HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 23 April 2019

RC MAKONDA ARIDHISHWA NA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA ILALA

* Asisitiza wazawa kupewa vipaumbele katika utekelezaji wa miradi mikubwa
*Atoa fursa kwa vijana wajasiriamali, neema yanukia

Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Ilala mradi ambao unatekelezwa na fedha takribani shilingi bilioni 1 na milioni 500 zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli katika kuboresha sekta ya afya nchini.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya kukagua miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo ni soko la kisasa la ghorofa tatu la Kisutu ambalo litakamilika ndani ya miezi 18 (Septemba 9, 2020) kituo cha afya Buguruni na barabara Makonda amesema kuwa kasi ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Ilala yenye majengo saba inayojengwa Kivule jijini humo inaridhisha na baada ya kukamilika kwake itawasaidia wananchi wengi wa maeneo hayo pamoja na kupunguza msongamano katika hospitali ya rufani ya Amana huku mkuu wa Wilaya hiyo Sophia Mjema amehaidi hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu mradi huo utakuwa umekamilika.

Makonda amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano ipo makini katika kuhakikisha wananchi wa chini wanapata huduma muhimu bila kizifuata kama ilivyokuwa awali na amehaidi barabara korofi ya eneo hilo zitashughulikiwa mapema iwezekanavyo.

Aidha amesema kuwa wataalamu wanaosimamia miradi hiyo watoe nafasi kwa wazawa ili nao waweze kunufaika kwa kuwa Mkoa huo una zaidi ya miradi ya shilingi trilioni 3 hivyo ni vyema wazawa wakanufaika.

Akiwa Lumumba Kariakoo Makonda amekutana na vijana wa fani mbalimbali na kuahidi kuwa Serikali itatoa mafunzo bila malipo ya ufundi kupitia VETA kwa vijana wengi kwa fani za ufundi gereji, umeme na vyuma ili kuwajengea uwezo na kuwapa fursa zaidi.

Kwa upande Mkuu wa Wilaya hiyo Sophia Mjema amewataka wananchi kuunga mkono jitihada za serikali katika kuleta maendeleo na wao kama wawakilishi watasimama imara ili huduma muhimu ziweze kuwafikia kwa urahisi.

Ziara hiyo ni mwendelezo wa ukaguzi wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa jijini humo na katika Manispaa ya Ilala amekagua ujenzi wa soko la kisasa la Kisutu, ujenzi wa barabara kata ya Kilawani, Hospitali ya Wilaya ya Ilala iliyopo Kivule pamoja na ukaguzi wa majengo mapya katika kituo cha afya Buguruni.
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda  akikagua ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Ilala ambayo inajengwa kwa fedha (bilioni moja na milioni 500) zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli katika kuboresha huduma za afya leo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akiwa ameambatana na  viongozi wa Wilaya hiyo wakati wa kukagua mradi wa ujenzi wa barabara hiyo na amewataka kufanya kazi kwa kasi zaidi na kumaliza miradi hiyo kwa wakati, leo jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akitoa maelekezo kwa viongozi wa Wilaya hiyo mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara hiyo na amewataka kufanya kazi kwa kasi zaidi na kumaliza miradi hiyo kwa wakati, leo jijini Dar es Salaam.
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akizungumza na vijana wajasiriamali katika mtaa wa Swahili Kariakoo jijini Dar es Salaam ambapo amewahaidi kutolewa bure kwa mafunzo ya ufundi ili kuwajengea fursa na uwezo zaidi leo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad