HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 13 March 2019

NAIBU WAZIRI MABULA AHIMIZA UPIMAJI VIJIJI KUONDOA MIGOGORO YA ARDHI

Na Munir Shemweta, KATORO
Serikali imehimiza  halmashauri nchini kupima maeneo ya vijiji ili kuwamilikisha wananchi ardhi kwa nia ya kuwapatia hati za kimila na wakati huo kupanga matumizi bora ya ardhi katika maeneo hayo kwa lengo la kuepuka migogoro ya ardhi na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa jana tarehe 12 Februari 2019 na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa kutoa hati 21 kwa wananchi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Katoro uliopo wilaya ya Geita mkoa wa Geita pamoja na kutoa Ramani za Urasimishaji kwenye wilaya za Chato na Geita wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.

Alisema suala  la kupima vijiji ni la lazima na halmashauri zinapaswa kuchukua  hatua za kuwapimia wananchi kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi lakini pia kuleta salama ya miliki ya maeneo yao kwa kuwa kutofanya hivyo kutasababisha kuwepo migogoro ya mipaka pamoja na kiwanja kimoja kumilikishwa kwa watu wawili    (double allocation).

Akigeukia suala la urasimishaji, Dkt Mabula alizitaka halmashauri za wilaya ya Geita kuhakikisha zinarasimisha maeneo yaliyojengwa kiholela na kusisistiza kuwa salama ya eneo la mtu haliishii kuwekewa vigingi bali kinachotakiwa ni mtu kumilikishwa ili aweze kuitumia ardhi hiyo kujiinua kiuchumi kwa kuwa anaweza kuitumia hati yake kwa ajili ya kukopea fedha benki,

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  alikabidhi ramani za urasimishaji kwa wakurugenzi wa halmashauri  mbili za wilaya ya Geita pamoja na ile ya Chato kwa nia ya kuendesha zoezi la urasimishaji katika maeneo ya halmashauri hizo.

Sambamba na hilo Dkt Mabula alishuhudia utiaji saini  makubailiano ya kupatiwa kiasi cha shilingi milioni 180 kwa halmashauri ya wilaya ya Geita kwa ajili ya kutwaa maeneo mapya ya halmashauri hiyo ambapo alieleza kiasi hicho cha fedha kitumike  kuepuka kero wakati wa kutwaa maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  fedha zilizosainiwa ni kama mkopo na halmashauri husika inatakiwa kuuza viwanja na kurejesha fedha hizo ndani ya miezi mitatu na kubainisha kuwa Wizara imetengewa  shilingi bilioni 7 kwa ajili ya kuzikopesha halmashauri mbalimbali nchini ili kutwaa maeneo.

Alisisitiza kuwa ni marufuku kuchukua eneo la mtu bila kulipa fidia na kubainisha kuwa sheria ya mwaka 2016 inaweka wazi kuwa ukitwaa eneo ndani ya miaka miwili kama hujalipa fidia basi mwenye eneo anaruhusiwa kubaki na eneo lake na kiasi cha riba kinaongezeka kila baada ya miezi sita.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Ally Kidwaka alisema pamoja na Halmashauri yake kuwa na miji midogo yenye wakazi 50,000 lakini Mji Mdogo wa Katoro ndiyo unaokuwa kwa kasi na sasa umefikia wakazi wapatao laki moja. Alisema kutokana na mji huo kukuwa kwa kasi wataalamu wa upimaji wanatakiwa kuongezwa katika mji huo ili kuepuka changamoto za urasimishaji maeneo ya mji huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halamashauri ya Wilaya ya Geita Elisha Lupuga alisema Mji wa Katoro pamoja na kukuwa kwa kasi kwa muda mrefu lakini  ulichelewa kupatiwa mamlaka ya Mji  jambo lililochelewesha maendeleo katika mji huo. Hata hivyo, alisema  pamoja na wananchi wa Mji wa Katoro kuwa na uwezo wa fedha na nyumba nzuri lakini wamekuwa wazito kutoa fedha kwa ajili ya kupimiwa maeneo yao jambo linalosababisha mji kutopangika vizuri.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro katika mkoa wa Geita wakati wa kutoa hati za ardhi kwa wananchi wa mji huo kwenye ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Kulia kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhandisi Ntemi Musafiri na kushoto ni Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Geita Ally Kidwaka.
 Mkuu wa wilaya ya Chato Mhandisi Ntemi Musafiri akizungumza wakati wa zoezi la kutoa hati za ardhi kwa wananchi wa Mji Mdogo wa Katoro mkoani Geita uliofanywa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati akihamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Makwasa Biswalo.
 Baadhi ya wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro mkoani Geita wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati akihamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoa wa Geita Eliurd Mwaiteleke alipomkabidhi ramani kwa ajili ya zoezi la urasimishaji katika halmashauri hiyo wakati Naibu Waziri akiwa katika ziara  ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi hati ya ardhi mmoja wa wakazi katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro mkoani Geita Dohoi Shimiyu wakati alipotoa hati 21 kwa wakazi wa Mji huo akiwa katika kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro mkoani Geita waliopatiwa hati za ardhi wakati Naibu Waziri akiwa katika ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Wa tatu kushoto aliyekaa ni Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhandisi Ntemi Musafiri na wa tatu Kulia aliyekaa ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Geita Elisha Lupuga
 Mkuu wa idara ya Ardhi na Maliasili katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoa wa Geita Deogratias Matiya akimuonesha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula eneo la uwekezaji la Lubambagwe (Chato Beach) wakati Naibu waziri akiwa katika ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi mkoani Geita, Kulia ni Meneja wa Shirika la Nyumba mkoa wa Kagera Benit Masika.
 Mkuu wa wilaya ya Chato Mhandisi Ntemi Musafiri  akimuonesha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula eneo lililopangwa kwa ajili ya makazi katika uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita wakati Naibu waziri alipotembelea eneo hilo  kwa nia ya kuhamasisha mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuzuia ujenzi holela eneo linalozunguka uwanja huo.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad