Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma amekishauri chama
cha wanasheria cha Tanganyika Law Society (TLS) kushirikiana na
Mahakama katika kutekeleza majukumu yake.
Akizungumza na Rais wa TLS pamoja na ujumbe wake walipomtembelea leo
ofisini kwake jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu amesema Mahakama pamoja
na chama hicho wanayo maeneo mengi ya kushirikiana pasipo kuingiliana
katika majukumu yao.
Aidha, Jaji Mkuu pia amekishauri chama hicho kuwa na mpango kazi wa
muda mrefu ili kuongeza ufanisi ndani ya chama hicho kwa kuwa kwa
mujibu wa Sheria, viongozi wa chama hicho hukaa madarakani kwa kipindi
cha mwaka moja kabla ya uchaguzi kufanyika tena.
Akizungumzia mapambano dhidi ya rushwa katika utoaji wa haki, Jaji
Mkuu amewataka Mawakili nao kupambana na rushwa kwa kushirikiana na
Mahakama ya Tanzania ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kufuata
maadili.
“Zifanyieni kazi changamoto za rushwa na shirikianeni na Mahakama ya
Tanzania kwa kuwa Mahakama ni mfumo wa kukosoana, alisema Jaji Mkuu.
Kwa upande wake, Rais wa TLS Mhe. Dkt. Rugemeleza Nshala ameiomba
Mahakama ya Tanzania kushughulikia changamoto mbalimbali wanazokutana
nazo Mawakili wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria Mahakamani
ikiwemo kuchelewa kuanza kwa kesi mahakamani.
Rais huyo pia aliishukuru Mahakama kwa ushirikiano inaoutoa kwa chama
chake na kuahidi kufanya kazi zake kwa kushirikiana na Mahakama ya
Tanzania.
Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezar
Feleshi amewapongeza viongozi wapya wa TLS waliochaguliwa hivi
karibuni na kuwashauri kufanya kazi kwa kushirikiana na Mahakama ya
Tanzania.
“Mifumo yetu iko wazi nasi tuko tayari kufanya kazi nanyi kwa kuwa
wote tunayo nia moja ya kumtumikia mwananchi”, alisema Jaji Kiongozi.
Wakati huo huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bwn. Hussein
Kattanga amewashauri viongozi wa TLS kushirikiana na Mahakama katika
kutatua changamoto mbalimbali za upatikanaji wa haki na kuwataka
kuwasilisha hoja na malalamiko kwa kuwa Mahakama kwa sasa inapokea
hoja, maoni na malalamiko ili kuboresha huduma zake.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma akizunzumza na viongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) walipomtembelea mapema Mei 16, 2019 ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia kwake ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, anaefuata ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga, kushoto kwake ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Dkt. Rugemeleza Nshala, anaefuata ni Makamu wa Rais wa Chama hicho Bw. Mpale Mpoki , pamoja na wajumbe wengine walioshiriki katika mazungumzo hayo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. ibrahim Hamis Juma akisisitiza jambo wakati akizungumza na ujumbe kutoka Chama cha Wnasheria Tanganyika, ukiongozwa na Rais wa chama hicho, Dkt. Rugemeleza Nshala.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika
picha ya pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS) Dkt.
Rugemeleza Nshala (kushoto kwa Jaji Mkuu) pamoja na wajumbe wengine.
No comments:
Post a Comment