HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 13, 2019

TUHUMA ZA KUKUTWA NA GRAMU 232.70 ZA HEROINE ZAWAFIKISHA KORTNI SHAMIM NA MUMEWE

Na Karama Kenyunko, Michuzi TV

MMILIKI wa Blog ya 8020 Fashion, Shamim Omary Mwasha (41) na mume wake, Abdul Nsembo(45) wamefikishwa katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa wakikabiliwa na tuhuma za kusafrisha dawa za kulevya aina ya Heroine Hydrochloride zenye uzito wa gramu 232.70.

Akisoma hati ya mashtaka leo Mei 13, 2019  Wakili wa Serikali, Costastine Kakula amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi, Kelvin Mhina kuwa washtakiwa wametenda kosa hilo Mei 1,2019 wakiwa huko Mbezi beach, Wilaya ya Kinondoni, jijini  Dar es Salaam.

Imedaiwa kuwa siku ya tukio washtakiwa hao walikutwa na gramu 232.70. za Dawa za kulevya kinyume na sheria ya uhujumu uchumi. 
 Hata hivyo,  washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa  kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi  mpaka Mahakama Kuu ama kwa kupata Kibali kutoka kwa DPP.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Wakili wa utetezi, Hajra Mungula ameuomba upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi haraka ili hatua nyingine iweze kuendelea licha ya kwamba Leo  ndiyo siku ya kwanza kwa kesi hiyo kusomwa Mahakama hapo.

Kesi imeahirishwa hadi Mei 27, 2019 kwa kutajwa na kuangalia kama upelelezi umekamilika au la.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad