WAZAZI, walezi na walimu wametakiwa kushirikiana kwa pamoja ili
kufanikisha wanafunzi waanze wakiwa wadogo kutumia akili zao ipasavyo
kwa kutatua matatizo yao kwa sasa ili miaka ijayo wakiwa wakubwa
waweze kuwa wabunifu na kufanya maendeleo.
Katibu wa bodi ya shule ya awali na msingi New Light ya Mji mdogo wa
Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Oscar Gunewe aliyasema
hayo juzi wakati akizungumza na wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule
hiyo.
Gunewe alisema watotot wanapaswa kupewa nafasi na kukuzwa kiakili kwa
kutakiwa kufundishwa kujiamini na kutumia akili zao kutatua changamoto
walizonazo ili wakiwa wakubwa wasishindwe kuyatatua.
"Nchi zilizoendelea wanasema sisi wa Afrika hatutumii akili zote
tulizonazo katika kufikiri, hovyo yatupasa kuwajenga watoto katika
msingi wa kutumia akili zao kwa asilimia zote wakiwa wadogo katika
kifikiri, alisema.
Alisema maendeleo ya miaka ijayo ya nchi ya Tanzania inawategemea
watoto, kutokana na hali hiyo hayo yatakwama bila kujengwa msingi
imara katika malezi, makuzi na masomo bora hivi sasa.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo ya awali na msingi New Light, Tumaini Mbise
alisema wanajivunia shule hiyo kwani ina walimu wazuri wanaofundisha
ipasavyo hivyo wazazi na walezi wasiwe na hofu pindi wakiwaleta watoto
wao.
Mbise alitoa mfano wa mwanafunzi wa darasa la tatu wa shule hiyo
ambaye alishindikana jijini Arusha akiwa darasa la pili kutokana na
utukutu lakini wakaweza kumrudisha akawa na nidhamu.
"Siku ya kwanza alipofika hapa shuleni sisi walimu tulichoka kwani
alikuwa mtundu mara apande juu ya mti, lakini tuliweza kukaa naye na
kumpa ushauri bila kumchapa na sasa ni mtoto mwenye nidhamu na bidii
ya masomo," alisema.
Mmoja kati ya wazazi mwenye watoto kwenye shule hiyo Happy Kayumbo
aliwaomba wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa walimu wa shule hiyo
ili waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo katika kuwafundisha wanafunzi.
Kayumbo alisema baadhi ya wazazi na walezi huwa hawafiki shuleni kujua
maendeleo ya watoto wao hivyo wanapaswa kufika na wasisubiri hadi
waitwe kwenye vikao.
Wanafunzi wa darasa la sita wa shule ya awali na msingi New Light Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkpani Manyara wakiwa kwenye kikao cha wazazi, walezi na walimu wao.
Wanafunzi wa darasa la tatu wa shule ya awali na msingi New Light wakiwa kwenye kikao hicho cha wazazi, walezi na walimi wao.
Mmoja kati ya wazazi wa wanafunzi wa shule ya awali na msingi New Light ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara akiwa na mwanafunzi aliyepata zawadi ya kuwa wa kwanza katika darasa lake.
No comments:
Post a Comment