HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 13, 2019

WAZIRI KAIRUKI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA UINGEREZA NCHINI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe.Angellah Kairuki amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke mapema hii leo Machi 13, 2019 katika ofisi zake Jijini Dodoma.

Lengo la mazungumzo hayo ilikuwa ni kujadili maeneo muhimu yanayohusu masuala  ya uwekezaji ambapo Waziri Kairuki alieleza vipaumbele muhimu vya uwekezaji  vitakavyochangia adhma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda ikiwemo kuwekeza katika maeneo ya kilimo, elimu, afya, viwanda vya nguo pamoja na ujenzi wa Miundombinu ya barabara.

“Ninafarijika kwa ujio wako na ni ishara nzuri ya mahusiano mazuri yaliyopo  baina ya nchi hizi mbili naamini yatasaidia katika fursa za uwekezaji hasa kwa namna Uingereza ilivyochangia katika maeneo muhimu nchini ikiwemo elimu,”alisema Kairuki

Waziri aliongezea kuwa, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwa kuzingatia mchango unaotokana  na wawekezaji hasa katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo nchini.

Waziri Kairuki alieleza kuwa, kuwepo kwa Idara ya uwekezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu ni hatua muhimu kwani itasaidia kuongeza nguvu ya ufuatiliaji na utekelezaji wa masuala hayo na kuendelea kuleta mabadiliko katika kutatua changamoto zilizozikabili sekta hiyo.

Aidha alimshukuru balozi huyo kwa hatua ya mazungumzo yenye tija pamoja na kuendelea kuunga mkono nchi ya Tanzania na kuwataka kuendeleza urafiki huo kwa kuwekeza zaidi katika maeneo aliyoyaainisha ikiweko yale ya vipaumbele.

Naye Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania, Sarah Cooke aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa na sera zinazovutia wawekezaji pamoja na maboresho yanayofanywa kuwavutia wawekezaji nchini ikiwemo maeneo ya ulipaji wa kodi.

“Tunaelewa kuwa Serikali inafanya jitihada kubwa katika kuboresha mazingira ya biashara ikiwa ni pamoja na mazingira ya ulipaji wa kodi tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuwa na mchango katika maendeleo ya nchi pamoja na kuimarisha mahusiano yaliyopo,”alisisitiza Cooke.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki akisalimiana na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke, ofisini kwake Jijini Dodoma Machi 13, 2019 alipokutana naye na kufanya mazungumzo.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki akizungumza na balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke pamoja na wenyeji alioambatana nao wakati wa kikao cha mazungumzo  na Waziri Kairuki kuhusu masuala ya fursa za uwekezaji nchini.
 Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke akizungumza jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki alipomtembelea Ofisini kwake Machi 13, 2019 Jijini Dodoma.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki akizungumza jambo na balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke wakati wa kikao hicho.
 Mwakilishi wa masuala ya Biashara Afrika Bw.Martin Kent akizungumza jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki (Hayupo pichani) wakati walipomtembelea katika Ofisi zake Dodoma.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki akiteta jambo na balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke mara baada ya kumaliza mazungumza yao, kulia ni Beth Arthy aliyeambatana na balozi huyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke (wa pili kutoka kushoto) pamoja na wajumbe alioongozana nao.

(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad