HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 11 March 2019

TUNDURU WAANZA MKAKATI WA KUMALIZA UGONJWA WA TB

HOSPITALI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,imeanza zoezi la upimaji wa viashiria vya ugonjwa wa kifua kikuu(TB) kwa wanafunzi wa Bweni katika shule za Sekondari  kama mkakati wa kumaliza na kuzuia maambukizi kwa ugonjwa huo hasa katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi.

Katika zoezi hilo, Hospitali kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma,inawashirikisha baadhi ya waganga wa jadi na tiba asilia pamoja na watu waliougua kifua kikuu na kupoma kukusanya makohozi kutoka kwa watu na kupeleka hospitalini kwa ajili ya vipimo.

Mratibu wa Kifua kikuu wa Hospitali ya wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema, zoezi la kukusanya makohozi kwa wanafunzi wa shule za sekondari hasa zile za Bweni ni mpango wa Serikali kwa kushirikiana na mfadhili MDH na GLOBAL FUND ambao unakusudia kumaliza ugonjwa huo unaotajwa kuwa ni kati ya magonjwa yanayoongoza kuuwa watu wengi hapa nchini.

Alisema, katika zoezi hilo kwa kuwatumia waganga wa jadi na tiba asili ambao wanakusanya makohozi hasa katika maeneo ya vijijini na kupeleka Hospitali kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kupunguza ukubwa wa tatizo na kuokoa Maisha ya wananchi ambaao wanaumwa Tb ambapo wale wanaogundulika kupata ugonjwa huo wanaanzishiwa dawa mara moja.

Alisema, kuanzia mwezi Januari hadi Februari mwaka huu tayari wamefanikiwa kutembelea shule nne za sekondari ambazo ni Tunduru Sekondari,Muhesi,Ligoma na Nandembo ambapo wale waliobainika kuwa na viashiria vya ugonjwa huo wanashauriwa kuanza dawa.

Dkt Kihongole alisema, wameamua kufanya zoezi la upimaji wa Tb kwa wanafunzi wa shule za Bweni kwa kuwa ni rahisi sana kuambukizana kutokana na kukaa pamoja  kwa muda mrefu.

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Nandembo Salma Ali na Gramaki Abdala , wameishukuru Hospitali ya wilaya ya Tunduru kwa kuendesha zoezi hilo ambalo litasaidia sana kupunguza uwezekano wa kuambukizana TB n ahata wale waliopata kuanza Dawa.

Salma Ali alisema,elimu inayotolewa inayokwenda sambamba na zoezi la upimaji wa kifua kikuu kwa  wanafunzi wa shule za Bweni  ni muhimu kutokana na muingiliano uliopo na kushauri elimu  na upimaji ufanyike kila mwezi au kila mwanzo wa muhula hasa pale shule zinapofunguiwa kwani kuna wanafunzi ambao wanatoka moja kwa moja nyumbani ambao wanakwenda kuishi na wenzao bwenini.

Mmoja wa wahamishaji na mkusanyaji makohozi katika Kijiji cha Nandembo Joseph Hyera alitaja dalili za ugonjwa huo ni kutokwa na jasho,kupungua uzito na kutokwa na Damu wakati wa kukojoa.

Alisema, ili kuzuia kuenea na kuambukizwa ni vema kuepuka msongamano,kutotema mate ovyo, kuishi kwenye mazingira safi, na kupata chanjo maalum kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Alisema, dalili za TB kwa kawaida zinaanza kujitokeza kuanzia siku 30 hadi 90 kutegemea na kinga ya mwili ya Binadamu, hata hivyo njia pekee ni watu kwenda kupima Afya zao mara kwa mara na kumaliza dozi wanazopewa badala ya kuamini ugonjwa huo na Imani za kishirikina.

Hyera alisema, madhara ya ugonjwa huo ni makubwa kuliko ukimwi kwani  ni ugonjwa ambao unaambukiza kirahisi sana watu na yule asiyetumia dawa anaweza kupoteza Maisha katika kpindi cha miaka miwili.
 Mmoja wa wahamishaji makohozi wanaofanya kazi ya kukusanya makohozi kwa ajili ya vipimo vya ugonjwa wa kifua kikuu wilaya ya Tunduru akiongea na wanafunzi wa shule ya sekondari Nandembo kabla ya zoezi la upimaji wa ugonjwa wa kifua kikuu kwa wanafunzi wa shule hiyo.
 Mhamishaji makohozi kutoka katika kijiji cha Nandembo Joseph Hyera akitoa elimu ya madhara ya ugonjwa wa kifua kikuu  kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Nandembo jana.
 Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Nandembo wakijaza fomu kabla ya kuanza kwa zoezi la upimaji makohozi ili kubaini waliopata ugonjwa wa Kifua Kikuu na kuanza kupatiwa Dawa zoezi linalofanywa na Idara ya kifua kikuu na ukoma katika Hospitali ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad