HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 18 February 2019

WALIMU WA WATAKIWA KUTUMIA ZAIDI ZANA ZA KUFUNDISHIA NA KUJIFUNZIA WANAPOFUNDISHA

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar 
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma amesema wakati umefika sasa kwa walimu wa skuli kutumia zaidi zana na vielelezo katika kufundisha wanafunzi badala ya kutumia chaki, mdomo na ubao pekee.

Alisema iwapo vitendea kazi na vielelezo vitatumika vizuri na kwa muda sahihi kuna uwezekano mkubwa kiwango cha ufahamu kwa wanafunzi wengi kuongezeka na kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya Taifa na kuinua kiwango cha elimu.

Waziri wa Elimu alitoa maelezo hayo Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Nkrumah kwenye ufunguzi wa Maonyesho ya zana za kufundishia na kujifunzia katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Idrissa Muslim Hija.

Alisema matumizi ya zana na vielelezo ni muhimu sana katika kumuandaa mwanafunzi kukabiliana na mitihani yake na amebainisha kuwa utaratibu uliozoeleka wa mwalimu kukaa mbele ya darasa na chaki ni potofu kwa sasa na inachangia kushuka kiwango cha elimu. 

Alishauri kutumika mpango wa Maendeleo  ya Elimu ya kutengeneza na kutumia zana zinazopatikana katika mazingira yaliyotuzunguka ambazo zinagharama nafuu.

Alisema vifaa hivyo vilivyotengenezwa na wanafunzi wanaosoma kada ya ualimu Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar  vinatrajiwa kuwa suluhisho kwa baadhi ya wanafunzi wa skuli wenye ufahamu mdogo katika masomo.

Aliongeza kuwa Serikali inaendelea kufanya juhudi ya kuongeza vifaa vya kufundishia na kujifunzia lakini kutokana na idadi ya wanafunzi kuongezeka kwa kasi, kuna umuhimu kwa walimu waliopatiwa mafunzo ya kutengeneza vifaa hivyo kuuedeleza katika skuli watakazo pangiwa baada ya kumaliza chuo.

Mkuu wa Skuli ya Elimu ya SUZA Dk. Maryam Jaffar Ismail alisema wanafanya juhudi ya kuwaandaa walimu wanaosoma chuoni hapo kutengeneza zana za kusomeshea kwa kutumia vitu vilivyopo katika mazingira yaliyowazunguka ambavyo havina gharama kubwa ili kuwasaidia wanafunzi wao na kuongeza ufanisi katika kazi hiyo.

Alisema tokea walipoanza mpango huo miaka mitano iliyopita ufanisi wa kutengeneza vifaa umekuwa ukiongezeka na wamekuwa kigenzo kwa vyuo vikuu vya nchi jirani kutaka kuja kujifunza .

Akielelezea changamoto inayoikabili kada ya elimu nchini ni vijana wengi kukataa kujiunga na kada hiyo na wanaojiunga ni vijana wanaokosa  masomo katika fani nyengine jambo ambalo alisema sio sahihi.

Akitoa neno la shukrani katika maonyesho hayo, Mkufunzi wa Mradi wa kutengeneza zana za kufundishia na kujifunzaia wa SUZA Maalim Said Yunus alisema vifaa vyote wanavyotumia kutengeneza zana za kufundishia na kujifunzia vinaweza kupatikana sehemu yeyote ya Zanzibar bila kutumia gharama kubwa.

Alisema hatua ya kutengeneza zana hizo itaziba pengo la upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia  unaozikabili skuli nyingi za Zanzibar ambavyo vimekuwa vikiagizwa na Serikali kwa gharama kubwa.
 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Dk. Idrissa Muslim Hija akipata maelezo ya chombo kinachotumika kupitisha umeme kutoka kwa mwanafunzi Husna Sharif wa Sekondari ya SUZA katika maonyesho ya zana za kufundishia na kujifunzia yaliyofanyika Kampasi ya Nkrumah.
  Mkufunzi wa somo la kutengeneza zana za kufundishia na kujifunzia wa SUZA Maalim Said Yussuf akieleza Mradi huo unavyoendelea kuwaandaa walimu wanafunzi wanaosomo chuoni hapo katika maonyesho yaliyofanyika Kampasi ya Nkrumah.
  Baadhi ya walimu wanafunzi wanaosoma SUZA wakifuatilia ufunguzi wa maonyesho ya zana za kufundishia na kujifunzia yaliyofanyika Kampasi ya Nkrumahi
 Mkuu wa Skuli ya Elimu ya SUZA Dk. Maryam Jaffar Ismail akizungumza katika ufunguzi wa maonyesho ya zana za kufundishia na kujifunzia yaliyofanyika Kampasi ya Nkrumah.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Taasisi mbali mbali za Zanzibar na Tanzania Bara walioalikwa ufunguzi wa maonyesho ya zana za kufundishia na kujifunzia yaliyofanyika Kampasi ya Nkrumah. Picha na Ramadhani Ali

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad