HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 8, 2019

WAZIRI MKUU KUONGOZA MAZISHI YA DK. MENGI KESHO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa anatarajiwa kuongoza mazishi ya Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dkt. Reginald Mengi yatakayofanyika kesho Mei 9, 2019 kijijini kwake, Kisereni, Machame, wilayani Hai, Kilimanjaro.

Waziri Mkuu anatarajiwa kuongoza mazishi hayo kwa niaba ya Serikali. Ibada ya mazishi itafanyika kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) la Kisereni, Machame.

Mwili wa Dkt. Mengi ambaye alifariki dunia alfajiri ya Mei 2, mwaka huu akiwa kwenye matibabu huko Dubai, Falme za Kiarabu, umewasili Moshi leo ukitokea Dar es Salaam na kupokekelewa na mamia ya wananchi waliojipanga barabarani.

Jana, (Jumanne, Mei 6, 2019) Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wa Serikali, waliongoza maelfu ya wananchi kutoa heshima za mwisho wakati wa shughuli za kuaga mwili huo katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Hadi mauti yanamfika, Dkt. Mengi alikuwa Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo Vya Habari Tanzania (Chairman of the Media Owners Association of Tanzania - MOAT). Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (Tanzania Private Sector Foundation – TPSF).

Baadhi ya nyandhifa ambazo Dkt. Mengi aliwahi kushika ni pamoja na Kamishna wa kamati inayoshughulikia mishahara (Salary Review Commission); Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi Tanzania (NBAA); Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mazingira Tanzania (NEMC); Mwenyekiti wa vyombo vya habari vya Jumuia ya Madola Tanzania (Chairman of the Tanzania Chapter-Commonwealth Press Union-CPU); Kamishna wa TACAIDS na Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad