HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 30, 2019

NAIBU WAZIRI KANYASU-"SERIKALI HAINA MPANGO WA KUNYANG'ANYA ARDHII"

NA LUSUNGU HELELA-MARA
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewatoa hofu wananchi kufuatia zoezi linaloendelea la kupanga matumizi bora ya ardhi katika wilaya kumi nchini hasa katika maeneo yanayopakana na Hifadhi za Taifa kuwa zoezi hilo halina mpango wowote wa kunyang'anya ardhi ya wananchi kwa ajili ya kuanzisha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori.

Rai hiyo imetolewa leo na Mhe. Constantine Kanyasu kufuatia hofu kubwa iliyokuwa imetanda miongoni mwa wananchi wa vijiji 8 vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wilayani Bunda mkoani Mara ambapo moja ya madai yao ni kwamba zoezi hilo limelenga kuchukua maeneo yao ya malisho kwa ajili ya kuanzisha Hifadhi ya Jumuiya ya Wanyamapori jambo ambalo sio kweli.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Sarakwa kinachotenganishwa kati ya mto Rubana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti , Mhe.Kanyasu amewaeleza wakazi hao kuwa zoezi la kupanga matumizi bora ya ardhi katika maeneo hayo lina faida kubwa ikiwemo kuepusha migogoro wa ardhi inayotokea mara kwa mara miongoni mwao.

Amesema mpango wa matumizi bora ya ardhi ni zoezi la kitaifa ambalo limelenga kutenga maeneo maalum kwa ajili ya malisho, kilimo pamoja na shughuli za maendeleo kwa malengo yakuepusha migongano inayotokea sehemu mbalimbali nchini na si kunyang'anya ardhi mpya kama inavyodaiwa.

"Nataka niwahakikishie Wizara yangu haina mpango wa kuanzisha msitu wa Hifadhi wala Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori katika kijiji chenu, Huu ni uzushi upuuzeni" Alisisitiza Kanyasu.

Aidha, Mhe.Kanyasu amewaeleza wananchi hao kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi utasaidia kuepusha watu wachache kujimilikishia eneo kubwa,"kinachofanyika kwa sasa ni kuweka rekodi na nyaraka kwa ajili ya vizazi vyenu" Alisisitiza.

Amesema katika zoezi hilo la mpango wa matumizi bora ya ardhi wanachoweza kufanya ni kutenga eneo la msitu asili wa kijiji kwa ajili ya manufaa yao ikiwemo kuokota kumi na eneo litakuwa chini ya umiliki wa kijiji na sio serikali kuu.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewatoa wasiwasi wananchi hao kuwa licha ya kijiji hicho kuingia katika zoezi la mpango wa matumizi bora ya ardhi mifugo yao haitazuiliwa kwenda kunyweshwa maji katika mto Rubana.

"Nimesikia baadhi ya watu wakieneza uzushi kuwa baada ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kukamilika hakuna mtu yeyote kupeleka mifugo katika mto Rubana, huu ni uwongo" alisema Kanyasu

Hata hivyo amewaeleza kuwa mita 500 kutoka katika mto huo ni eneo la kijiji kwa ajili ya malisho ya mifugo isipokuwa vitu ambavyo havitaruhusiwa kufanywa na mtu yeyote ni kulima pamoja na kujenga nyumba kwa vile eneo hilo ni shirikishi kwa Wanyamapori pamoja na mifugo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bunda vijijini, Boniface Getere amewataka wananchi kuwa watulivu kwani serikali haina mpango wowote wa kunyang'anya ardhi badala yake mpango huo utakuwa mkombozi kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha badae.

" Mimi ni Mbunge wenu nisingeweza kukubali hata kidogo kama mpango huu wa matumizi bora ya ardhi umelenga kunyang'anya ardhi yenu." Alisisitiza Getere.

Naye, Mwenyekiti wa kijiji cha Sara, Samson Kapeta amekiri mbele ya Naibu Waziri kuwa mpango wa matumizi bora ni mpango mzuri isipokuwa kumejitokeza vikundi vya watu vilivyolenga kupotosha malengo mazuri ya serikali kwa ajili ya ardhi yao.

Mpango wa matumizi bora ya Ardhi ni mpango unaotekelezwa katika wilaya kumi nchini kwa ushirikiano katika ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi kwa kugharamiwa na Hifadhi ya Taifa ( TANAPA)
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sarakwa kuhusu umuhimu wa zoezi la mpango wa matumizi bora wa ardhi unaofanywa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Ardhi katika wilaya kumi katika wilaya kumi nchini kuwa haujikiti kupokonya maeneo mapya ya wananchi kwa ajili ya kuanzisha Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori kama inavyodaiwa.
 Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Sarakwa wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe, Constantine Kanyasu akiwaeleza kuwa serikali inaendesha zoezi la mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya manufaa ya wananchi.
 Mbunge wa Bunda vijijini, Mhe, Boniface Getere akizungumza na wananchi wa Sarakwa kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe, Constantine Kanyasu kuzungumza na wananchi hao kuhusu nia ya serikali ya kuendesha zoezi la mpango wa matumizi bora ya ardhi katika kijiji hicho.
Mratibu wa mipango wa matumizi bora ya ardhi, Rose Mdendemi akitoa ufafanuzi kwa wananchi wa kijiji cha Sarakwa wilayani Bunda mkoani Mara kuhusu zoezi linaloendelea la mpango wa matumizi bora ya ardhi (Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad