HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 7 March 2019

SERIKALI YAAGIZA KUHAMISHWA KWA DAMPO LA KIHESA KILOLO

Na Lulu Mussa, Iringa
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima ameagiza kuhamishwa kwa dampo la Kihesa Kilolo lililopo katika Kata ya Kihesa Manispaa ya Iringa kutokana na kuwepo katika mazingira yasiyo rasmi. 
Agizo hilo limetolewa hii leo Mkoani Iringa mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kukagua namna bora ya kuteketeza taka bila kuathiri mazingira  na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Iringa Bw. Richard Kasesela kusimamia maelekezo hayo mapema iwezekanavyo ikiwa ni pamoja na kuteketeza taka zilizozagaa katika eneo hilo na kuweka katazo la watu kuingia katika dampo kwa lengo la kuokota chupa za plastiki kwa ajili ya kuziuza. 
Akiwa katika eneo hilo la dampo la Kihesa Kilolo Naibu Waziri Sima ameshuhudia maji machafu yakitiririka kutoka katika dampo hilo na kwenda kwenye makazi ya watu jambo ambalo linahatarisha afya za wakazi wa maeneo ya jirani pamoja na tishio la mlipuko wa magonjwa.
Akitoa msimamo wa Serikali Naibu Waziri Mussa Sima ameagiza kwa hatua za haraka kuwekwa utaratibu wa  kudhibiti maji yanayotiririka kutoka katika dampo kwa kujenga mifereji ili kunusuru ikolojia ya vyanzo vya maji katika maeneo hayo.
“Ndugu zangu hali ni mbaya sana katika dampo hili, simamieni uteketezaji wa taka mapema iwezekanavyo, Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya namna hii, wananchi wanalipia gharama za ubebaji wa taka, zinaletwa dampo kisha mnaruhusu tena wananchi kuingia dampo, kwa maana nyingine tunakusanya taka katika mitaa na kuzirudisha tena katika mitaa, hii haikubakiki ” Sima alisisitiza.
Naibu Waziri Sima pia ameagiza eneo lililotengwa na Manispaa kwa matumizi ya dampo lililopo katika Kijiji cha Mkoga, Kata ya Isakalilo lenye ukubwa wa ekari Ishirini na tano kufanyiwa Tathmini ya Athari kwa mazingira kabla ya kuanza kutumiwa, sambamba na kulipa fidia wakazi wa maeneo hayo
Wakati huo huo, Naibu Waziri Sima pia amemuagiza Mratibu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kanda za Nyanda za juu kusini Bw. Godlove Mwamsojo kuhakikisha anafuatilia utekelezaji wa agizo hilo na endapo Halmashauri haitatekeleza kwa kipindi walichokubaliana hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao . 
Nae Mkuu wa Idara ya Udhibiti wa Mazingira ya Uteketezaji wa taka gumu Bw. Christian Ndenga amekiri kuwa kwa takribani mwezi mmoja taka katika dampo hilo hazijateketezwa kutokana na sababu za kuharibika kwa ‘kijiko – Wheel loader’.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Bw. Richard Kasesela amesema kuwa takriban tani 108 huzalishwa kwa siku katika Manispaa ya Iringa, na kuahidi kusimamia zoezi la kuteketeza taka zilizopo na kuhamisha dampo ndani ya wiki mbili ikiwa ni utekelezaji wa maagizo.
Naibu Waziri Mussa Sima yuko katika ziara ya kikazi ya kukagua maeneo yenye changamoto za kimazingira hususan katika sekta ya afya na udhibiti wa taka ngumu pamoja ikolojia ya vyanzo vya maji vinavyo changia maji katika bonde la Rufiji.
 Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima (katikati) akiongea na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Bw. Richard Kasesela (Kulia) na Bi. Ritha Kabati Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Iringa mara baada ya kutembelea dampo la Kihesa Kilolo lilipo katika Kata ya Kihesa Manispaa ya Iringa
Sehemu ya dampo la Kihesa Kilolo kama linavyoonekana pichani, taka hazijateketezwa kwa kipindi kirefu na halina uzio wowote. Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mussa Sima ametoa muda wa wiki mbili kuhakikisha eneo lote linasafishwa ili kuepuka mlipuko wa magonjwa na kulinda ikolojia ya vyanzo vya maji.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad