HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 18, 2019

WAZIRI MHAGAMA AFUNGUA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI OFISI YA WAZIRI MKUU.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amefungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi yake upande wa Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu uliofanyika mapema mwishoni mwa wiki hii.

Akifungua mkutano huo uliofanyiaka Machi 16, 2019 katika Ukumbi wa mikutano wa Magadu mkoani Morogoro waziri aliwataka watumishi wa ofisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na ubunifu ili kuendelea kuleta tija na utendaji wenye kuleta maendeleo nchini.

“Naamini mkutano huu unalenga kugusa maeneo yote ya utendaji kazi ikiwemo kubainisha changamoto, fursa na jinsi ya kujipanga ili kuongeza tija na ufanisi katika maeneo yetu ya kazi,”alisema Mhagama

Waziri aliwaeleza watumishi kuutumia mkutano huo kama chombo muhimu cha kuendelea kujadili na kuweka maazimio yanayotekelezeka kwa kuzingatia umuhimu wa chombo hicho kilichopo kisheria katika kusaidia watumishi wa umma.

“Tumieni mabaraza haya kama eneo muhimu la kujadili na kutoa mapendekezo juu ya kuboresha mazingira ya kazi ili kuendelea kuwa na weledi katika kutekeleza majukumu ya ujenzi wa Taifa,”alieleza Mhagama

Waziri aliongezea kuwa, matumizi sahihi ya mkutano huo ni kuona namna  utavyosaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili Idara, Vitengo pamoja na Taasisi zilizopo chini ya Ofisi hiyo na kuwa na  maoni, ushauri na mapendekezo yanayotekelezeka ili kufikia malengo waliojiwekea kwa mwaka wa fedha ujao 2019/2020

Pamoja na hayo Waziri alipongeza utendaji wa watumishi wa ofisi yake hususan Idara ya Kazi, inayoshughulikia masuala ya vibali vya kazi na kuendelea  kuboresha mifumo na mazingira wezeshi ili kuendelea ,kulinda mazingira ya kazi na ajira nchini.

“Pamoja na idara zote kuendelea kufanya vyema, kipekee naipongeza Idara ya kazi kwa mabadiliko mapya ya kiutendaji kwa kuzingatia ilikuwa Idara inayotupa shida hususani upande wa vibali vya ajira, tunashukuru kwa mageuzi makubwa yaliyofanyika katika Idara hiyo kwa kuwa na usimamizi mzuri na kulinda mazingira ya ajira na kuleta manufaa nchini,”alieleza Mhagama

Sambamba na hilo waziri aliwapongeza watendaji wa Ofisi kwa ujumla kwa nafasi zao kwa kuwepo na mafanikio makubwa ya kiutendaji pamoja na mchango wa kila mtumishi katika utoaji wa huduma bora bila upendeleo kwa wananchi wote kwa haki na usawa.

“Sina budi kuwapongeza kwani kila mmoja wetu ametimiza majukumu na kuwa na mchango mkubwa katika kutimiza majukumu ya serikali yetu kwa kuendelea  kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020,”alisisitiza Waziri Mhagama.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ofisi hiyo Bw. Andrew Massawe aliahidi kuendelea kusimamia maagizo na ushauri wa waziri kwa watumishi wa ofisi yake ili kuleta matokeo chanya yanayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika kuboresha mazingira ya utendaji kwa watumishi ikiwemo kuendelea kupambana na rushwa mahali pa kazi na kuzingatia haki na usawa kwa watumishi wote.

Aidha Katibu Mkuu aliongezea kuwa, uwepo wa mabaraza hayo ni kwa mujibu wa sheria na  agizo Na. 1 la mwaka 1970 ambalo linaelekeza utaratibu wa kuundwa kwa mabaraza katika Taasisi na Ofisi za Umma kwa kuzingatia sheria mbalimbali za Kimataifa ikiwemo zile za Shirika la Kazi Dunia (ILO)

“Kwa kuzingatia lengo la kuanzishwa kwa mabaraza haya ni pamoja na kuona utekelezaji wa Bajeti za Ofisi zetu pamoja na kutoa mapendekezo katika kuboresha utekelezaji wa bajeti zetu za kila mwaka,”alisisitiza Massawe

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe.Jenista Mhagama akihutubia watumishi wa Ofisi yake wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika Machi 16, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Magadu Mkoani Morogoro.
 Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Bw.Andrew Massawe akizungumza jambo wakati wa mkutano wa baraza la wafanyakazi wa ofisi yake Machi 16, 2019


  Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) wakifuatilia mkuatano huo.
 Mkurugenzi wa ajira Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Ally Msaki akichangia jambo wakati wa mkutano huo.
 Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Mipango Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Bw. Godfrey Chambo akichangia jambo wakati wa mkuatano huo.
 Mkurugenzi wa Sera na Mipango Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Bw. Gabriel Saelie akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/2019 pamoja na Mada ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2019/ 2020 wakati wa mkutano huo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa ofisi yake mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo, uliofanyika Mkoani Morogoro.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad