HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, March 2, 2019

Uzalishaji Sekta ya Kilimo na Ufugaji Kuongezeka Chamwino

Frank  Mvungi - MAELEZO, Dodoma
Urasimishaji ardhi Wilayani Chamwino mkoani Dodoma umetajwa kuwa kichocheo cha kukuza uzalishaji katika sekta ya kilimo na ufugaji baada ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wakulima wilayani humo.
Akizungumza katika mahojiano maalum Meneja Urasimishaji Ardhi Vijijini kutoka Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Bw. Antony Temu amesema kuwa wakulima wamejengewa uwezo kupitia mafunzo yaliyoratibiwa na mpango huo baada ya urasimishaji wa mashamba ya wakulima hao.
“ Wakulima hawa wataweza kuzalisha kwa tija na kuongeza uzalishaji kutoka magunia 4 kwa sasa hadi kufikia magunia 10 kwa ekari moja na pia wataweza kutekeleza dhana ya ufugaji bora wa kuku na mifugo mingine ili kuendana na fursa zilizopo kutokana na Serikali kuhamia Dodoma,”alisisitiza Temu.
Akifafanua, Bw. Temu amesema kuwa wakulima zaidi ya 100 wamenufaika na mafunzo ya kuwajengea uwezo ambapo wakulima kutoka kijiji  cha Membe wameonesha mwitikio mkubwa katika mafunzo hayo hali inayoonesha kuwa mafunzo yataleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa wakulima wilayani humo.
Aliongeza kuwa wakulima hao sasa wametambua mbegu bora za mazao wanayozalisha ikiwemo alizeti hali itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wao baadhi ya wakulima wa kijiji cha Membe akiwemo Bi. Pelestatili Msilili amesema kuwa urasimishaji ardhi utawasidia kutatua changamoto zilizopo katika uzalishaji kwenye sekta ya kilimo na hivyo kujikwamua kiuchumi.
“Tutaweza kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha hivyo tunawashukuru MKURABITA kwa kuja na mpango huu wa kutujengea uwezo ambao ni ukombozi wa kweli,”alisisitiza  Bi Msilili
Naye Bi Suzana Kuanikwa ambaye ni mkazi wa kijiji cha Membe amebainisha kuwa anaishukuru Serikali kwa namna inavyowajali wananchi wake kupia uwezesjhaji  huu unaotuwezesha kuwa na matumizi bora ya ardhi katika kijiji chetu.
Aidha, Bi Kuanikwa amebainisha kuwa kwa sasa wakulima wa kijiji hicho watapata mwamko mpya katika uzalishaji kwenye sekta ya kilimo na mifugo.
MKURABITA imekuwa  ikiendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wakulima baada ya kurasimisha mashamba yao katika halmashauri mbalimbali hapa nchini, kwa ujumla halmashauri 24 zimeshafikiwa na Mpango wa Urasimishaji wa Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania.
 Meneja Urasimishaji Ardhi Vijijini wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Bw. Antony Temu akisisitiza kuhusu  faida watakazopata wananchi baada ya za kutumia fursa zinazotokana na mafunzo ya kuwajengea uwezo wakulima wa kijijin cha Membe wilayani Chamwino hivyo  kuchangia katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi hao .
Sehemu ya wakulima zaidi ya 100 wa Kijiji cha Membe Wilayani Chamwino wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoratibiwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA).
(Picha zote na Frank  Mvungi- MAELEZO, Dodoma)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad