HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 7, 2019

WASHTAKIWA SABA WA KESI YA BOMBA LA MAFUTA WAFUTIWA KESI NA KUACHIWA HURU

Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru, washtakiwa saba kati ya 12 waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kujiunganishia isivyo halali bomba la mafuta, mali ya Mamlaka ya Bandari Tanzania ( TPA).

Washtakiwa hao wameachiwa huru leo Februari 7.2019 baada ya upande wa mashtaka kuomba kuliondoa shtaka hilo. Mapema,  wakili wa Serikali mwandamizi , Patrick Mwita aliieleza mahakama kuwa, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) amewasilisha hati ya kuwaondolea baadhi ya washtakiwa mashtaka yao kwa sababu hana nia ya kuendelea na kesi dhidi yao

Washtakiwa hao saba wamefutiwa kesi hiyo chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai  (CPA), sura ya 20 , iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Kufuatia taarifa hiyo, Hakimu Simba  amesema kupitia kifungu hicho kilochowasilishwa,  mahakama hiyo imewafutia mashtaka washtakiwa hao saba na imewaachia huru.

Waliofutiwa  mashtaka ni Samwel Nyakirang'ani(63)ambaye ni  mfanyakazi mstaafu wa Shirika la Mafuta Tanzania na Zambia(Tazama), ) na Nyangi Mataro( 54) ambaye ni mwalimu wa shule ya  msingi Ufukoni na mkazi wa Kisiwani Mkajuni Kigamboni.

Wengine ni Farijia Ahmed(39)mkazi wa Soko Maziwa Kigamboni;  Malaki Mathias(39) mkazi wa Magogoni; Kristomsi Angelus(25) mkazi wa Soko Maziwa;  Fundi Ujenzi Pamfili Nkoronko(40) mkazi wa Tungi Kasirati na Henry Fredrick (38) mkazi wa Tungi Kigamboni.

Kuhusu mshtakiwa waliobaki ambao wa nane hadi wa 12, upande wa mashtaka umedai, unaendeleaje kulifanyia kazi jalada hilo na  upelelezi wakei  bado haujakamilika.

Mwita amewaja washtakiwa ambao bado wanashikiliwa kuwa ni, Audai Ismail (43) ambaye ni mkazi wa Kibaha, Chibony Emmanuel, Roman Abdon, Amina Shaban na Zubery Ally.

Washtakiwa hao watano, wamerudishwa rumande hadi Februari 21, 2019 kesi hiyo itakapotajwa.

Inadaiwa kuwa kati ya mwaka 2015 hadi Januari 8, 2018 katika eneo la Tungi Muungano wilaya ya Kigamboni, washtakiwa wanadaiwa kujiunganishia bomba la mafuta ya dizeli lenye upana wa inchi moja kutoka katika bomba lenye upana wa inchi 24, bila kuwa na kibali.

Katika shtaka la pili ambalo ni kuharibu miundo mbinu, inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa walitoboa bomba la hilo, ambalo lilikuwa likitumika kufirisha mafuta,  mali ya Mamlaka ya Bandari nchini( TPA).

Pia wanadaiwa kuharibu bomba la mafuta mazito( Crude oil) lenye upana wa inchi 28, ambalo lilikuwa likitumika kusafirisha mafuta ghafi, mali ya Mamlaka ya Bandari nchini( TPA).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad