HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 17, 2019

SERIKALI YASHUSHA GHARAMA ZA URASIMISHAJI

Na Munir Shemweta, WANNM

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema kuanzia sasa gharama za urasimishaji haitazidi shilingi 150,000 badala ya 250,000 iliyopangwa awali na makampuni yatakayoenda kinyume yatachukuliwa hatua ikiwemo kufutwa.

Lukuvi alitoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokutana na Makampuni ya Upangaji na Upimaji yanayofanya kazi ya urasimishaji katika mitaa mbalimbali nchini pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, baada ya Wizara yake kuona zoezi la urasimishaji linasuasua wamegundua asilimia 30 pekee ndiyo iliyorasimishwa tangu kuanza zoezi hilo na hali hiyo imechangiwa na uwezo mdogo wa wananchi wengi kumudu gharama za urasimishaji.

Waziri Lukuvi alisema, alichotegemea kwa makampuni yaliyopewa kazi ya urasimishaji ni kuwa na uzalendo kwa kushusha gharama lakini yameshindwa kupunguza gharama jambo lililoifanya serikali kuona haja ya kupitia upya gharama hizo na kubaini gharama za msingi ili kumuwezesha mwananchi kupata hati na kusisitiza punguzo hilo halitawahusu waliolipia gharama za urasimishaji.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameyataka makampuni yanaoyoendesha zoezi la urasimishaji kuhakikisha kiasi cha fedha inachowatoza wananchi kinaishia hatua ya Hati na gharama itakayolipwa na mwananchi baada ya kurasimishwa ni kodi ya ardhi na kuyatahadharisha kutochukua muda mrefu kukamilisha zoezi hilo.

Amewataka wananchi wote wanaoishi kwenye maeneo yasiyo rasmi kuhakikisha wanaingia katika zoezi la urasimishaji ili kupata hati itakayowawezesha kiuchumi na kusisitiza kuwa suala hilo linafanyika kwa nia njema kwa nia ya kuwaongezea mtaji wananchi kwa kupatiwa nyaraka itakayowasiadia kukopa fedha benki.

Akigeukia suala la Leseni za Makazi, Waziri Lukuvi alisema zoezi hilo linaendelea vizuri katika jiji la dar es Salaama kwa gharama ya shilingi elfu tano hadi hatua ya upatiwaji leseni ya makazi na kusisitiza kuwa leseni hiyo siyo ya kudumu bali itakuwa kwa miaka mitano na kuwataka wananchi walio katika maeneo ya urasimishaji kuendelea na zoezi hilo kwa kuwa wizara inayo kanzi data itakayotunza takwimu za mazoezi yote mawili.

‘’Tunataka kuwa na database ya nani anamiliki ardhi kiasi gani na kila mwananchi lazima awe na leseni ya makazi au hati kwa lengo la kushiriki kulipa kodi’’ alisema Lukuvi

Hata hivyo, Lukuvi alisikitishwa na baadhi ya Makampuni ya urasimishaji kushindwa kutoa takwimu wakati wa zoezi la upimaji zinazoendana na miongozo ya wizara na kuyataka yote yaliyoenda kinyume kurudia zoezi na kuongeza kuwa kuna makampuni 34 yaliyotuma takwimu ambazo ni chafu na kuyapongeza makampuni mawili ya Visible Planners na Afro Max kwa kufuata taratibu zote za urasimishaji.

Lukuvi alionya baadhi ya makapuni ya urasimishaji kuacha kuwalaghai wananchi kwa kuwapatia leseni za makazi badala ya hati kwa gharama za urasimishaji na kusema kufanya hivyo ni kosa la uhujumu uchumi na hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Vile vile Lukuvi amewataka watendaji wa serikali ambao wana makampuni yanayofanya kazi ya urasimishaji kuchagua jambo moja la kuitumikia serikali ama makampuni yao kwa kuwa wanatumia muda mwingi kufanya kazi katika makampuni yao badala ya kuitumikia serikali.

‘’Ninyi watendaji wa serikali badhi yenu mna makampuni ya urasimishaji na ndiyo mnaoharibu zoezi mnataka squatters ziendelee ili mnufaike na mnapima halafu michoro mnapitisha ninyi hii ni conflict of interest’’ alisema Likuvi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad