HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 24 July 2019

UTUNZAJI WA VYANZO VYA MAJI UNAANZA KWAKO MWANANCHI- MZEE ALI

Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2019 Mzee Mkongea Ali amesema kazi ya kutunza vyanzo vya maji sio ya serikali peke yake inaanza na wananchi wenyewe. Hayo ameyasema baada ya Mwenge wa Uhuru kutembelea chanzo cha maji Kulungu kinachopatikana kwenye Kijiji cha Mkwalia Kitumbo chenye uwezo wa kuzalisha maji Lita Milion 1.8 kwa siku.

Akitoa salamu za Mwenge, Mzee Mkongea amesema vyanzo vya maji vinatakiwa kutunzwa na wananchi wanatakiwa kuwa wa kwanza kwenye kuhakikisha wanavitunza kwa kuacha kufanya shughuli za kijamii pembezoni.

Mkongea amesema, ili vyanzo viweze kudumu na kuwa endelevu kwa kizazi cha sasa na cha baadae na kuendelea kutoa huduma ya maji safi,  wananchi hawana budi kupanda miti rafiki inayopenda maji na ufugaji wa nyuki.

Amesema, Mwenge wa Uhuru umeridhishwa na utunzaji huu wa Chanzo cha Maji na amempongeza Mkuu wa Wilaya kwa hatua kubwa waliyoifanya kwa kuzungushia uzio na kupanda miti wakishirikiana na wananchi wa eneo hilo.

Kwa upande wa Hlamashauri ya Mkuranga, Afisa Mazingira Herman Basisi amesema kuna vyanzo kumi na nne katika wilaya vinavyoendelea kutunzwa na kuhifadhiwa kwa kusimamia uoto wa asili usiharibike.

Amesema, kuanzia mwaka 2008 miti 500 ilipandwa aina ya michuja na mikorosho poro ambayo ni rafiki wa vyanzo vya maji ili kuitunza isivamiwe na shughuli za kibinadamu.

Chanzo cha maji Kulungu kinapeleka maji kwenye Tanki la Hospital lenye ujazo wa lita Laki moja na tisini na tano (195,000) na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es salaa DAWASA wameanza ujenzi wa miundo mbinu ikiwamo kulaza mabomba na ujenzi wa tanki la maji la ujazo Lita Milioni 1.5

Pia, Mwenge wa Uhuru umezindua tanki la maji la ujazo wa lita laki moja (100,000) linalopatikana Mwanambaya litakalopokea maji kutoka kwenye chanzo cha Kulungu.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 Mzee Mkongea Ali akipanda mti kwenye eneo la Chanzo cha maji Kulungu baada ya Mwenge wa Uhuru kutembelea eneo hilo leo Mkoa wa Pwani. Picha ya Chini akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga baada ya kupanda mti kwenye eneo hilo.

 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 Mzee Mkongea Ali akiwa ameongozana na Mkuu wa Wilaya Mkuranga Filberto Sanga baada ya  kutembekea chanzo cha Maji Kulungu Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2019 ulipotembelea kujionea uhifadhi wa vyanzo vya maji bila kuharibu uoto wa asili.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 Mzee Mkongea Ali akiyagusa maji yanayotoka kwenye chanzo cha Maji Kulungu yanayotiririka kwa wingi.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 Mzee Mkongea Ali akipokea taarifa ya uhifadhi wa chanzo cha maji Kulungu uliosomwa na Afisa Mazingira Herman Basisi(kulia) baada ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 kutembelea chanzo hicho leo Mkuranga Mkoa wa Pwani.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad