HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 19, 2019

LUKUVI ATANGAZA KUANZISHWA OFISI ZA ARDHI KILA MKOA

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Waziri wa Adhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema Wizara yake itaanzisha ofisi mpya za ardhi katika kila mikoa ili kuboresha utoaji huduma za ardhi nchini.

Lukuvi alisema hayo jana wakati akifungua Mkutano wa siku tatu wa Wataalamu wa Sekta ya Ardhi nchini unahudhuriwa pia na Makatibu Tawala wa mikoa pamoja na Wakurugenzi wa halmashauri unaoendelea katika jiji la Dodoma.

Alisema, kutokana na mabadiliko hayo sasa huduma zote za ardhi zilizokuwa zikitolewa katika ofisi za ardhi za kanda sasa zitatolewa mkoani na wananchi hawatahangaika tena kufuata hati au kusajili kiwanja katika ofisi za Kanda.

Kwa mujibu wa Lukuvi, katika kila mkoa kutakuwa na Mkuu wa Idara ya Ardhi wa Mkoa sambamba na Mpima na Mthamini wa mkoa lengo likiwa kuondoa kero kwa wananchi waliokuwa wakipata shida ya kwenda umbali mrefu kufuata huduma za ardhi.

Pia Lukuvi alisema Wakuu wa Idara za Ardhi katika kila wilaya watapangwa upya kulingana na sifa na kufafanua kuwa suala Mkuu wa Idara kuwa na taaluma ya Afisa Nyuki au Misitu sasa halitakuwepo tena na wakuu hao watakuwa chini ya Wakurugenzi wa Halmashauri na kuhudhuria vikao vya menejimenti.

Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pia alipiga marufuku Maafisa Ardhi kujishughulisha na kazi binafsi zinazoendana na kazi walizoajiriwa nazo na kubainisha kuwa kufanya hivyo ni kutumia muda wa serikali kwa kazi binafsi.

Vile vile, Lukuvi alibainisha kuwa Wizara yake itaanzisha Kanzidata ya matapeli wa ardhi na kuwataka wananachi wanaowafahamu matapeli wote wa ardhi kumtumia majina ili awafuatilie na kuweka majina yao hadharani.

Katika kile kinachooneka kusikia kilio cha wananchi kuhusiana na gharama kubwa ya uuzaji viwanja, Lukuvi alizitaka halmashauri kuwa na bei ekekezi ya viwanja pamoja na upimaji mashamba kwa kuwa sasa hivi kumekuwa na gharama kubwa inayowafanya wananchi wa hali ya chini kushindwa kumudu gharama.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alieleza kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Ofisi za Ardhi za Kanda lakini bado malengo ya kuwaondolea kero wananchi katika eneo hilo haijafikiwa.

Aliwataka Watendaji wa Sekta ya Ardhi nchini kuzingatia suala la huduma kwa mteja wakati wa utendaji kazi wao wa kila siku ili kuwaondolea kero wananchi wanaohitaji huduma za ardhi.

Aidha, aliwaonya washiriki wa mkutano huo ambao ni Maafisa Ardhi, Maafisa Mipango Miji na Wapima kuwa Uafisa Ardhi Mteule wa eneo lolote unaweza kukoma iwapo Afisa huyo hatatenda kazi yake vizuri ya kuwahudumia wananchi.
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na Wataalamu wa Sekta ya Ardhi katika mkutano wa Wadau wa Sekta hiyo unaofanyika kwenye ukumbi wa Dodoma Convention Center jijini Dodoma.
  Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Wataalamu wa Sekta ya Ardhi katika mkutano wa Wadau wa Sekta hiyo unaofanyika kwenye ukumbi wa Dodoma Convention Center jijini Dodoma.
 Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Wataalamu wa Sekta ya Ardhi unaofanyika kwenye ukumbi wa Dodoma Convention Center jijini Dodoma.
 Baadhi ya Makatibu Tawala wa Mikoa wakiwa katika Mkutano wa Wataalamu wa Sekta ya Ardhi unaofanyika kaika ukumbi wa Dodoma Convention Center jijini Dodoma jana. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad