HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 12 February 2019

WAZIRI KAIRUKI, TIC WAWAHAKIKISHIWA WAWEKEZAJI KUTOKA HONG KONG KUWA TANZANIA NI SEHEMU SALAMA YA KUWEKEZA

Na Said Mwishehe, Blogu ya Jamii
KITUO cha Uwekezaji Tanzania(TIC)kimepokea ujumbe wa watu saba kutoka Hong Kong -China ambao lengo lake ni kufanya mazungumzo na taasisi mbalimbali za Serikali na kufanya tafiti kabla ya kuwekeza ikiwemo kwenye eneo la la ujenzi wa viwanda vya vifaa tiba na dawa. Akizungumza mbele ya wajumbe hao leo Februari 12, 2019 ,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji Angellah Kairuki amesema ujumbe huo umekuja nchini kwa lengo la kufanya tafiti katika maeno mbalimbali ya uwekezaji ambapo tangu wamefika nchini wamekuwa wakifanya mazungumzo na taasisi za Serikali wakiongozwa na TIC.

"Ujumbe huo kutoka Hong Kong ambayo ni sehemu ya China upo nchini kwa ajili ya kufanya mazungumzo na taasisi mbalimbali za Serikali.Pia wamekuja kufanya tafiti na lengo lao kubwa ni kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya dawa na vifaa tiba, viwanda vya magodoro pamoja na viwanda vingine kadhaa kulingana na tafiti yao.

 "Pia wameonesha nia ya kuwekeza katika kununua ufuta yakiwamo majani yake hasa kwa kuzingatia ufuta katika nchi hiyo unatumika katika kusaidia pia kutibu magonjwa mbalimbali na hivyo kiu yao ni kuona wanawasaidia wakulima wa zao hili nchini Tanzania kuzalisha ufuta kwa wingi.Pia ni fursa ya kupata soko la uhakika kwani wakulima wetu sasa watakuwa na uhakika wa kuuza majani ya ufuta pamoja na ufuta wenyewe,"amesema Waziri Kairuki.

Ameongeza pia ujumbe huo baada ya kufika nchini wamefanya mazungumzo na Bohari ya Dawa nchini(MSD) hasa kwa kuzingatia wanalo eneo la hekari 150 ambalo wanatafuta watu wa kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya dawa na vifaa tiba.Pia wamezungumza na uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kuangalia ni namna gani wawakezaji kutoka Hong Kong wanaweza kuwekeza nchini Tanzania kwa lengo la kuboresha sekta ya afya.

Waziri Kairuki ameongeza kuwa ujumbe wa watu hao saba , wameonesha nia pia ya kujenga viwanda vya kuchakata korosho na kwamba kupitia mazungumzo kati ya ujumbe huo na taasisi za Serikali kuna muelekezo mzuri Hong Kong ambayo imekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania kuwekeza zaidi nchini.Pia amewahakikishia kuwa Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dk.John Magufuli imeendelea kuweke mazingira mazuri ya uwekezaji na kwamba ni sehemu salama.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Geofrey Mwambe amesema uhusiano baina ya Hong Kong na Tanzania umezidi kuimarika katika kufungua fursa za uwekezaji na utalii na kwamba kihistoria inafahamika Hong Kong ilikuwa ni nchi inayojitegemea lakini baadae ikawa sehemu ya China.
 Amesema kutokana na Hong Kong kuwa sehemu ya China , taarifa nyingi za uwekezaji ambazo zilikuwa zinatoka Tanzania Hong Kong zilikuwa zinarekodiwa China, hivyo Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kufanya jitihada ikiwa pamoja na kufungua Ofisi ya Ubalozi Mdogo ambao kazi yake ni kuimarisha uhusiano wa kibishara na utalii.

Amesema kuwa Ofisi hizo za Ubalozi Mdogo Hong Kong zinasimamiwa na Balozi Mdogo Dk.Anne Wu ambaye tangu awali alionesha nia ya dhati ya kuisaidia Tanzania katika kukuza uhusiano kati yao na Tanzania, hivyo ujumbe wa ujumbe wa watu saba ni sehemu ya kuimarika kwa uhusiano uliopo. "Tangu kuwepo kwa Ubalozi Mdogo wa Hong Kong hata idadi ya wanaomba kuja nchini kwetu imeongeza mara tatu zaidi ya awali.Hata hivyo tunatarajia fursa za kiuwekezaji na kiutalii kunufaisha sehemu zote mbili.

Watanzania watumie fursa ya kufanyabiashara Hong Kong na hivyo hivyo Hong Kong nayo itumie fursa hiyo kuwekeza nchini Tanzania.Tumeendelea kuwahamasisha Hong Kong kuja nchini kutalii kutokana na vituo vilivyopo hapa kwetu na kweli wameongeza,"amesema Mwambe na kusisitiza kuwa Tanzania inayo mazingira mazuri ya uwekezaji.

Wakati huo huo Kiongozi wa msafara wa ujumbe huo ambaye pia ni Mwakilishi wa Balozi Mdogo Hong Kong Dk.Annie Wu, Jessica So amesema ujio wao nchini Tanzania umekuwa na manufaa makubwa kwani kuna maeneo mengi ambayo yanafaa kwa uwekezaji na hivyo kupitia utafiti ambao wameufanya kwa kuzungumza na taasisi za umma kuna maeneo ambayo wameonesha nia ya kuwekeza.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji Angellah Kairuki akizungumza leo jijini Dar es Salaam kuhusu ujio wa ujumbe wa watu saba kutoka Hong Kong ambao wapo nchini kuangalia fursa za uwekezaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania Geofrey Mwambe (aliyesimama) akifafanua jambo leo jijini Dar es Salaam kuhusu ujumbe wa watu saba kutoka Hong Kong ambao wako nchini kuangalia fursa za uwekezaji ukiwemo uwekezaji wa ujenzi wa viwanda vya dawa na vifaa tiba.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad