HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 6, 2019

DKT. NDUGULILE ATOA RAI KWA VIONGOZI WA KISIASA KUTOINGILIA KAZI ZA TAALUMA YA AFYA

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile ametoa rai kwa viongozi wa Kisiasa hapa nchini kuacha kuingilia kazi za Kitaaluma katika sekta ya Afya na kuwaomba wawaache wataalam wafanye kazi zao kwa misingi na miiko ya Kitaaluma inayowaongoza.

Dkt. Ndugulile ameyasema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, chini ya Kauli Mbiu “Wakunga Watetezi wa Haki za Wanawake”, ambapo alikuwa akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Amesema hivi karibuni kumekuwa na matamko yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa yanayowakatisha tamaa watumishi wa sekta ya afya na baadhi ya viongozi wameanza kuingilia masuala ya kitaalum, hivyo akawaomba ikiwa viongozi hao watakutana na changamoto za watendaji wa afya waishirikishe wizara ya afya ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa taaluma zao.

“Niwaombe sana viongozi wa Serikali na Viongozi wa vyama, masuala ya kitaaluma yanashughulikiwa kitaaluma kama kuna changamoto na wanataaluma ndiyo maana tuna mabaraza ya taaluma na ndiyo maana sisi wizara tupo mtushirikishe, nimelisema hili kwa sababu nimeona sekta imeanza kuingiliwa” alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha, Dkt. Faustine Ndugulile amewataka wakunga hapa nchini kuendelea kuzingatia miiko na misingi ya taaluma yao katika huduma wanazotoa kwa jamii na kuahidi kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaokiuka misingi hiyo kwa kuwa jamii inahitaji heshimu, utu, upendo na kutiwa moyo

Katika hatua nyingine Dkt. Ndugulile ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo na jamii kwa ujumla kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za afya ili changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi vibaki kuwa historia ambapo amesema kwa sasa wanawake 11,000 wanakufa kila mwaka kutokana na uzazi.

Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania, Bibi. Feddy Mwanga ameiomba Serikali kuongeza idadi ya wakunga ili mkunga aweze kutoa huduma kwa kiwango kinachokubalika Kitaifa na kimataifa huku akisisitiza Serikali kuona haja ya kujenga nyumba za wakunga katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinavyoboreshwa na vinavyojengwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthoy Mtaka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa shilingi bilioni saba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali tatu za Wilaya Bariadi, Busega na Itilima ambazo ujenzi wake unaendelea vizuri.

Aidha, Kiswaga ameshukuru Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani(UNPFA) kwa namna linavyoshirikiana na Serikali mkoani Smiyu kwa kukarabati baadhi ya vituo, kununuaa vifaa mbalimmbali, kutoa mafunzo kwa wakunga jitihada ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Akitoa taarifa ya Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema Idadi ya wakunga katika vituo vya kutolea huduma za afya Simiyu imeongezeka hali iliyofanya wajawazito wengi kujifungulia katika vituo vya afya kutoka asilimia 62 mpaka asilimia 68, hivyo vifo vya mama wajawazito vimepungua kutoka vifo 48 mwaka 2017 mpaka vifo 40 mwaka 2018.

Naye Makamu Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA hapa nchini, Dkt.Hashina Begum amesema kwa kushirikiana na Chama cha Wakunga nchini (TAMA) limetoa mafunzo kwa wakunga 90 kutoka katika vituo vilivyoboreshwa ili kuwasaidia wakina mama wajawazito na watoto kupata huduma za dharura na kupunguza vifo kwa mama na mtoto vitokanavyo na uzazi.

Grace Magengeni Mkunga kutoka Jijini Dodoma amesema” siku yetu imefana tunashukuru hotuba ya Naibu Waziri imetutia moyo katika kuwahudumia wanawake na watoto, nawashauri wenzangu tusimamie taaluma zetu tufanye kazi kwa bidii naamini hao wanaotuingilia majukumu yetu wataachaa maana ni kweli, tunashukuru Naibu Waziri kulisemea hili suala”
 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (kulia ) akipokea maelezo kutoka kwa mmoja wa wakunga ya namna wanavyowahudumia wakina mama wajawazito na watoto wakati alipotembelea Banda la Chama cha Wakunga Tanzania(TAMA), katika Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo yamefanyika Kitaifa katika Uwanja wa Bariadi Mkoani Simiyu.
 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (kulia ) akiangalia baadhi ya vitabu vinvyotuika kutoa elimu kwa wananchi wakati alipotembelea banda la maonesho la Shirika lisio la kiserikali la AGPAHI, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo yamefanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
 Baadhi ya wakunga wakiwa katika maandamano wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo yamefanyika Kitaifa Mei 05, 2019 katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akimkabidhi mmoja wa kunga wa moa wa Simiyu cheti kama zawadi ya kufanyakazi nzuri, katika Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo yamefanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad