HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 6 March 2019

WANAWAKE WAFANYAKAZI WAKUTANA DODOMA KUJADILI CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI DUNIA IKIHADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Tanzania inaungana na Nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku Wanawake Duniani kwa lengo la kutafakari mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto lakini pia kuwakomboa kifikra, kiutamaduni, kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongomano la wanawake wafanyakazi kuhadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike alisema wanawake na wasichana wafanyakazi ni kundi kubwa na muhimu katika jamii linalohitaji kulindwa.

Bw. Golwike alitoa Rai kwa wanawake hao kuwa Haki inakwenda pamoja na Uwajibikaji lakini pia Usawa unakwenda pamoja na kukidhi vigezo, ambavyo ni sifa za kielimu, kitaaluma na uzoefu wa kazi.

Ameongeza kuwa Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani hufanyika kila mwaka ifikapo Machi 8, kwa mwaka huu hapa Tanzania yanafanyika ngazi ya Mkoa, ambapo kila Mkoa umeadhimisha sikukuu hii kulingana na mazingira yake na rasilimali zilizopo kwa kuzingatia Kaulimbiu ya mwaka husika ambayo ni “Badili fikra kufikia usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu”.

Aidha Bw. Golwike aliyataja Madhumuni ya Maadhimisho haya kuwa ni kutoa fursa kwa Serikali, Wananchi, Wadau, Wanawake na Jamii yote kubadili fikra na mtizamo ili kuleta Usawa wa Jinsia na kuonesha nia ya kuhamasisha jamii, juu ya umuhimu wa kutambua uwezo wa wanawake katika kuchangia na kuleta Maendeleo Endelevu lakini pia  Kuwezesha ushiriki na kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanawake kufikia maendeleo jumuishi.

Wakati huo huo Msimamizi wa Maadhimisho hayo kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bi. Silivia Siriwa alitaja mafanikio yaliyopatikana kutokana na juhudi za Wizara kuwa  ni pamoja kutoa elimu kwa jamii kuhusu utatuzi wa changamoto zinazowakabili wanawake ikiwemo Madhara ya Mila na Desturi potofu ambazo zinaelekeza aina ya kazi na nafasi za uongozi za kushikwa na wanawake ambazo ni za kutoa huduma zaidi.

Aliyataja mengineyo ni kuhamasisha jamii kuhusu kuondoa madhara ya ndoa na mimba za utotoni, ambazo zinafifisha ndoto na matarajio ya mtoto wa kike, hamasa na ushiriki  wa wafanyakazi katika  majukwaa ya uwezeshaji wanawake ambayo yanatumika kwa ajili ya kuelimishana, kubadilishana uzoefu na kujiunga katika mtandao wa mashirikiano.

Bi. Siriwa pia alizitaja baadhi ya changamoto zinazojitokeza kwa wanawake mahali pa kazi ni pamoja na kukosa taarifa za mabadiliko ya Sheria na Kanuni za utumishi, Matumizi ya lugha ya kiingereza katika matumizi ya vifungu vya kisheria inawanyima baadhi ya wafanyakazi, haki ya kuzifahamu sheria.

Aidha Wingi wa shughuli na majukumu ya kifamilia, kikazi na kijamii ni hali inayopunguza ufanisi wao, kipato kidogo cha kumudu mahitaji ya familia na ongezeko la wahitaji kutoka katika makundi maalum ya jamii ambayo wanawake wafanyakazi wanayabeba.

Chimbuko la Siku ya Wanawake lilianza mwanzoni mwa miaka ya 1900 kufuatia maandamano ya wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda nchini Marekani kupinga mazingira duni ya kazi.

Waandamaji hao, walilalamikia ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira ikiwemo wanawake kulipwa mshahara mdogo kwa kazi sawa na wanaume.
 Mwakilishi wa Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike akifungua Kongamano la wafanyakazi Wanawake jiijini Dodoma liliofanyika kwa lengo la kuwakutanisha wafanyakazi hao kujadiliana na kupata namna bora za kuweza kumuwezesha kiuchumi  mwanamke.
 Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Silvia Siriwa akieleza chimbuko la Siku ya Wanawake Duniani katika Kongamano la wafanyakazi Wanawake jiijini Dodoma liliofanyika kwa lengo la kuwakutanisha wafanyakazi hao kujadiliana na kupata namna bora za kuweza kumuwezesha kiuchumi mwanamke.
  Mkurugenzi Msaidizi Wanawake kutoka  Idara ya Jinsia Bi. Mboni Mgaza akielezea umuhimu wa Siku ya Wanawake Duniani katika  kiuchumi mwanamke katika kongamano la wafanyakazi wanawake Dodoma.  
 Baadhi ya Wafanyakazi Wanawake wa Mkoa wa Dodoma wakifuatlia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa katika Kongamano la wafanyakazi Wanawake jiijini Dodoma liliofanyika kwa lengo la kuwakutanisha wafanyakazi hao kujadiliana na kupata namna bora za kuweza kumuwezesha kiuchumi mwanamke.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wanawake waliohudhuria Kongamano la wafanyakazi Wanawake jiijini Dodoma liliofantika kwa lengo la kuwakutanisha wafanyakazi hao kujadiliana na kupata namna bora za kuweza kumuwezesha kiuchumi mwanamke.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad