HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 9, 2019

Balozi Seif atembelea shule ya Sekondari Kinyasini

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi msaada wa Laptop Mbili kwa ajili ya matumizi ya kimasomo Kwa Walimu na Wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Kinyasini iliyopo Wilaya ya Kaskazini “A” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Huo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati alipofanya ziara kipindi cha nyuma ya kukagua na kuangalia maendeleo na changamoto zinazoikabili skuli hiyo na kuzungumza na Uongozi wa Kamati ya Skuli, walimu, Wazazi na Wanafunzi wa Skuli hiyo.

Akipokea Msaada huo uliowasilishwa na Msaidizi wa Makamu wa Pili wa Rais anayesimamia masuala ya Ustawi Bibi Siti Abass, Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Kinyasini Mwalimu Kombo Ali Machano alisema msaada huo umeleta ukombozi kubwa kwao na watalazimika kuutunza ili uweze kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu.

Hata hivyo Mwalimu kombo aliomba iwapo utakuwepo uwezekano wa kupatiwa Printa itakuwa ni jambo la faraja litakalowawezesha kuweputa matatizo yanayojitokeza wakati wanapoamua kwenda ku\ichapisha kumbukumbu zao kwenye Kompyuta za nje.

Akielezea furaha yake Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Skuli ya Kinyasini Bwana Is-haka Vuai Kidawa alisema Uongozi wa Skuli hiyo, Wazazi na Wanafunzi bado wanaamini kwamba Kiongozi huyo kamwe hatosita kuendelea kusaidia nguvu za kuimarisha Elimu Skulini hapo.

Bwana Is-haka alisema Wananchi wa Kijiji hicho na vitongoji vyake wanaelewa kwamba Kiongozi huyo wa Juu Serikalini akiwa ndie Mtendaji Mkuu wa Serikali amekuwa akikabiliwa na ahadi nyingi na ukweli usiopingika kwamba inakuwa vigumu kuzitekeleza kwa wakati jambo ambalo wao walilazimika kufanya subra kutokana na ahadi yao hiyo.

Wakati wa ziara yake Skulini hapo Miaka michache iliyopita Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Wazazi wana wajibu na ulazima wa kuhakikisha kwamba watoto wao wanawasimamia vyema katika kupata elimu bora itakayotoa mwanga wa kimaisha katika hatma yao ya baadaye.

Balozi Seif alisema elimu ndio ufunguo pekee pekee utakaowapa njia watoto hao kukabiliana na mazingira ya kimaisha yanayokwenda kwa kasi na haraka ndani ya mfumo wa sasa wa sayansi na Teknolojia.

Katika kuipa sifa Skuli hiyo kongwe ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja Balozi Seif aliwahimiza Wafaunzi wa Skuli hiyo kuwa na dhamira ya kutafuta elimu kwa gharama yoyote ile.

Alisema wanafunzi lazima wawe na nia ya kutafuta elimu hasa ile ya sayansi ambayo bado ina mapungufu katika taasisi za kijamii kwani kuamua kusoma ni wajibu kwao ili kufanikiwa kimaisha.

Alifahamisha kwamba masomo ya sayansi yanayoonekana kupigwa chenga na wanafunzi walio wengi maskulini ndio yanayotoa fursa kubwa ya ajira katika ulimwengu huu wa sasa wa Sayansi na Teknolojia Ulimwenguni.

Skuli ya Kinyasini ikiwa ni miongoni mwa skuli kongwe ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja iliasisiwa mnamo mwaka 1946 kwa Darasa la Quran na kuanza kwa darasa la kwanza mwaka 1947 lililoendelea hadi darasa la kumi na moja Mwaka 1973 na sasa limefikia darasa na Kumi na Mbili.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na Walimu pamoja na Uongozi wa Kamati ya Skuli ya Sekondari Kinyasini alipofanya ziara fupi skulini hapo Miaka michache iliyopita na kuahidi kusaidia Kompyuta.
 Balozi Seif akiangalia mabadiliko makubwa ya majengo ndani ya Skuli ya Sekondari ya Kinyasini ambapo ndipo alipoanzia kupata elimu ya msingi katika miaka ya 46.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizunguma na wazazi, kamati ya skuli, walimu na wanafunzi wa skuli ya Sekondari ya Kinyasini kipindi alipofika kuona maendeleo na changamoto zinazoikabili Skuli hiyo. Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad