hao wawalinde watalii ili waitangaze vema nchi ya Tanzania pindi wakirudi makwao. “Ili kukuza na kutangaza utalii, tunapaswa tuwe na mapenzi mema kwa watalii lakini kikubwa zaidi ni usalama wao.”
Aliwataka wakazi hao waendelee kuiamini Serikali ya awamu ya tano na waendelee kumuombea Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili apate nguvu ya kuleta maendeleo zaidi.
Pia aliwashukuru viongozi wa Tanzania Association of Tour Operators (TATO) kwa kuchangia ujenzi wa vituo hivyo na kutoa gari jipya la polisi kwa ajili kituo hicho cha Karatu. Gari hilo aina ya Toyota Landcruiser lililogharimu dola za Marekani 45,000, limepewa namba za usajili za PT 4190.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wakazi wa Bashay waliohudhuria hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo alisema ujenzi wa vituo hivyo umetokana na malalamiko aliyopokea kwamba watalii wakitoka uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) hadi kufika Karatu wanakuwa wamesimamishwa njiani zaidi ya mara 20.
“Tulijiuliza hawa watalii wamekuja kutalii, wanataka kupumzika, sasa ni kwa nini wasumbuliwe kiasi hicho? Tuliamua kuanzisha vituo vya aina hii, ili watalii wafanyiwe ukaguzi kwenye check-points maalum,” alisema.
Aliomba Jeshi la Polisi liwapange barabarani askari ambao ni weledi na wana uelewa wa masuala ya utalii na kutolea mfano wa wiki iliyopita ambapo alikuwa akitokea mjini kwenda Karatu na kukuta magari ya watalii zaidi ya 10 yamesimamishwa njiani.
“Niliona baadhi yao wakiwa wamelala kwenye magari kwa uchovu, nilipowauliza wamekalishwa kwa muda gani, walisema ni kwa zaidi ya dakika 45. Nilipomuuliza askari aliyewasimamisha ni kwa nini anafanya hivyo, akanijibu kwamba dereva amemjibu vibaya. Hivi ni kwa nini watalii wateseke juani wakati mwenye makosa ni dreva?”
Naye, Makamu Mwenyekiti wa TATO, Bw. Henry Kimaro aliishukuru Serikali kwa jitihada inazofanya za kupambana na ujangili na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini. “Tumeona hivi karibuni watalii wengine kutoka Israel, China na sasa ndege yetu imeanza kwenda India kuwafuata hukohuko,” alisema.
Alisema wameanza na vituo hivyo vinne mkoani Arusha lakini tatizo hilo liko maeneo mengi nchini na wao hawawezi kufika nchi nzima kutoa huduma kama hiyo. Hivyo, alimuomba Waziri Mkuu awahimize Wakuu wa Wilaya ambao wilaya zao zinajihusisha na sekta ya utalii, waige mfano wa wilaya ya Karatu ili kuhakikisha usalama wa watalii wawapo nchini.

Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Karatu Theresia
Mahongo, wakati alipofungua kituo cha huduma za utalii, katika Wilaya
ya Karatu, mkoani Arusha, Julai 21, 2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua kituo cha huduma za utalii, kilichopo
katika Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha kabla ya kukifungua rasmi, Julai
21.2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia kituo kidogo cha Polisi kilichopo
katika kituo cha huduma za utalii, wilayani Karatu, kabla ya kukifungua
rasmi, Julai 21.2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akipewa maelezo na Mrakibu wa Polisi Joseph
Bukombe, ndani ya kituo kidogo cha Polisi, kilichopo katika kituo cha
huduma za utalii wilayani Karatu, Julai 21.2019. Tokea kushoto ni Mkuu
wa Wilaya ya Karatu Theresia Mahongo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho
Gambo.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akizindua gari jipya la Polisi, lililokabidhiwa
kwa ajili ya kuwahudumia watalii, kwenye kituo cha huduma za utalii
wilayani Karatu, Julai 21.2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akikabidhi gari jipya la Polisi, litakalotumika
kwa ajili ya kuhudumia watalii, kwa Kaimu RPC Mkoa wa Arusha James
Manyara, kwenye kituo cha huduma za utalii wilayani Karatu, Julai
21.2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akizindua kituo cha huduma za utalii wilayani
Karatu, katika Mkoa wa Arusha, Julai 21.2019. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa
Arusha Mrisho Gambo.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akikata utepe kuzindua rasmi kituo cha huduma za
utalii wilayani Karatu, katika Mkoa wa Arusha, Julai 21.2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi, baada ya kuzindua rasmi
kituo cha huduma za utalii wilayani Karatu, katika Mkoa wa Arusha,
Julai 21.2019.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akipeana mkono na Mke wa Bwana Joseph Erro, Bibi
Evalina Madawe, ambaye amejitolea kiwanja kilichotumika kujengea kituo
cha huduma za utalii wilayani Karatu, katika Mkoa wa Arusha, Julai
21.2019. Kulia ni mtoto wa bwana Francis Theodosia. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu).
No comments:
Post a Comment