HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 26, 2019

NAIBU WAZIRI NISHATI ATAKA BUSARA ITUMIKE KUUNGANISHA UMEME VIJIJINI

Na Veronica Simba – Nachingwea
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kutumia busara katika kazi hiyo ili iwaongoze kufanya maamuzi sahihi hususan uunganishaji umeme katika taasisi na miradi ya umma. Alitoa wito huo kwa nyakati tofauti jana, Februari 25 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi.

Akizungumza ofisini kwa Mkuu wa Mkoa na baadaye katika vijiji vya Kihuwe, Muungano na Mapochero, ambavyo aliviwashia umeme rasmi; Naibu Waziri alisisitiza kuwa pamoja na kila mkandarasi kuwa na wigo wa eneo analopaswa kuunganisha umeme, lakini siyo busara kwake kuruka taasisi za umma na miradi muhimu kama vile ya maji, afya na mingineyo kwa sababu tu iko nje ya wigo.

“Unafika eneo, unaona Zahanati ile pale, akina mama wanajifungua gizani; Shule ile pale, kuna hosteli, unaziachaje bila umeme sababu tu hazipo ndani ya wigo! Mkandarasi unapaswa kutumia busara, ikibidi tuandikie sisi Serikali, tuone namna gani gharama husika zitalipwa ili maeneo kama hayo yasikose umeme,” alisema.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alisema kuwa serikali inaendelea kujivunia kugundulika kwa gesi katika mikoa ya kusini na kwamba watanzania wanapaswa kufahamu kwamba serikali imedhamiria kuitumia ipasavyo.

Akifafanua, alisema gesi inapaswa itumike katika viwanda vya mbolea, majumbani na katika kuzalisha umeme. Hivyo, aliwataka wananchi kupuuza maneno yanayosemwa na baadhi ya watu kuwa serikali haitoi tena kipaumbele kwa gesi iliyogunduliwa mikoa ya kusini.

Naibu Waziri alifafanua zaidi kuwa, ili kupata umeme mwingi, wenye bei nafuu na wa uhakika; ni lazima serikali ihakikishe inatumia vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ikiwemo maji, upepo, jua, gesi, tungamotaka na vinginevyo.

“Ndiyo maana tunaanzisha miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme ambayo inatumia vyanzo mbalimbali, siyo gesi peke yake. Ni muhimu mkalitambua hilo kwamba, kama nchi, hatuwezi kutumia gesi peke yake katika kuzalisha umeme, tukaacha vyanzo vingine. Inabidi tutumie vyanzo vyetu vyote tulivyojaaliwa na Mungu.”

Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme maeneo mbalimbali ya nchi hususan vijijini, Naibu Waziri alisema kazi hiyo inaendelea kufanyika  kwa ufanisi ambapo sasa serikali imewaelekeza wakandarasi wa miradi hiyo kuhakikisha wanawasha umeme katika vijiji vitatu kila wiki kwa kila mkandarasi.

Hata hivyo, aliwataka wananchi kuwa na subirá kwani kazi ya kuunganisha umeme inatekelezwa hatua kwa hatua.

Naibu Waziri anaendelea na ziara yake mkoani Lindi ambapo amefuatana na wataalamu mbalimbali kutoka wizarani, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kihuwe, Wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi, Februari 25, 2019, akiwa katika ziara ya kazi, ambapo pia aliwasha rasmi umeme katika kijiji hicho.
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mwenye kinasa sauti) akifurahi pamoja na wananchi wa kijiji cha Kihuwe, Wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi, Februari 25, 2019, mara baada ya kuwasha rasmi umeme katika kijiji hicho.
 Sehemu ya umati wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Namatula, iliyopo wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao, kabla ya kuwasha rasmi umeme katika shule hiyo, Februari 25, 2019.
 Baadhi ya wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na REA wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Muungano, wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi, Februari 25, alipokuwa katika ziara ya kazi ambapo aliwasha rasmi umeme katika kijiji hicho.
 Mkazi wa Kijiji cha Kihuwe, wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi, Samwel Ndungo akiuliza swali na kueleza changamoto kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), alipofika katika kijiji hicho kuwasha rasmi umeme na kuzungumza na wananchi, akiwa katika ziara ya kazi, Februari 25, 2019.
 Mkazi wa Kijiji cha Kihuwe, wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi, William Hassan akiuliza swali na kueleza changamoto kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), alipofika katika kijiji hicho kuwasha rasmi umeme na kuzungumza na wananchi, akiwa katika ziara ya kazi, Februari 25, 2019.
Mkazi wa Kijiji cha Kihuwe, wilayani Nachingwea, Mkoa wa Lindi, Matthew Ntunga akiuliza swali na kueleza changamoto kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), alipofika katika kijiji hicho kuwasha rasmi umeme na kuzungumza na wananchi, akiwa katika ziara ya kazi, Februari 25, 2019.
Sehemu ya umati wa wananchi wa kijiji cha Mapochelo, Wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji hicho, Februari 25, 2019 alipokuwa katika ziara ya kazi ambapo pia aliwasha rasmi umeme katika kijiji hicho.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad