HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 25, 2019

ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 30 KUSHINDANIWA SIMIYU JAMBO FESTIVAL 2019

Na Stella Kalinga, Simiyu
Tamasha kubwa la michezo ambalo hufanyika kila mwaka Mkoani Simiyu (Simiyu Jambo Festival) linatarajiwa kufanyika Juni 30, mwaka huu katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi huku takribani shilingi milioni 32 zikishindaniwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 25, Mratibu wa tamasha hilo Bi. Zena Mchujuko amesema Mgeni rasmi katika Tamasha hili anatarajiwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson.

Amesema katika Tamasha hilo kutafanyika mashindano ya mbio za baiskeli wanaume na wanawake, mbio fupi kilometa tano wanaume na wanawake na mashindano ya mdahalo kwa wanafunzi wa shule za sekondari.

“Jumla ya shilingi milioni 32 zitashindaniwa kwa michezo yote, mshindi wa kwanza mbio za baiskeli kwa wanaume atapata 1,000,000, Wanawake 700, 000, walemavu 500, 000 na tutatoa zawadi mpaka kwa mshindi wa 25; ngoma za asili mshindi atapata 1,000,000” alisema Bi. Zena

Aidha, amesema fomu za ushiriki zinapatikana kataika ofisi ya Chama cha Baiskeli Mkoa wa Simiyu Mjini Bariadi na katika Tovuti: www.simiyutalent.co.tz kwa gharama za shilingi elfu tano(5000) kwa mashindano ya baiskeli na shilingi elfu mbili (2000) kwa ajili ya mashindano ya mbio fupi.

Katika hatua nyingine Bi. Mchujuko amesema kupitia Tamasha la Simiyu Jambo Festival jamii ya watu wa Simiyu itapata ujumbe wa kupinga mimba za utotoni jambo litakalopelekea watoto wa kike waweze kutimiza ndoto zao kupitia Kauli Mbiu ya Tamasha ambayo ni :-WEZESHA MTOTO WA KIKE ATIMIZE NDOTO ZAKE, INAWEZEKANA KUZUIA MIMBA KATIKA UMRI MDOGO”

Mratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu Duniani(UNFPA) Mkoa wa Simiyu, Dkt. Amir Batenga amesema shirika hilo limekuwa likishirikiana na Serikali katika jitihada za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, ambapo waathirika wakubwa ni wasichana wenye umri mdogo, hivyo anaamini kupitia Tamasha hilo wananchi watapata ujumbe mahususi wa kukabiliana na mimba katika umri mdogo.

Naye Katibu wa Chama cha Mbio za Baiskeli Mkoa wa Simiyu, Bw, Samwel Richard washiriki takribani 260 kutoka mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara, Mwanza, Geita na Kagera wanatarajia kushirikia mashindano ya baiskeli, huku akiwahakikishia wananchi kuwa wachezaji wao wamejiandaa vizuri na wamekuwa kambi kwa takribani wiki mbili.

Kwa upande wake Kiongozi wa Ngoma za Asili Mkoa wa Simiyu, Bw. Buhimila Shala amesema kupitia ngoma za wagika na wagalu watatoa ujumbe uliobebwa na Kauli mbiu ya Tamasha kwa lengo la kuwaokoa wasichana kupata mimba katika umri mdogo.

Tamasha la Simiyu Festival mwaka 2019 limedhaminiwa na Jambo Food Products Company, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani-UNFPA, NGM Gold Mine Limited, NGS Petroleum, Alliance Ginneries Limited, Busega Mazao Limited, Maswa Standard Chalk, Ms Hotel na Vetreces Company Limited.
 Mratibu wa Tamasha la Simiyu Jambo Festival Bi. Zena Mchujuko(kulia) akizungumza na waandishi wa habari na kutoa taarifa ya tamasha hilo ambalo linatarajiwa kufanyika Juni 30, 2019 Mjini Bariadi.
 Mratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu Duniani(UNFPA) Mkoa wa Simiyu, Dkt. Amir Batenga(kushoto) akizungumza na waandishi wa habari na kutoa taarifa ya namna Shirika hilo liakavyotumia Tamasha la Simiyu Jambo Festival kupeleka ujumbe wa Kupinga mimba za utotoni tamasha ambalo linatarajiwa kufanyika Juni 30, 2019 Mjini Bariadi.
 Kiongozi wa Ngoma za Asili, Bw. Buhimila Shala (kushoto) akizungumza katika Mkutano wa Waandishi wa Habari na kueleza namna ngoma za asili zitakavyopamba Tamasha la Simyu Jambo Festival ambalo linatarajiwa kufanyika Juni 30, 2019.
Katibu wa Chama cha Baiskeli Mkoa wa Simiyu, Bw. Samwel Richard(kulia) akizungumza na waandishi wa habari juu ya namna chama hicho kilivyojiandaa na mashindano ya baiskeli katika Tamasha la Simiyu Jambo Festival, linalotarajiwa kufanyika Juni 30, 2019

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad