HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 23, 2019

WANAWAKE WAASWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UJENZI

Wito umetolewa kwa makandarasi wanawake kwenye mikoa ya Kanda za Magharibi na Nyanda za Juu Kusini kujitokeza na kuchangamkia fursa za miradi midogo inayojitokeza katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa mkoani Kigoma.

Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga, ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye mafunzo ya wiki mbili kwa makandarasi wanawake kutoka mikoa minne ya Kanda ya Magharibi na Nyanda za Juu Kusini kwa ajili ya kuwajengea uwezo ili kushiriki kwenye kazi za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara hapa nchini.

"Wanawake msilale changamkieni fursa za hii miradi na msing'ang'anie tu kazi hizi za kufyeka nyasi na kuzibua mitaro kwenye madaraja bali mjitokeza hata kwenye kazi za ujenzi wa barabara", amesisitiza Mhe. Anga.

Aidha, Mkuu wa Wilaya hiyo ameongeza kuwa fursa za utekelezaji wa miradi midogo kwenye miradi mikubwa inayo nafasi kubwa ya kuwajengea uwezo wa kitaalam na kifedha wahandisi wanawake nchini hivyo ni wajibu wao kutumia nafasi hiyo sasa ambapo mkoa wa Kigoma unayo fursa ya utekelezaji wa miradi mingi ya ujenzi ambayo wakandarasi wengi wanaweza kujitokeza na kuifanya.

Mhe. Anga amesema kuwa bado makandarasi wengi wanawake mkoani Kigoma hawajajitokeza kwa wingi kushiriki kwenye miradi ya ujenzi fursa ambayo inawanyima kukua kimtaji na uwezo wa utekelezaji wa kazi na miradi mingi ya ujenzi.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, amesema kuwa kwa sasa mkoa Kigoma unatekeleza mradi mkubwa wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 260 ambapo zipo kazi ambazo wakandarasi hao wanawake wanaweza kuzifanya.

Mhandisi Choma amesema kuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Sera ya uwezeshaji wanawake kiuchumi imeweka mkakati wa kuwasaidia na kuwapa kipaumbele kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa chini ya Wizara hiyo. 

Awali Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji Wanawake katika kazi za barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Gladiness  Kitaly, amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwapa ujuzi makandarasi hao wanawake kujua namna ya kuomba miradi ya barabara, taratibu za kujaza zabuni za maombi ya miradi, ufanisi wa teknolojia ya nguvu kazi katika kufanya matengenezo ya barabara katika maeneo ambayo yanatoa kipaumbele kwa wanawake.

Mafunzo hayo ya wiki mbili yameshirikisha wahandisi wanawake  kutoka katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Tabora na wenyeji Kigoma.
 Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga,  akifungua semina ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake makandarasi wa mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa na Katavi. Mafunzo hayo yanafanyika katika Chuo cha Veta mkoani Kigoma.
 Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Kigoma Mhandisi Narcis Choma, akizungumza na wanawake makandarasi kuhusu kuchangamkia fursa za kazi ya matengenezo ya barabara hasa kwa mkoa huo. Mafunzo hayo yamejumuisha wanawake makandarasi kutoka mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa na Katavi.
 Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wanawake kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta  ya Ujenzi) Mhandisi Gladiness Kitaly, akizungumza na wanawake makandarasi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya zaidi ya wiki moja kwa ajili ya kuwajengea ufanisi katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara, mkoani Kigoma.
 Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga,  akipokea asali kutoka mwanamke mkandarasi Bi. Rosemary Augen, ambaye pia anajishughulisha na biashara ndogondogo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wananawake makandarasi yanayofanyika mkoani Kigoma.
 Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga, akiwa katika picha ya pamoja na wanawake makandarasi kutoka mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa na Katavi mara baada ya kufungua mafunzo ya makandarasi hao ya kuwajengea uwezo, mkoani Kigoma.
Meneja wa Kanda ya Kati ya Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB), Mhandisi David Msekeni, akifundisha namna ya taratibu za kujisajili kupitia bodi hiyo kwa wanawake makandarasi kutoka mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa na Katavi walioshiriki semina ya kuwajengea uwezo, mkoani Kigoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad