HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 20, 2019

DKT. MWANJELWA AWATAKA WAAJIRI SERIKALINI KUZINGATIA UBUNIFU KATIKA UJUMUISHWAJI WA MASUALA YA KIJINSIA SEHEMU ZA KAZI ILI KULETA TIJA KIUTENDAJI

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amewataka waajiri serikalini kuzingatia kigezo cha ubunifu wanapotekeleza zoezi la ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi ili kuleta matokeo chanya na yenye tija katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa (Mb) amesema hayo mapema leo, alipokuwa akifungua kikao kazi cha siku mbili kinachohusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia mahala pa kazi kilichofanyika mjini Morogoro.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, endapo waajiri watazingatia kigezo cha ubunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea serikali itapata watendaji kazi bora watakaoleta matokeo chanya katika maendeleo ya nchi kwani watafanya kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa (Mb) ameongeza kuwa, ubunifu katika utendaji kazi utawezesha watumishi kuondokana na mitazamo hasi juu ya dhana ya jinsia ya kike kutegemea kupata kazi kutokana na jinsi yao badala yake watambue kuwa vigezo na sifa za kiushindani ndiyo vinazingatiwa. 
“Tunapodai haki zetu kama wanawake tuwe na hoja zenye mashiko zitakazoendana na sifa na vigezo husika, tusiseme kuwa sisi ni wanawake hivyo tupewe nafasi” amesema Dkt. Mwanjelwa.
Dkt. Mwanjelwa amewataka waajiri kuzingatia vigezo vya ubunifu wanapoajiri wanawake na kutenga bajeti kwa ajili ya ujumuishwaji wa masuala ya jinsia mahala pa kazi ili kuboresha  utendaji kazi. 
Aidha, Dkt. Mwanjelwa amewaagiza watendaji katika Idara za Utawala na Rasilimaliwatu kuwa kioo katika utekelezaji wa masuala ya kijinsia mahala pa kazi ili kuepuka vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, rushwa ya ngono, ubaguzi wa aina yoyote, upendeleo, ubadhilifu wa mali za umma na uvujishaji wa siri za serikali.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais , Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Agnes Meena amesema kuwa, ofisi yake kama mratibu wa masuala ya anuai za jamii imeona umuhimu wa kuandaa kikao cha ujumuishaji wa masuala ya kijinsia sehemu za kazi kwa kushirikiana na wakurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi Rasilimaliwatu kwa kuwa wao ndio wahusika katika usimamizi wa mipango ya rasilimaliwatu na masuala yote ya kiutumishi.
Bi. Meena amesema kuwa, kikao hicho kimefanyika kutokana na kuwapo kwa mwitikio wa wastani katika utekelezaji wa masuala ya jinsia sehemu za kazi unaosababishwa na kukosekana kwa utayari wa taasisi , mipango katika taasisi, mitazamo hasi, unyanyapaa na ufinyu wa bajeji.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao hicho, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala, Mahakama ya Tanzania, Bi. Wanyenda Kutta amekiri kuwapo kwa changamoto katika utekelezaji wa masuala ya kijinsia mahali pa kazi na kuahidi kuwa kikao hicho kitatoa maazimio yatakayoiwezesha serikali kutekeleza masuala ya kijinsia ipasavyo mahali pa kazi.
Lengo la kikao hicho ni kujadili fursa za masuala ya kijinsia katika utumishi wa umma na kuweka mikakati itakayofanikisha Usawa wa Jinsia kwa Maendeleo Endelevu.
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akifungua kikao kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia mahali pa kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
 Mkurugenzi Msaidizi Idara wa Utawala, Mahakama ya Tanzania, Bi. Wanyenda Kutta akitoa neno la shukrani katika kikao kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia mahali pa kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
 Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora , Bi. Agnes Meena akimkaribisha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb)  (hayupo pichani) kufungua kikao kuhusu Ujumuishwaji wa masuala ya ya kijinsia mahali pa kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Anuai za Jamii, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ,Bi. Leila Mavika akiwasilisha mada katika kikao cha ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia mahali pa kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
 Baadhi ya washiriki wa kikao kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya Kijinsia mahali pa kazi kutoka katika Wizara na Taasisi za serikali wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) wakati akifungua kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao kuhusu ujumuishwaji wa masuala ya kijinsia mahali pa kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Glonency Hotel, mjini Morogoro.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad