HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 11, 2019

TEMESA TANGA YAALIKA WADAU KUSIKILIZA KERO ZAO

Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoa wa Tanga jana umealika wadau wanaotumia huduma zake ili kujadilli na kupata mrejesho kuhusu namna zinavyotolewa. Kikao hicho cha wadau kilichoandaliwa na meneja wa mkoa wa Tanga Mhandisi Margareth Gina kilifanyika katika eneo la wazi la karakana ya wakala huo na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa na wadau mbalimbali wa taasisi za umma, taasisi binafsi, wazabuni, pamoja na wauzaji wa vipuri vya magari na mitambo.

Awali, Akifungua kikao hicho, meneja wa TEMESA mkoa wa Tanga alisoma taarifa ya utendaji kazi kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ambapo taarifa hiyo imeonyesha kiwango kikubwa cha ukuaji wa uzalishaji ambapo hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu uzalishaji wa mkoa huo umeweza kufikia zaidi ya shilingi Bilioni moja nukta tano sawa na asilimia tisini nukta nne ya uzalishaji wa mkoa.

Mhandisi Margareth alizungumzia pia changamoto mbalimbali wanazokutana nazo ikiwemo kucheleweshewa malipo ya madeni wanayodai wateja hasa wa Umma, ‘’hadi kufikia Juni mwaka 2019 tunadai zaidi ya shilingi milioni mia sita, tunaendelea na usuluhishi wa madeni hayo na wateja wetu ili kuingiza deni sahihi katika taarifa zetu za fedha za mwaka,’’alisema.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle alieleza mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika Wakala ambapo huduma za karakana zimeanza kusogezwa kwa wateja wa mbali hasa uanzishwaji wa karakana mpya za Wilaya ikiwemo uanzishwaji wa karakana ya TEMESA katika Halmashauri ya mji wa Ifakara ambayo tayari imekwishaanza kufanya kazi.

‘’TEMESA imeanza kubadilika, tuna mpango wa kuanzisha karakana katika Wilaya ya Same, Wilaya ya Simanjiro, Wilaya ya Korogwe pamoja na Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, tumesambaza vifaa vipya vya kisasa kwa ajili ya karakana kumi na mbili na tayari vingine vipo kwenye mchakato wa manunuzi’’. Alisema Mhandisi Maselle.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa alimshukuru meneja kwa kumkaribisha kwenye kikao hicho kama mdau, pia aliipongeza TEMESA kwa ubunifu na hatua wanazochukua kutatua kero za wateja wao ambapo alisema malalamiko mengi kwa sasa yamepungua tofauti na hapo awali ambapo akiwa Wilayani Manyara malalamiko yalikuwa mengi sana na kwa sasa hayapo tena.

Nao baaadhi ya wadau walizungumzia kero zinazowakabili ikiwemo kucheleweshewa matengenezo ya magari, gharama kuwa juu pamoja na upungufu wa vipuri. Pia wadau hao waliomba mafundi wa karakana wapewe elimu ya kumhudumia mteja kwani wengi wao wamekuwa na kauli ngumu kwa wateja wao. 

Akijibu malalamiko hayo Mtendaji Mkuu alisema kucheleweshwa kwa matengenezo ni kutokana na kukosekana kwa vipuri katika karakana husika lakini tatizo hilo limekwishatatuliwa kwa kuwa sasa Mkoa wa Tanga una akiba ya kutosha ya vipuri, aliongeza kuwa Wakala sasa unaanzisha huduma ya kuhudumia wateja maarufu ambapo kipaumbele kitatolewa kwa wateja hasa wa magari ya viongozi ikiwemo wakuu wa Wilaya, wakuu wa Mikoa pamoja na Mawaziri ambao magari yao yatakuwa yakipatiwa huduma ya haraka pindi yanapofika katika karakana husika. Kikao kingine cha wadau kinategemewa kufanyika mkoani Kilimanjaro pamoja na mkoani Arusha siku ya Ijumaa.  
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle akizungumza na wadau (hawapo pichani) wakati wa kikao cha wadau kilichoandaliwa na Wakala huo kusikiliza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo, maoni na ushauri kuhusu huduma za TEMESA. Kikao hicho kilifanyika katika karakana ya mkoa wa Tanga. Kulia ni Meneja wa mkoa wa Tanga Mhandisi Margareth Gina na kushoto ni msaidizi wake Mahangaiko Ngoroma.
 Mkuu wa Wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa katikati akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa TEMESA mkoa wa Tanga kilichofanyika katika karakana ya wakala huo kwa ajili ya kupata maoni, ushauri na changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau wa TEMESA mkoani humo. Kulia ni Meneja wa mkoa wa Tanga Mhandisi Margareth Gina na kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Mhandisi Japhet Y. Maselle
 Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoa wa Tanga Mhandisi Margareth Gina kulia akisoma taarifa ya utendaji kazi ya karakana ya Wakala wakati wa kikao cha wadau (hawapo pichani) kilichofanyika katika karakana hiyo. Katikati ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle na kushoto ni Meneja msaidizi wa mkoa huo Mhandisi Mahangaiko Ngoroma.
 Baadhi ya wadau walioshiriki katika kikao cha wadau wa TEMESA mkoa wa Tanga wakichangia mada mbalimbali kuhusu utolewaji wa huduma za karakana ya mkoa huo wakati wa kikao kilichofanyika katika karakana ya TEMESA mkoa wa Tanga. Kikao hicho kiliandaliwa na meneja wa mkoa huo kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau hao na namna ya kuzipatia ufumbuzi.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle kushoto akifurahia jambo na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Thobias Mwilapwa katikati mara baada ya kumalizika kwa kikao cha wadau kilichofanyika katika karakana ya TEMESA. Kulia ni Meneja wa (TEMESA) mkoa wa Tanga Mhandisi Margareth Gina.
PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (TEMESA TANGA)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad