HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, March 16, 2019

MAKAMU WA RAIS AONGOZA KONGAMANO LA KUIMPONGEZA RAIS SHEIN

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na wanawake kwa ujumla kuchapa kazi zaidi na kushikamana katika kuleta maendeleo kwa jamii nzima.

Makamu wa Rais ameyasema hayo kwenye Kongamano la Wanawake la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  kwa kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi lililofanyika kwenye hoteli ya Verde, wilaya ya Magharibi A, mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

“Sisi ni sehemu muhimu sana ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, hivyo Kongamano hili liwe chachu yetu katika kuchapa kazi zaidi”alisema Makamu wa Rais.

Aidha, aliwasihi wanawake kuchukua jukumu la kuzisemea na kuzitangaza kwa sauti kubwa kazi nzuri zinazofanywa na viongozi  wa Serikali zetu mbili ili wananchi wazijue na wasipotoshwe.

“Sote ni mashuhuda wa kazi kubwa na nzuri iliyofanyika hapa Zanzibar kwa kipindi cha miaka mitatu. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Uongozi mahiri wa Dokta Shein imefanya kila liwezekanalo kuboresha hali ya maisha ya wananchi wa Zanzibar kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi.”Alisisitiza Makamu wa Rais.

 Rais Shein ametekeleza kwa umahiri mkubwa ilani ya Uchaguzi na kuweza kuleta mafanikio makubwa katika Uimarishaji wa Huduma za afya, Elimu , ujenzi wa miundombinu,Kilimo, ufugaji, uvuvi na Ushirika, kuwawezesha Wazee, wanawake na Walemavu na kuwateua wanawake kwenye nafasi za Uongozi.

Makamu wa Rais ameupongeza uongozi wa UWT Taifa pamoja na Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar kwa kuandaa kongamano hilo ambalo sit u la kumpongeza Dkt. Shein kwa kazi kubwa aliyofanya kwa kipindi cha miaka mitatu, bali Kongamano la kutoa ushuhuda kwa wananchi kuhusu kazi nzuri inayofanywa na Chama Cha Mapinduzi katika kusimamia maendeleo ya wananchi.

Mawaziri wa SMZ , Wawakilishi wa Viongozi na Naibu Waziri wa Nishati kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano walipata nafasi ya kuelezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika Kongamano hilo.

Kongamano hili lilifanyika Pemba tarehe 9, Machi 2019 ambapo lilitanguliwa na ziara liyoanza tarehe 6-8 mwezi Machi 2019 na ziara kama hiyo imefanyika Unguja kuanzia tarehe 11-14 Machi 2019 ambapo tarehe 15 Kamati ya Utekelezaji ya UWT Taifa ilikutana.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye Kongamano la UWT la kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi lililofanyika kwenye hotel ya Verde. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Mwenyekiti wa UWT Taifa Gaudensia Kabaka akihutubia kwenye Kongamano la UWT la kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi lililofanyika kwenye hotel ya Verde. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais) 
Sehemu ya Waliohudhuria Kongamano la UWT la kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi lililofanyika kwenye hotel ya Verde. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad