HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, July 6, 2019

Hukumu za Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa mashauri manne


Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana kwa siku mbili Juni 22 na Juni 23,2019 ilisikiliza mashauri 4 na baadaye kuyatolea hukumu.

Shauri la Kwanza 

ERICK AMBAKISYE

Mlalamikiwa katika shauri hili hakuwepo katika kikao hiki licha ya kwamba taarifa ya wito ilitumwa kwa njia ya E-mail mnamo tarehe 16 Juni 2019 na kwa EMS Mnamo tarehe 17 Juni 2019 na risiti ya malipo ya kutumia nyaraka hizo iliwasilishwa mbele ya kikao kwa ajili ya uthibitisho lakini hata hivyo Mlalamikiwa hakutokea katika kikao hiki.Baada ya uthibitisho huo Kikao kiliazimia kuendelea bila uwepo wa Mlalamikiwa kwakuwa inaonekana alipata wito lakini hakutoa taarifa yoyote ya udhuru.

Tuhuma zilizomkabili ERICK AMBAKISYE ni mbili akiwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Songwe kama ambavyo zinaonekana katika hati ya mashtaka.

Pamoja na tuhuma hizo Mlalamikaji alikuwa na shahidi mmoja Nugu JAMES MHAGAMA ambaye aliitwa kwa nia ya kuthibitisha tuhuma hizo,Ambapo Shahidi alieleza namna ambavyo Mlalamikiwa alifanya vitendo kinyume na Katiba ya TFF ikiwemo kutokutoa ushirikiano kwake akiwa kama Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya TFF,Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Msimamizi wa RCL Kituo cha Songwe.

Changamoto kubwa ilikuwa ni kuzuia kwa Maafisa,Waamuzi na watahmini wa mechi kutokana na deni la Tshs 5,700,000 na hatimaye shahidi huyu kufunguliwa kesi katika Mahakama ya Mwanzo Mkoani Songwe na kuwekwa ndani kwa siku tatu baada ya kukosa dhamana kitendo kilichofanywa na mmiliki wa hoteli ya Mkulima ambayo viongozi waliyofikia.

Pamoja na juhudi zote za kusuluhisha mgogoro huu na fedha kulipwa lakini Mmiliki wa hotel aliendelea kuwaghasi viongozi hao kwa kushirikiana na Mlalamikiwa.Kimsingi Mwenyekiti alitoa taarifa kuwa maandalizi yamekamilika na kila kitu kinaenda sawa jambo ambalo si kweli na hakuwahi kuonekana kipindi chote cha mashindano kuanzia tarehe 27 Machi 2019 hadi 9 Aprili 2019.Shahidi alifafanua zaidi kwa kusema kwamba mwenye mamlaka ya kuomba kituo ni Mkoa husika baada ya kujiridhisha kuwa umekamilisha maandalizi yote kwa ajili ya kuendesha mashindano ya RCL.

Wajumbe walipata fursa ya kumuuliza shahidi maswali mbali mbali kuhusiana na ushahidi uliotolewa kwa nia ya kujiridhisha kabla ya kutoa maamuzi katika shauri hili.

UAMUZI
Kamati imepitia vizuri mashtaka mawili dhidi ya Mlalamikiwa pamoja na ufafanuzi uliotolewa na Mlalamikaji akiungwa mkono na ushahidi wa Ndugu JAMES MHAGAMA ambaye alikuwa Mkoani Songwe wakati mashindano hayo yakiendelea.

Pia Shahidi ni mhanga wa vitendo visivyo vya kiungwana vilivyofanywa na Mlalamikiwa dhidi yake ikiwepo kufikishwa mahakamani kwa madai ya fedha ambayo yalilipwa na TFF lakini bado alifunguliwa kesi na kulazwa mahabusu baada ya kukosa dhamana.

Hii yote ilitokana na udhaifu ulionyeshwa na Mlalamikiwa katika uaandaaji wa mashindano haya ya RCL Kituo cha Songwe.

Kamati imeona kwamba TFF ilijitahi kuwa na mawasiliano yakaribu na Mlalamikiwa ili kujitahidi kuepesha fedheha hiyo lakini hakuonyesha juhudi zozote katika kutatua mgogoro huu zaidi ya kumtaka mimiliki wa hotel aendelee kudai fedha yake kwakuwa wageni/Viongozi wa TFF wanakaribia kuondoka na hata lipwa fedha zake jambo ambalo halikuwa na chembe ya ukweli.

Hivyo Kamati imejiridhisha kwamba Mlalamikiwa alikuwa na nia mbaya dhidi ya Shirikisho na hakujipanga kwa namna yoyote kuandaa mashindano haya na kutoa taarifa zisizo sahihi kuwa Mkoa una uwezo wa kuandaa mashindano jambo ambalo si kweli na kuonekana hana mahuasiano mazuri na viongozi wenzake akiwemo Katibu wake ambaye alitoa ushirikiano mkubwa tangu kuanza kwa mashindano hayo.

Pia kitendo cha kuto hudhuria kusikilizwa kwa shauri hili pasipo kutoa udhuru wowote inaonekana jinsi Mlalamikiwa alivyokusudia kutotoa ufafanuzi ambao ungekuwa ni utetezi wake kutokana na tuhuma ambazo zinamkabili.

ADHABU
Baada ya kupitia kwa kina ushahidi wa Mlalamikaji na vitendo vilivyoonyeshwa na Mlalamikaj, Kamati inamtia hatiani Mlalamikiwa kwa kumpa adhabu ya kutojihusisha na shughuli za Mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka mitano (5) kwa mujibu wa Kanuni ya 73 ya Kanuni za Maadili za TFF za Mwaka 2013.
 
 
Shauri la Pili 
 
ATHUMAN KILUNDUMYA

Mlalamikiwa hakuwepo katika kikao hiki isipokuwa aliwakilishwa na Ndugu MAULID MWIKALO ambaye aliwasilisha mbele ya Kamati barua ya uwakilishi toka kwa Mlalamikiwa.

Mwakilishi alifafanua kwamba Mlamikiwa ni mtumishi wa Umma na ameshindwa kufika mbele ya Kamati kwa kuwa ana majukumu mengine kwa Mwajiri wake Mkoani Tabora.

Baada ya uthibitisho huo Kikao kiliazimia kuendelea na shauri kwakuwa Mwakilishi wa Mlalamikiwa alikuwepo.

Tuhuma tatu ambazo zinamkabili Ndugu ATHUMANI KILUNDUMYA akiwa ni Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora kama ambavyo zinaonekana katika hati ya mashtaka.

Mlalamikiwa aliingiziwa fedha kiasi cha Tshs 680,000/= kwa ajili ya kuhudhuria mkutano Mkuu wa TFF Jijini Arusha katika akaunti yake Namba 51001612542 iliyopo katika Benki ya NMB mnamo tarehe 29 Januari 2019 lakini hakudhuria kikao hicho ingawa fedha alipata na hata alipotakiwa kurejesha fedha hizo alikaidi maelekezo ya TFF.

Mlalamikiwa pamoja na kutuma Mwakilishi aliwasilisha utetezi wake kwa njia ya maandishi na katika tuhuma zote tatu alitoa majibu ya kufanana kuwa hajawahi kupokea fedha hizo wala maelekezo ya namna ya kurejesha fedha hizo na alijipanga kwa safari bahati mbaya safari yake iliishia Wilayani Nzega baada ya kuitwa kazini na Mwajiri wake kwani yeye ni Mtumishi wa Umma.

Hata hivyo Mwakilishi wa Mlalamikiwa alifafanua kuwa ni kweli Mlalamikiwa hakudhuria mkutano huo jijini Arusha pia ni hivi karibuni ndio amebaini uwepo wa fedha katika akaunti yake kwa zaidi ya miezi mitano isipokuwa mpaka sasa hajapewa utaratibu wa kurejesha,Iwapo atapewa utaratibu huo yupo tayari kurejesha fedha hizo kiasi cha Tshs 680,000/=.

Kamati ilimuuliza maswali ili kupata ufafanuzi wa iwapo aliingiziwa fedha hizo na kwakuwa hakuhudhuria Mkutano Mkuu Jijini Arusha kuanzia tarehe 2 Februari 2019 basi anapaswa kurejesha,Mwakilishi alikiri kuziona fedha isipokuwa hajaambiwa taratibu za kurejesha na akipewa hata leo yupo tayari kurejesha.

UAMUZI
Kamati imepitia vizuri mashtaka matatu dhidi ya Mlalamikiwa pamoja na ufafanuzi uliotolewa na Mlalamikaji na utetezi wa maandishi wa Mlalamikiwa ukiungwa mkono na ushahidi wa Ndugu MAULIDI MWIKALO,Kamati imejiridhisha kwamba Mlalamikiwa ametenda makosa yote matatu na hakuna utetezi wa msingi uliotolewa na ikizingatiwa kwamba maelezo yake na ufafanuzi wa Mwakilishi unaonekana kukinzana.Fedha kiasi cha Tshs 680,000/= kiliingizwa kwa Mlalamikiwa kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano Mkuu wa TFF Jijini Arusha katika akaunti yake Namba 51001612542 iliyopo katika Benki ya NMB mnamo tarehe 29 Januari 2019 lakini hakuhudhuria kikao hicho ingawa fedha alipata na hata alipotakiwa kurejesha fedha hizo alikaidi maelekezo ya TFF.

Mkanganyiko wa maelezo yake unaonekana Mlalamikiwa si muaminifu pamoja kuwa ni mtumishi wa umma na hakuwasilisha vielelezo vyote ili kuonyesha kwamba alisafiri ingawa safari yake iliishia njiani na Mwakilishi wake hajui aina ya usafiri ambao ulitumiwa na Mlalamikiwa wala tarehe ya safari hivyo alikusudia kutumia fedha hizo kwa makusudi yasiyokusudiwa.

Mlalamikiwa akiwa mtumishi wa Umma anafafahamu taratibu za kurejesha fedha ambazo hazikutumika kwa lengo lililopangwa na kama angeona ni utaratibu tofauti basi alipaswa kufanya mawasiliano na viongozi wake waliondaa Mkutano huo jambo ambalo hakulifanya.

Maelezo kwamba fedha hii ameiona katika akaunti yake wili moja iliyopita yanaonekana hayana ukweli wowote.

ADHABU
Baada ya kupitia kwa kina ushahidi wa Mlalamikaji na vitendo vilivyoonyeshwa na Mlalamikaji hasa ubadhirifu wa fedha za Taasisi, Kamati inamtia hatiani Mlalamikiwa kwa kumtaka kwanza arejeshe fedha hizo kwenye taasisi, pili kumpa adhabu ya kutojishusisha na shughuli za Mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka mitano (5) kwa mujibu wa Kanuni ya 73 ya Kanuni za Maadili za TFF za Mwaka 2013 tatu,TFF kumchukulia Mlalamikaji hatua za jinai iwapo itaona inafaa kwa ubadhirifu wa fedha alioufanya .
 
 
Shauri la Tatu 
 
CONSTATINE MORANDI

Tuhuma tatu ambazo zinamkabili Ndugu CONSTATINTE MORANDI akiwa ni Mwenyekiti wa Geita Gold Football Club kama ambavyo zinaonekana katika hati ya mashtaka.

Mlalamikiwa alizuia kuonyeshwa moja kwa moja na Azam TV kwa mechi ya mchezo wa mchujo play off kati ya timu yake dhidi ya Mwadui,Pia alikaidi maelekezo ya ufafanuzi wa kuonyeshwa kwa mechi hiyo kutoka katika shirikisho na kufanya vitendo vilivyoshusha hadhi ya TFF.

Mlalamikiwa katika utetezi wake alikana tuhuma zote tatu kuwa hakuhusika katika vitendo hivyo wala maandalizi ya mchezo huo kwa kuwa katika kipindi chote hicho alikuwa wilayani Chato katika kikao cha Wenyeviti wa Halmashauri kwa kuwa yeye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Geita,Hivyo alifika siku ya mchezo Timu zikiwa tayari na maandalizi yote yalifanywa na viongozi wenzake hasa Katibu wa Klabu ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za Klabu yao.

Aliiomba Kamati imuone hana hatia kwakuwa hakuna mawasiliano yoyote aliyofanya na TFF kwa niaba ya Klabu kuhusiana na mechi hiyo na hajawahi kuwazuia watu wa Azam TV kuonyesha moja kwa moja (Mubashara) mechi yao ya mchujo dhidi ya Mwadui,Hivyo alimalizia kwa kusema hakushiri katika kikao chochote cha maandalizi ya mechi hiyo kutokana kuwa nje ya Mji kwa muda huo wakati maandalizi yanafanyika.

Kamati ilimuuliza maswali ili kupata ufafanuzi hasa ushiriki wake katika kuzuia mechi, utendaji wa klabu yao namna mawasiliano yanavyofanyika ya kutoka nje ya Klabu yao,Majibu yake ni kuwa Katibu wa Klabu ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za kila siku na yeye huwa anapewa tu taarifa na kubariki lakini hili la kuzuia mechi hakushirikishwa.

UAMUZI
Kamati imepitia vizuri mashtaka matatu dhidi ya Mlalamikiwa pamoja na ufafanuzi uliotolewa na Mlalamikaji na utetezi wa Mlalamikiwa na kuona kwamba upande wa Mlalamikaji umeshindwa kuthibitisha tuhuma zote tatu dhidi ya Mlalamikiwa,Mlalamikiwa hakushiri kuzuia kuonyeshwa kwa mchezo kwakuwa hakuna uthibitisho wowote uliotolewa,Hakuwahi kupewa maagizo au maelezo yoyote toka TFF na kuyakaidi na wala hakufanya vitendo vyovyote vile ambavyo vilishusha hadhi ya TFF Kinyume na Ibara ya 50 (1) vya Katiba ya TFF.Hivyo kwa ujumla mashtaka dhidi yake hayajathibitishwa.

ADHABU
Baada ya kupitia kwa kina tuhuma dhidi ya Mlalamikiwa, Ushahidi wa Mlalamikaji na Utetezi wa Mlalamikiwa, Kamati imemuona Mlalamikiwa hana hatia yoyote na inamuachia huru.


Shauri la Nne 

SEIF KULUNGE

Tuhuma tatu ambazo zinamkabili Ndugu SEIF KULUNGE akiwa ni Katibu wa Geita Gold Football Club kama ambavyo zinaonekana katika hati ya mashtaka.

Mlalamikiwa alizuia kuonyeshwa moja kwa moja na Azam TV kwa mechi ya mchezo wa mchujo play off kati ya timu yake dhidi ya Mwadui.Pia alikaidi maelekezo ya ufafanuzi wa kuonyeshwa kwa mechi hiyo kutoka katika shirikisho na kufanya vitendo vilivyoshusha hadhi ya TFF.

Katika shauri hili Mlalamikaji aliwasilisha vielelezo mbalimbali ambavyo ni barua za mawasiliano kati ya Mlalamikaji,Bodi ya Ligi dhidi ya Mlalamikiwa ili vielelezo katika ushahidi wake na Kamati ilivipokee kwa kuwa hakukuwa na pingamizi lolote.

Shahidi wa Mlalamikaj iambaye ni Msimamizi wa Matangazo ya Moja kwa moja kutoka kituo cha Azam TV aliileza kamati kuwa alikuwa Geita katika Uwanja wa Nyankumbu kwa ajili ya maandalizi ya kuonyesha mechi hiyo lakini walizuiwa getini kwa maelezo kuwa mechi hiyo haitaonyeshwa mubashara la sivyo watapasua gari la matangazo,Hivyo kama msimamizi alichukua jukumu la kuwasiliana na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi ambaye alimuunganisha kwa kiongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoani Geita Ndugu PIUS KIMISHA ambaye alimpa ushirikiano mkubwa,Kimsingi alieleza hakuwafahamu watu hao isipokuwa lilikuwa ni kundi la Vijana waliokuwa getini kuanzia saa tatu asubuhi hivyo mechi hiyo haikuonyeshwa kutokana na vitendo vya vijana hao.

Mlalamikiwa katika utetezi wake alikana tuhuma zote tatu kuwa hakuhusika katika vitendo hivyo wala maandalizi ya mchezo huo kwa kuwa katika kipindi chote hicho alikuwa anaumwa hapa Kigamboni Jijini Da Es Salaam na hajaenda Geita zaidi ya Miezi sita.

Alifafanua kuwa mnamo tarehe 2 Juni 2019 alipigiwa simu na Katibu wa TFF kwa kumuuliza yupo wapi kwa wakati huo,Ambapo baada ya muda kidogo alipigiwa tena simu kuwa kuna watu wamezuia gari la matangazo la Azam TV na alimjibu kuwa hafahamu watu waliozuia ingawa watu walikuwa wanahoji uhalali wa matangazo hayo na faida kwa Klabu ukizingatia kuwa timu inategemea viingilio vya mashabiki na Katibu akamsihi aruhusu na matatizo hayo yatamalizwa.Shahidi anasema alifanya juhudi binafsi za kuwasihi watangazaji wa Azam warejee kuonyesha mechi ambapo aliwasiliana na Watangazaji hao ambao ni Pascal Kabombe na Ahmed pia alimtaarifu Katibu Msaidizi wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Geita lakini juhudi zake hazikuzaa matunda.Azam TV walimjibu kuwa maandalizi yao yanachukua muda mrefu hivyo hawako tayari kurejea na usalama wao ni mdogo hasa mali.

Mlalamikiwa alikiri kuwa kulikuwa na mawasiliano baina yake na TFF pamoja na Bodi ya Ligi kwa emails na njia ya simu.

Kamati ilimuuliza maswali ili kupata ufafanuzi hasa ushiriki wake katika kuzuia mechi, utendaji wa klabu yao namna mawasiliano yanavyofanyika ya kutoka nje ya Klabu yao,Majibu yake ni kuwa hakuzuia mechi kuonyeshwa na yeye kama Katibu wa Klabu ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za kila siku na yeye huwa anawasilisha taarifa za utendaji kwa Mkurugenzi wa Mji kwakuwa timu hiyo si ya wanachama ni ya Halmashauri hivyo hakuna viongozi wengine,Pia alikiri kuandika barua kwenda TFF ili kujua namna ambavyo Klabu yao itanufaika na matangazo ya moja kwa moja ya mechi yao na alipata ufafanuzi toka kwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi.

UAMUZI
Kamati imepitia vizuri mashtaka matatu dhidi ya Mlalamikiwa pamoja na ufafanuzi uliotolewa na Mlalamikaji na utetezi wa Mlalamikiwa hasa vielelezo na kubaini kwamba kulikuwa na mawasiliano ya pande tatu juu ya uhalali wa mechi hiyo kuonyeshwa ambao ni Mlalamikaji,Bodi ya Ligi na Mlalamikiwa jambo ambalo halikupingwa na Mlalamikiwa.

Kamati imemtia hatiani Mlalamikiwa katika tuhuma zote tatu kwa kuwa ameonekana kushiriki katika kuzuia, kukosa uaminifu ikizingatiwa alikiri kuwepo mawasiliano baina yake na TFF na Bodi ya Ligi hasa barua yake ya ufafanuzi kwenda Bodi ya tarehe 31 Mei 2019 yenye Kumb na. GGFC/350/GT ambapo aliomba ufafanuzi wa mambo matano na ninakuu jambo la tano aliloliomba "Natumaini mawazo na ombi letu kama hakuna majibu au malipo ya pesa hatutakubali kuonyesha mubashara mechi yetu maana haina faida na timu" Kauli hii inathibitisha namna ambavyo Mlalamikiwa alishiriki katika kuhamasisha mechi isionyeshwe pamoja na kupewa ufafanuzi kutoka Bodi ya Ligi,Pia ni dhahiri kwamba hakuonyesha uaminifu kwa TFF ikizingatiwa kwamba alifanya maawasiliano na kupewa ufafanuzi kuanzia tarehe 31 Mei 2019 hadi 2 Juni 2019 na mwishoni akakiri makosa hayo kwa kukiri makosa na kupokea ushauri kwa mikono miwili na kuahidi kuimarisha ulinzi kwa mujibu wa email ya Mlalamikiwa kwenda TFF,vitendo hivyo vilishusha hadhi kwa wadau mbalimbali waliohudhuria mechi hiyo tangu siku ya kwanza.

ADHABU
Baada ya kupitia kwa kina tuhuma dhidi ya Mlalamikiwa, Ushahidi wa Mlalamikaji na Utetezi wa Mlalamikiwa, Kamati inamtia hatiani Mlalamikiwa kwa kumpa adhabu ya kutojihusisha na shughuli za Mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka mitano (5) kwa mujibu wa Kanuni ya 73 ya Kanuni za Maadili za TFF za Mwaka 2013.

Kwakuwa vitendo vyake vingweza kuhatalisha usalama wa raia na mali zao hasa wapenzi wa mpira waliofika uwanjani kwa siku hiyo,Kitendo hicho kingeweza kuwaondoa Azam TV na wadhamini wengine kutodhamini mpira wa miguu nchini Tanzania,Hivyo kama kuna hasara iliyotokea basi Mlalamikiwa anapaswa kurejesha au kufidia hasara hiyo.


Wakili Kichere Mwita Waissaka
Mwenyekiti Kamati ya Maadili,TFF
Julai 5,2019

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad