Na John Nditi
UTAFITI wa Teknolojia ya Uhandisi Jeni ( GMO) katika Kituo cha
Utafiti wa Kilimo Makutupora na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania
(TARI ), Mikocheni unaendelea na utakapokamilika matokeo yake
yatawasilishwa serikalini kwa ajili ya kufanyiwa maamuzi ya kuitumia
au kitoitumia.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Tafiti za bioteknolojia za kilimo
nchini, Dkt. Fredy Tairo kutoka Taasisi ya Utafiti ya TARI Mikocheni
wakati akiwasilisha mada ya hali ya utafiti wa GMO nchini kwenye
mkutano wa mjadala wa wazi wa siasa za uchumi wa GMO nchini.
Mkutano wa mjadala huo uliofanyika Chuo Kikuu Dar es Salaam na
kuandaliwa na Idara ya Sayansi ya Siasa na utawala ya Chuo Kikuu
hicho.
Dk, Tairo alisema, msimamo wa Serikali ni kuendelea Utafiti wa GMOs
ili uweze kukamilika katika hatua zake muhimu na kisha utakapokamilika
katika hatua zote utapeleka katika Mamlaka husika kwa ajili ya kutoa
maamuzi hapa nchini.
Alisema, watu na baadhi ya vyombo vya habari walielewa vibaya kauli
iliyotolewa na serikali ilitaka watafiti wafuate utaratibu wa kutoa
matokeo waliyokuwa wanayapata kwenye majaribio hayo ili kuondoa
mkanganyiko.
Mratibu huyo wa Bioteknolojia katika mada yake alisema , sababu na
umuhimu wa serikali kufanya tafiti za GMO ili kukabiliana na
Changamoto sugu zinazotokana na madiliko ya tabia nchi ikiwemo ukame,
wadudu na magonjwa sugu ili kuongeza tija kwa wakulima.
Amesema, kuwa majaribio yanayofanyika katika taasisi ya utafiti ya
Makutupora Mkoani Dodoma unalenga kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya
ukame na bungua wa mahindi na kwa matokeo ya awali yameonyesha
kufanikiwa pia kupambana pia na Viwavi jeshi vamizi.
Kwa upande wa utafiti wa zao la Muhogo unaofanyika katika Taasisi ya
utafiti ya TARI Mikocheni alisema ,unalenga kuipa kinga mihogo
kupambana na magonjwa sugu ya Batobato kali na michirizi ya kahawia
ambayo yanaathiri zao hilo Afrika hasa kusini mwa Jangwa la Sahara.
Naye Mtafiti kutoka Chuo kikuu cha Sayansi na teknolojia cha Nelson
Mandela , Mashamba Philipo alisema , teknolojia hiyo ni nzuri na kwa
serikali,wakulima na Watafiti ni kuona kama ni muda muafaka wa
teknolojia hiyo kutumika hapa nchini.
Mtafiti huyo (plant breeder) alisema, teknolojia hiyo ina uwezo wa
kuwezesha nyanya kuwekewa jeni ambayo inauwezo wa kuifanya isiharibike
ndani ya mwezi mmoja hata baada ya kuichuma na hivyo kumuongezea tija
mkulima.
“Hii sio teknolojia ngeni duniani maana nchi za Marekani, China,
Brazil na nyingine nyingi za Afrika zinaitumia , lakini ni muhimu
wadau wote wapewe elimu ili kuondoa mashaka waliyonayo kuhusu
teknolojia hii” alisema Mtafiti Philipo.
Naye Mratibu wa tafiti za Bioteknolojia nchini, Dk Raphael Nduguru
alisema ,walizunguka nchini nzima na kukusanya mbegu za asili na
kuanzia utafiti na kuongeza jeni ili kuweza kukabilina na magonjwa
yanayohusiana na mihogo.
Naye Mtafiti Emmanuel Sulle ambaye ni Mwanafunzi wa Shahada ya
Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Western Cape Afrika Kusini alisema ,
kuna haja ya Serikali ya Tanzania kuongeza bajeti kwenye tafiti za
kilimo nchini ili kuwezesha watafiti wa ndani kupatafuta ufumbuzi wa
changamoto zinazowakabili wakulima.
Alisema , mbali na fedha lakini iongeze idadi ya watafiti kwenye
aina ya utafiti huo ambao unakuwa kwa kasi Duniani ili waweze kuwa na
uwezo wa kufanya tafiti hizo katika viwango vinavyotakiwa kimataifa.
Sulle alisema , licha ya kufanya tafiti za GMO lazima watafiti
waangalie na pia na mbinu zingine za asili wanazozitumia wakulima na
kuziboresha.
Mratibu wa Tafiti za Bioteknolojia katika kilimo kutoka TARI Mikocheni , Dk. Fredy Tairo akizungumza na na waandishi wa habari wakati wa mjadala wa wazi wa siasa za uchumi wa GMO nchini na kuandaliwa na Idara ya Sayansi ya Siasa na utawala ya chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Baadhi ya Washiriki kutoka idara, taasisi, mashirika na wadau wengine wa kilimo wakifuatilia mada wakati wa mjadala wa wazi wa siasa za uchumi wa GMO nchini na kuandaliwa na Idara ya Sayansi ya Siasa na utawala ya chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Mratibu wa Tafiti za Bioteknolojia katika kilimo kutoka TARI Mikocheni
, Dk. Fredy Tairo ( Kulia) , pamoja na Profesa Daudi Mukangara (
kati kati ) wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) ambaye alikuwa ni
Mwongoza mada pamoja na Mtafiti wa Chuo Kikuu cha Sayansi na
Teknolojia cha Nelson Mandela ,Mashamba Philipo ( kushoto)
wakisilikiza hoja mbalimbali ziliozolewa kwenye mjadala wa wazi wa
siasa za uchumi wa GMO nchini ulioandaliwa na Idara ya Sayansi ya
Siasa na utawala ya chuo kikuu cha Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment