HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 26 February 2019

RAIS WA ZANZIBAR DK.SHEIN AFUNGUA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI LEO UKUMBI WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  amesema kuwa suala la kupambana na rushwa lina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa ikizingatiwa kwamba vitendo hivyo vinazorotesha uchumi na maendeleo.

Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani mjini Zanzibar wakati akizindua Mkutano wa Nne wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) ambapo kwa mwaka huu unafanyika hapa Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa Mswada wa rushwa katika mkutano wa Bunge hilo mwaka huu kuna umuhimu mkubwa kwani utasaidia katika kupambana na vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikiathiri sana uchumi na maendeleo ya nchi na wananchi wake.

Amesema kuwa Mkutano huo ambao katika Miswada yake ambapo miongoni mwao kutakuwepo Mswada huo ambao utajadiliwa unakwenda sambamba na juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na nchi wanachama katika kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu wa uchumi.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika jitihada zake za kukomesha vitendo vya rushwa imeunda Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kwa lengo la kushughulikia suala zima la kupambana na rushwa.

Alisema kuwa juhudi hizo zinaendelea kwa mashirikiano ya pamoja na wananchi hatua ambayo imepelekea Mamlaka hiyo kuweza kupiga hatua kubwa.

Aliongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli imeongeza juhudi zaidi katika kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kuweka mikakati mbali mbali.

Alisema kuwa Serikali zote mbili ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeimarisha usimamizi wa sheria na kuongeza Bajeti katika sekta ya sheria sambamba na kuongeza wataalamu ili kusimamia kesi zinazohusiana na rushwa.

Hivyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa juhudi hizo zitasaidia sana pamoja na zile sheria zitakazotungwa na Bunge hilo ambazo zote kwa pamoja zinaweza kufikia lengo lililokusudiwa.

Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza suala zima la kuzingatia umhimu wa maadili na tabia njema katika kutekeleza majukumu ya viongozi hao hasa katika wakati huu ambao teknolojia na mifumo ya maisha imebadilika na baadhi ya wakati hupelekea Wabunge kufanya vitendo ambavyo vinahitaji umakini na maamuzi ya busara ili waweze kulinda hadhi yao.

Alisema kwamba inatia moyo kuona kwamba Ukanda wa Afrika Mashariki ni miongoni mwa Kanda zinazoongoza katika ukuaji mzuri wa uchumi duniani ambapo katika mwaka wa 2017 uchumi ulikuwa kwa asilimia 4.6 ikilinganishwa na mwaka 2016 ambapo uchumi ulikuwa asilimia 4.4.

Alieleza kuwa hayo ni mafanikio makubwa ambayo yanapaswa kuendelezwa  huku akisisitiza kuwa kutokana na Afrika ya Mashariki kuwa na zaidi ya watu milioni 162 hali hiyo inapelekea kuwepo kwa soko kubwa la bidha mbali mbali pamoja na huduma muhimu.

Pia, alieleza kuwa Afrika Mashariki ina ardhi kubwa yenye kilomita za mraba 1.82 milioni ambayo ni vyema rasilimali hiyo ikatumika vizuri ili iweze kuleta tija kwa nchi wanachama.

Vile vile, Rais Dk. Shein alipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na nchi wanachama katika kuhakikisha kwamba Jumuiya hiyo inafikia malengo yake hasa katika suala zima la kukuza uchumi, uimarishaji wa utawala Bora, uismarishaji wa sheria pamoja na uimarishaji wa amani na utulivu.

Rais Dk. Shein ameeleza kutiwa moyo sana na juhudi za Umoja huo za kuimarisha lugha ya Kiswahili ambayo hivi sasa imekuwa ni lugha inayounanisha wanachama katika shughuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii.

Alieleza kuwa Zanzibar inathamini sana fursa iliyopewa ya kuwa Makamo Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na kuahidi kuwa fursa hiyo itaitumia vizuri ili kuhakikisha malengo yaliokusudiwa yanafikiwa.

Dk. Shein alimuhakikishia Spika wa Bunge hilo Martin Ngonga kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuendeleza na kuitangaza lugha ya Kiswahili na kufahamisha kwamba kupitia Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) imekuwa ikiandaa makongamano mbali mbali ya Kiwahili ambayo yanajumuisha wataalamu kutoka sehemu mbali mbali duniani.

Alisema kuwa hatua hiyo ina lengo la kukiimarisha na kukuza matumizi sahihi ya Kiswahili fasaha kwa kuangalia kwamba Zanzibar ndio chimbuko la Kswahili sanifu.
Rais Dk. Shein alisema anaamini kwamba Jumuiya hiyo inaweza kuwa eneo muhimu la kiuchumi duniani, hivyo jitihada zaidi zinahitajika katika utekelezaji wa malengo makuu yaliopangwa na Jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kushajiisha uekezaji, kuendeleza sekta ya utalii, viwanda, elimu na kutilia mkazo  suala zima la kuongeza ajira na kuimarisha miundombinu.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein aliitaka Jumuiya ya Afrika Masharik kupitia Bunge lake hilo kuchukua jitihada katika kupambana na vitendo mbali mbali vyenye kuathiri uchumi ikiwemo suala zima la utakasishaji wa fedha.

Vile vile, Rais Dk. Shein alieleza haja ya kuendeleza teknolojia ya Habari na Mawasiliano huku akiwasisitiza Wabunge wa Bunge hilo kufanya kazi kwa mashirikiano mazuri na Mabunge mwengine ya nchi wanachama ili kuweza kufanya kazi kwa ufanisi mzuri zaidi.

Aidha, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kulipongeza Bunge hilo kwa kufanya mkutano wake huo hapa Zanzibar na yeye kupata fursa kwa mara ya pili kuufungua mkutano huo na kutoa shukurani zake kwa kuweza kukaa pamoja na chombo hicho muhimu cha kutunga Sheria.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Spika wa Bunge hilo kwa  kuchaguliwa kuwa Spika wa tano na kuweza kukiongoza chombo hicho huku akiwapongeza Wajumbe wote wa Bunge hilo kwa kuchaguliwa kukiongoza chombo hicho muhimu katika Afrika Mashariki.

Pamoja na hayo, alisifu utaratibu wa Bunge wa kufanya mikutano katika miji ya nchi wanachama jambo ambalo linapelekea wananch kufahamu majukumu ya chombo hicho ambapo alisema utaratibu huo unaenda sambamba na falsafa ya kuweka umoja na mshikamano kwa watu wa Afrika Mashariki.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein ameleza kufurahishwa kwake na moja ya Miswada ambayo itajadiliwa katika Bunge hilo ambayo ni pamoja na Mswada wa vita dhidi ya rushwa, masuala ya kijinsia,ulemavu pamoja na mada nyengine zitakazojadili vitendo vya ugaidi vilivyojitokeza nchini Kenya.

Nao Wabunge hao walitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa heshima kuwa aaliyowapa ya kwenda kuzindua mkutano wao huo na kueleza kufurahishwa kwa kiasi kikubwa na hotua aliyoitoa ambayo imewapa matumaini makubwa.

Nae Spika wa Bunge hilo Martin Ngoga alitoa shukurani kwa Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na uongozi wake chini ya Spika wa Baraza hilo Zubeir Ali Maulid kwa mashirikiano mazuri wanayoyapata ambayo ni chachu katika utekelezaji wao wa kazi.

Aidha, Spika huyo alieleza umuhimu wa lugha ya Kiswahili katika Umoja huo pamoja na Wajumbe wa Bunge hilo na kueleza mikakati waliyoiweka katika kuhakikisha lugha hiyo inatumika vyema ndani ya Bunge hilo pamja na nchi zote za Jumuiya hiyo.

Nae Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid alieleza mashirikiano mazuri yaliopo kati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Bunge hilo Afrika Mashariki na kueleza mafanikio makubwa yaliopatikana katika mashirikiano hayo.
Katika uzinduzi huo wa Mkutano wa (EALA) ambao unatarajiwa kuwa wa siku 10 moja, viongozi mbali mbali walihudhuria akiemo Spika wa Bunge hilo Martin Ngoga, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Wenyeviti na Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zubeir Ali Maulid, Spika Mstaafu Pandu Ameir Kificho, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wajumbe wa Bunge hilo la Afrika Mashariki.
 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akikagua gwaride maalum llililoandaliwa kwa ajili ya Ufunguzi wa Bunge la Afrika Mashariki katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.(Picha na Ikulu)
 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Martin Ngoga, alipowasili katika viwa vya Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.(Picha na IKULU)
 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Martin Ngoga wakiingia katrika ukumbi wa Mkutano kwa ajili ya Ufunguzi.(Picha na Ikulu)
  RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Afrika Mashariki lililofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar leo.(Picha na Ikulu)

Baadhi ya wabunge wa bunge la Afrika Mashariki wakisikiliza hotuba  ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar leo.(Picha na Ikulu)

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad