HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 22, 2019

HALMASHAURI ZA MKOA WA RUVUMA ZATAKIWA KUDHIBITI BIDHAA ZA CHAKULA, VIPODOZI NA DAWA ZISIZO NA UBORA NA USALAMA

Waganga wakuu wa halmashauri katika mkoa wa Ruvuma wameagizwa kusimamia kwa karibu  ubora na usalama wa chakula,dawa na vipodozi uliokasimiwa kwao  na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini(TFDA).
Agizo hili limetolewa jana mjini Songea na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Edmund Siame wakati alipofungua kikao kazi kati ya watendaji wa TFDA na halmashauri nane za Ruvuma

Siame amesema kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Chakula na Dawa Kanda ya Kusini imeonyesha halmashauri za Ruvuma zimeshindwa kutekeleza kwa ufanisi usimamizi wa majukumu yaliokasimiwa kwao kwa mujibu wa makubaliano kati ya Wizara ya Afya na TAMISEMI
Sheria ya Chakula ,Dawa na Vipodozi  Sura 209 na kanuni zake za mwaka 2015 ilikasimu baadhi ya majukumu kwa halmashauri  nchini kote ili kudhibiti bidhaa zisizo na ubora na salama.

Amezitaja changamoto zilizokwamisha utekelezaji wa majukumu ya TFDA kuwa ni kushindwa kutenga bajeti ya fedha zinazotokana na makusanyo ya ada na tozo za vibali vya TFDA ili ziweze kutumika katika udhibiti wa bidhaa na kufanya ukaguzi.
“Ni kosa kwa halmashauri kushindwa  kufanya vikao vya robo mwaka vya kamati za chakula na dawa kwani kunasababisha bidhaa zisizo na ubora na usalama kuingia mitaani na kuweza kusababisha madhara kwa wananchi” alisema Siame

Halmashauri hizo pia zimeshindwa kuwasilisha taarifa za za utendaji kazi kwa kila robo mwaka kama ambavyo imeelekezwa kwenye kanuni
Siame ameagiza waganga wakuu wa halmashauri za Ruvuma kuanzia sasa kurekebisha mara moja upungufu na kuhakikisha lengo la TFDA na serikali kulinda afya ya jamii linatimizwa .
Kaimu Katibu Tawala huyo wa Mkoa ametaka kuwepo ushirikiano wa karibu kati ya TFDA na wilaya ili kuepusha madhara kwa walaji na kuepusha uchumi wa nchi kushuka.

“Bidhaa za chakula,dawa,vipodozi na vifaa tiba visipodhibitiwa ipasavyo zinaweza kusababisha madhara ya vifo na kudhoofisha uchumi wa nchi yetu”alisisitiza Siame
Kwa upande wake Meneja wa TFDA kanda ya Kusini, Juma Bukuku amezishauri halmashauri za mkoa wa Ruvuma kuacha kutoza ada na tozo kwa maeneo ambayo hayakukasimiwa kwao mfano maduka ya vipodozi na maduka ya dawa ya jumla.

Akizunguzia tatizo la bajeti Mganga Mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru Dkt .Wendy Robert amesema tatizo la ukosefu wa bajeti  lilisababisha washindwe kufanya ufuatiliaji wa shughuli za udhibiti na ubora wa chakula na dawa kwenye baadhi ya maeneo pembezoni.
Naye Dkt.Aron Hyera kutoka halmashauri ya wilaya ya Nyasa ameshukuru kwa TFDA kuratibu kikao kazi hiki kwani kimesaidia kuweka uwelewa na mipaka ya utendaji kazi kati ya TFDA na halmashauri kwenye usimamizi wa majukumu.

Mwisho.
Imetolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Ruvuma

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad