HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 22 March 2019

TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUWEKA MAZINGIRA RAFIKI YATAKAYOWEZESHA UTEKELEZAJI WA UJUMUISHWAJI WA MASUALA YA KIJINSIA SEHEMU ZA KAZI

Taasisi za umma nchini zimetakiwa kuweka mazingira rafiki sehemu za kazi ili kuwezesha utekelezaji wa masuala ya kijinsia kwa ufanisi na hatimaye kufikia usawa wa kijinsia  utakaokuwa na tija kwa maendeleo ya Taifa.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Leila Mavika wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili cha ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia mahali pa kazi kilichofanyika mjini Morogoro kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji kazi katika taasisi za umma.
Leila amesema kuwa, mazingira rafiki ya ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi yanategemea  menejimenti za taasisi za umma kutoa kipaumbele kwa masuala ya anuai za jamii kuwa ni sehemu ya shughuli za uendeshaji wa ofisi za kila siku.

Leila ameainisha kuwa, ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia utafanikiwa iwapo kutakuwa na uelewa wa pamoja wa masuala ya kijinsia kwa watumishi wa umma na menejimenti zao ambao utasaidia kuepuka ubaguzi na unyanyapaa mahala pa kazi na kuongeza kuwa,  taasisi za umma zikijenga majengo jumuishi yenye miundombinu inayofikika kwa urahisi na wadau wote hususan watu wenye ulemavu wa viungo, zitawezesha jinsia zote kupata huduma bora bila kikwazo cha aina yoyote. 

“Ni vema taasisi zikaweka mifumo thabiti itakayoweka mazingira rafiki, wezeshi na mifumo rejeshi inayotoa fursa kwa wananchi kutoa taarifa za masuala ya  unyanyasaji wa kijinsia  na ukiukwaji wa maadili kwa ujumla” amesema Bi. Leila.

Leila amezitaka taasisi zote za umma kuhakikisha kwamba, zinatenga bajeti kwa ajili ya  ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi na kuyafanya masuala ya kijinsia kuwa ajenda ya kudumu katika vikao  vya kitaasisi vya ndani na nje.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Hamidi Mbegu amesema kuwa, kikao kazi hicho cha ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi kitakuwa ni chachu ya kuboresha utekelezaji wa masuala ya kijinsia katika wizara yake na taasisi zote za umma.
Aidha, Bw. Mbegu amesema, kikao hicho kimeazimia kuwepo mwongozo rasmi utakaowezesha utekelezaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi, ambao utasaidia uanzishaji wa madawati ya kijinsia sehemu za kazi ambayo yatarahisisha   utekelezaji na ufuatiliaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi.

Naye, Mshauri wa Masuala ya Jinsia wa Mradi wa SAUTI kutoka Shirika la Jhpiego, 
 Grace Munisi amesema kuwa, serikali imekuwa ikishirikiana na mradi huo katika utekelezaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi kupitia udhamini wa warsha mbalimbali zinazosaidia kuwapa uelewa watendaji juu ya mahusiano ya kijinsia yanavyoweza kusababisha  maambukizi ya virusi vya UKIMWI na kuepuka mila potofu zinazosababisha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI sehemu za kazi na kwenye jamii kwa ujumla.

Kikao kazi cha siku mbili kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi katika Taasisi za Umma kilijumuisha Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi kutoka katika Wizara, kwa lengo la kujadili fursa na changamoto za masuala ya kijinsia katika utumishi wa umma ili kuweka mikakati endelevu itakayofanikisha uwepo wa Usawa wa Jinsia mahala pa kazi  utakaowezesha maendeleo endelevu.
 Mkurugenzi Msaidizi, Idara wa Utawala, Mahakama ya Tanzania, Wanyenda Kutta akitoa mada kuhusu uzoefu wa taasisi yake katika masuala ya kijinsia kwenye kikao cha ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Leila Mavika akifunga kikao kazi cha siku mbili kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
 Baadhi ya washiriki wa kikao kazi kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi kutoka katika Wizara na Taasisi za serikali wakifuatilia mada wakati wa kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
 Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Christina Mangwai akichangia mada wakati wa kikao kazi kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
 Baadhi ya washiriki wa kikao kazi kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi kutoka katika Wizara na Taasisi za serikali wakijadiliana maazimio wakati wa kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
 Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, BLeila Mavika akitoa maelekezo kuhusu maazimio wakati wa kikao kazi cha siku mbili kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad