Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amewataka
Wananchi waache tabia ya kuwatishia maisha Askari wanyamapori wa
vijiji (VGS) wakati wanapowakataza wananchi hao kuendesha shughuli za
kibinadamu katika maeneo ya mtawanyiko na mapito ya wanyamapori
(shoroba)
Kufuatia hali hiyo, Mhe.Kanyasu amemtaka Mkuu wa wilaya ya Namtumbo,
Mhe. Sophia Mfaume afanye uchunguzi kwa kutumia vyombo vyake vya
usalama ili kuwabaini Wananchi hao wanaowatishia Askari
wanapotekeleza majukumu yao na watakaobainika hatua kali za kisheria
zichukuliwe dhidi yao.
Mhe. Kanyasu, ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya
Askari 20 wa Wanyamapori wa Vijiji wa kutoka mikoa ya Ruvuma, Mbeya
na Singida waliohitimu mafunzo hayo katika Chuo cha Mafunzo ya
Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu Sekamaganga kilichopo
katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma
“leo mmehitimu na tumewaapisha, mmekuwa askari kweli lakini tambueni
kuwa kazi za kiuchumi zinapelekea uharibifu mkubwa sana wa mapito ya
wanyama, nendeni mkawaelimishe wananchi wasiendelee kuharibu kwa
ustawi wa hifadhi zetu"
Amefafanua kuwa maeneo ya mtawanyiko na shoroba lazima zilindwe ili
kuruhusu wanyamapori waendelee kuzaliana na pia kwenda kupata
virutubisho maalum ambayo havipo mbugani.
'' Tunazihitaji hizi shoroba, tulikuwa tumejisahau shoroba nyingi
zimekuwa mashamba na makazi na wanyama wamekuwa hawana sehemu ya
kupita'' amesema Kanyasu
Amesema shoroba na maeneo ya mtawanyiko zisipokuwepo utalii na Hifadhi
vitatoweka.
" Lazima tufike mahali tuamue eneo hili ni kwa ajili ya kilimo na eneo
hili kwa ajili ya makazi, haiwezekani maeneo yote tukaanzisha kilimo
na makazi ilhali wanyamapori hawana mipaka" Alisisitiza Kanyasu .
Amesema uwepo wa shoroba na maeneo ya mtawanyiko husaidia kupata
kizazi imara cha wanyamapori kwani wakifungiwa sehemu moja huzaliana
ndugu na kukosa ubora,ikiwamo kuwa rahisi kushambuliwa na magonjwa.
Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewataka askari hao kufanya kazi
kwa uaminifu kwa kujiepusha kuungana na mtandao wa majangili.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Mhe. Sophia Mfaume
amewahakikishia askari hao kuwa wafanye kazi kwa kufuta sheria na wale
watakaowakwamisha katika kutekeleza majukumu yao hatasita
kuwachukulia sheria.
Aidha, Amewataka Wananchi wafuate sheria kwa kuheshimu maeneo ya
mtawanyiko na shoroba ili Hifadhi ziendelee kuwepo
Kwa upande wake, Mhitimu wa mafunzo hayo Musa Alfred Wakati akisoma
risala, Amemueleza Naibu Waziri kuwa mafunzo waliyopewa yatakuwa
chachu katika shughuli za uhifadhi nchini.
Naye Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Ruvuma, Jaqueline Msongozi
amewataka askari hao wa vijiji watekeleze majukumu yao bila kutishwa
na mtu yeyote kwa vile maliasili hizo ni za watanzania wote na wao
wanazilinda kwa niaba ya Watanzania.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu, akizungumza na wahitimu wakati akifunga mafunzo ya Askari 20 wa Wanyamapori wa Vijiji wa kutoka mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Singida waliohitimu mafunzo hayo katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu Sekamaganga kilichopo katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akizungmza na Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu Sekamaganga, Jane Nyau huku akiangalia mnara mpya uliowekwa na TTCL kwa ajili ya huduma za mtandao katika chuo hicho mara baada ya kuwasili kwa ajili ya kufunga mafunzo ya askari 20 wa wanyamapori wa vijiji katika wilya ya Namtumbo mkoani Ruvuma. Katikati ni Mkuu wa wilaya ya Namtumbo, Sophia Mfaume pamoja na viongozi wengine.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akikagua paredi kwa Askari 20 wa Wanyamapori wa Vijiji wa kutoka mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Singida wakati akifunga mafunzo kwa wahitimu wa mafunzo hayo katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii cha Likuyu Sekamaganga kilichopo katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Ruvuma
Baadhi ya Askari wa wanyamapori wa Jamii wakiwa wanamsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu wakati akizungumza nao katika mahafali ya kufuzu mafunzo yao katika Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili cha Likuyu Sekamaganga,
Mkuu wa chuo Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili cha Likuyu
Sekamaganga akizungumza wakati wa mahafali ya kufuzu kwa Askari
wanyamapori wa Jamii mkoani Ruvuma.
(PICHA ZOTE NA LUSUNGU HELELA-WMU)
No comments:
Post a Comment