NA MWAMVUA MWINYI, KIBITI
Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Mzee Mkongea Ali amekemea kilimo
cha bangi kwani kinaharibu mazingira na kuweka rehani maisha na afya
ya watumiaji ambapo asilimia kubwa ni nguvu kazi ya Taifa ambayo ni
kundi la vijana.
Ameeleza,licha ya hayo serikali inaendelea kupambana na matumizi ya
madawa ya kulevya ikiwemo,milungi,cocaine,heroine, bangi pamoja na
kudhibiti mianya ya wauzaji wa madawa hayo ili kuokoa nguvu kazi hiyo
ambayo inaangamia siku hadi siku.
Hayo aliyasema wakati mbio za mwenge wa uhuru Jaribu Mpakani, kata ya
Mjawa wilayani Kibiti mkoani Pwani.
Mkongea alieleza Taifa letu bado kuna matumizi ya madawa ya kulevya
hivyo tushirikiane kudhibiti na kupambana na janga hilo .
"Chakusikitisha vijana hawa wanaita bangi kwa majina mengi kama vile
misuba,cha Arusha,jani,ganja,msokoto,Bob Marley na Jamaica lakini
ukweli unabaki pale pale bangi ni bangi tu, vijana tubadilike
tupambane na janga hili na tujiingize katika shughuli za kujenga Taifa
kuchapa kazi"alisisitiza Mkongea.

Hata hivyo, Mkongea aliwaasa vijana kuacha kuvuta bangi ,kujidunga
sindano za madawa ya kulevya kwakuwa wanakuwa hatarini kupata ugonjwa
wa ukimwi,moyo,ini,mapafu na hatimae kifo.
Akizungumzia suala la Ukimwi, mkimbiza mwenge kitaifa huyo alisema
ugonjwa huo bado ni hatari jamii ijilinde na kuwa waaminifu.
"Watanzania takriban milioni 1.4 wanaishi na VVU ,maambukizi mapya
kila mwaka ni watu 81,000 tuendelee kujikinga na kuwa na tahadhari na
maambukizi mapya"alibainisha .
Mkongea alieleza, mkoa wa Njombe unaoongoza kwa maambulizi nchini kwa
asilimia 11.4,Iringa asilimia 11.3,Mbeya asilimia 9.3,Mwanza asilimia
7.2 na Kagera 6.5 huku kitaifa ikiwa asilimia 4.7.
Kwa upande wake ,mkuu wa wilaya ya Kibiti ,GulamKifu alisema ,mwenge
wa uhuru ukiwa Kibiti utapitia miradi 13 yenye gharama ya bilioni
2.59.
Alieleza katika miradi hiyo ,mradi mmoja utafunguliwa,mmoja
utazinduliwa,miradi mitatu itawekwa jiwe la msingi na mingine nane
itatembelewa.
Nae mbunge wa viti maalum mkoani Pwani, ambae pia ni naibu waziri wa
nishati Subira Mgalu aliwahamasisha wananchi kujitokeza katika
shughuli za uwekaji jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa umeme Stigo
wilayani Rufiji,itakayofanyika Julai 26 mwaka huu.
Aliwaambia wananchi hao baada ya mradi huo kukamilika maeneo ambayo
hayajafikiwa na umeme yatanufaika na mradi huo .
No comments:
Post a Comment